24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA ALAANI KONGAMANO KUZUIWA

Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana kuhusu kuahirishwa kwa Kongamano la Kidemokrasia lililokuwa lifanyike jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Dk. Makongoro Mahanga. PICHA: SILVAN KIWALE

 

 

Na AGATHA CHARLES, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesikitishwa na Rais Dk. John Magufuli kutohudhuria shughuli za mazishi ya wanafunzi 33 wa darasa la saba wa Shule ya Msingi ya St. Lucky Vincent, walimu wao wawili na dereva mmoja wa basi, pia akasema kutokana na kitendo hicho, hana mgogoro naye, lakini watu wa Arusha kimewafanya wawe wanyonge.

Lowassa, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitoa kauli hiyo ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam jana, alipokutana na waandishi wa habari na kuzungumzia mambo manne, likiwamo la kuzuiliwa kwa Kongamano la Demokrasia na Siasa za Ushindani lililotarajiwa kufanyika jana katika Ukumbi wa Anatoglou, uliopo Ilala. 

“Nilichosikitika na wakazi wengi wa Arusha ni kitendo cha Rais Magufuli kutohudhuria shughuli za mazishi,  kimeniuma na badala yake kumtuma Suluhu (Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan), sina mgogoro na Rais hata kidogo, lakini nasema kuna msemo unasema shughuli hatumwi mtoto. Hii haikuwa shughuli ya kumtuma mtoto, Amiri Jeshi Mkuu ni mfariji mkuu, watu wa Arusha walijisikia wanyonge sana, kwamba Rais kwenye tukio kama lile anashindwa kuungana nasi,” alisema.

Lowassa alitoa mfano wa namna Malkia Elizabeth wa Uingereza alivyoungana na raia wake na kuagiza askari aliyeuawa katika tukio la kigaidi kuzikwa kitaifa na kuhudhuria mazishi hayo kuwa ni kuonyesha umoja na kuhuzunika pamoja.

Alisema Magufuli alishindwa kuhudhuria shughuli za msiba huo uliotokana na ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu, baada ya basi la shule hiyo walilolipanda kutumbukia katika korongo lililopo Marera, eneo la Rotia, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, lakini hakukuwa na taarifa iliyowekwa hadharani kueleza sababu iliyomzuia.

VYETI, MITANDAO YA KIJAMII

Katika hatua nyingine, alisema hatetei baadhi ya watumishi wa umma kubainika kuwa na vyeti feki, lakini anataka ubinadamu utumike wanapofukuzwa, hasa suala la mafao yao.

Lowassa alitoa kauli hiyo wakati akipongeza ukuaji wa mitandao ya kijamii unavyosaidia kutoa taarifa na kuwataka wasikubali kuminywa, bali waendelee kama ilivyo kwa upande wa magazeti.

Alisema katika suala hilo wapo watu waliofanya kazi kwa miaka mingi, hivyo wanaponyimwa mafao pamoja na mshahara wa mwisho wa mwezi huo wanakosa la kufanya.

“Ukisoma hotuba za viongozi zinatisha na kutia hofu, natumia hofu kwa maana halisi ya hofu, kwa mfano kuwafukuza wafanyakazi zaidi ya 9,000 kwa wakati mmoja, wanakwenda wapi? Vyeti feki, wala siwatetei, nauliza ubinadamu, watu hawa 9,000 wananyimwa mishahara yao, wananyimwa mafao yao waliyojiwekea kwa miaka 20, miaka 40, sawa amekosea, amekosea sana lakini mafao ya mtu,  anakwenda wapi, amemwacha nyumbani mke, ana watoto wadogo, na mjomba amekuja kusalimia.

“Watoto wako shule anarudi nyumbani hana kazi, hana mshahara wa mwezi ule na hana mafao, hata kama amekosa tunahitaji ubinadamu, moyo wa huruma, sawa amekosa mimi simtetei kosa lake, natetea na ubinadamu wake kwamba ingenifika mimi leo ningefanya nini,” alihoji.

Katika hilo, alisema wafikiriwe wazee kwa vijana waliotoa utumishi kwa nchi kwa uaminifu kwa sababu shule nyingi zitakosa walimu kama hatua zisipochukuliwa.

Pia alisema kuna wakunga vijijini ambao huwa wanakaa huko porini kufanya kazi kwa uaminifu, ingawa wanakuwa hawana elimu, lakini baada ya uzoefu hufanya kazi zao vyema pamoja na wauguzi wanaojituma na kupanda vyeo, hivyo wafikiriwe kibinadamu.

“Kibinadamu wametumika miaka 20, miaka kadhaa, mimi kuna mtu mmoja namjua, amemaliza kidato cha nne.

Lakini anasema alipokwenda kuomba kazi ya udereva aliambiwa kupeleka cheti cha NIT (Chuo cha Taifa cha Usafirishaji) ndiyo kigezo chake cha kupata udereva, sasa hii form four (kidato cha nne) niliyopita na kufeli, tafadhali nawaomba hao ni Watanzania hawana sehemu ya kwenda,” alisema.

MAFURIKO

Kuhusu mafuriko, alisema yalifuatana na kipindi cha ukame mkubwa na kusababisha wananchi kuathirika.

Hata hivyo, alisema anasikitika kutouona mkono wa Serikali wala kiongozi wa Serikali akiwapa wananchi matumaini, kuwapoza na kuwapa pole.

“Wananchi wanapata tabu kweli, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu bei ya mahindi imepita ya mchele, maharage bei juu, unga bei juu, everything (kila kitu) ni bei juu, there is problem (kuna tatizo),” alisema.

Lowassa alisema kuna maeneo Kagera wilayani Bukoba hayana mawasiliano kutokana na kukatika kwa barabara, huku wananchi wengine wakiwa hawajui watalala vipi.

“Serikali inafanya nini, tunasaidiaje wananchi kuishi kwa matumaini? Naiomba Serikali itangaze na ichukue hatua kuhusu hali ya chakula,” alisema.

Pia aliwapongeza wabunge waliojitokeza na kuzungumzia suala la maafa ya mafuriko yanayoendelea sehemu mbalimbali.

Kongamano

Akizungumzia kongamano hilo, alisema lilikuwa na lengo la kuwaleta Watanzania pamoja, kuzungumzia demokrasia na waandaaji waliweka picha akiwa na Kinana wakitabasamu kwa kuwa nchi ni moja na watu ni wale wale.

Lowassa alisema hata wakati wa Tume ya Nyalali, watu walihofu mfumo wa vyama vingi, lakini lugha iliyotumika ilikuwa nzuri ya tupingane bila kupigana.

Kutokana na kongamano hilo kuzuiwa kufanyika, Lowassa, aliyekuwa ni mwenyekiti wake, alisema wanalaani kwa nguvu zote kitendo cha kuminya demokrasia.

“Tunajenga nchi moja, watu wale wale, kila mtu ana haki ya kuwa na maoni yake, iko siku nchi itatawaliwa na wengine, si CCM kila siku, kama hatutakuwa sisi watakuwa watoto wetu,” alisema.

Lowassa alisema ana masikitiko kwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuvunja kongamano hilo na kwamba hivi sasa vyama vingi vilivyopigania uhuru havipo tena madarakani, hivyo iwapo Chadema wana makosa yanapaswa kuwekwa wazi.

Akijibu swali la waandishi kuhusu kauli ya Magufuli aliyoitoa Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwa amewasamehe wananchi wa mkoa huo, Lowassa alisema Rais alipaswa kusema amewasamehe kwa lipi?

Alisema yeye anatafuta njia ya kuwashukuru wananchi, lakini hapatiwi, lakini Rais ambaye anatumia kodi za wananchi anaruhusiwa.

“Rais anatumia gari na ndege za Serikali kwenda kuwashukuru wapiga kura wake lakini eti ni dhambi kwa Lowassa kwenda mikoani kuwashukuru walionipigia kura, hata kama anatumia gharama zake za kutoka mfukoni, lakini yeye anakwenda kwa kodi za wananchi tena na kuwaambia amewasamehe eti kwa kumpa Lowassa kura, hii siyo sawa,” alisema.

Pia alitoa pole kwa familia ya aliyekuwa Katibu wa Kwanza wa Rais (Ikulu- Habari) wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa na ile ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, ambao wote walifariki dunia juzi katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) walikokuwa wakipatiwa matibabu.

Naye Kiongozi wa Waandaaji wa kongamano hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilala, Dk. Milton Mahanga, alisema mwaliko wa kadi ya kwanza na ya pili ulikwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles