Charles Mullinda na Jimmy Charles, Dodoma
HATIMAYE Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana alivunja ukimya wa muda mrefu alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Katika mkutano huo,Lowassa aliitumia nafasi hiyo kutangaza msimamo wake wa siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa aliitumia fursa ya mahojiano hayo, yaliyofanyika nyumbani kwake eneo la Area C mjini hapa, kuwaeleza wahariri kuwa hana mpango wa kuhama CCM licha ya kuwapo shinikizo la chini kwa chini la kumtaka aondoke na kwamba wale wote wanaomtaka au wanaotamani aondoke, wanapaswa kuondoka wao.
Kauli hiyo aliitoa wakati akijibu swali iwapo CCM hakitamteua kuwa mgombea urais atachukua uamuzi gani kwa sababu jina lake limekuwa likihusishwa na mpango wa kukihama endapo jina lake halitapitishwa.
Alisema maisha yake yote ya siasa yamekuwa ndani ya CCM na kauli zinazomuhusisha na kuhama chama hicho, amekuwa akizisikia na kuzipuuza kwa sababu jambo hilo hawezi kulifanya.
“Nimekuwa mwanachama wa CCM tangu mwaka 1975, maisha yangu yote ya siasa yamekuwa ndani ya chama hiki isipokuwa muda mfupi ambao nilikwenda kupigana vita Uganda na nilipokuwa nikifanya kazi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (IACC). Sitahama chama isipokuwa wasionitaka waondoke wao,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye alikataa kujibu baadhi ya maswali ya wahariri waliotaka kujua iwapo minong’ono ya muda mrefu inayohumusisha na kuwania urais ni ya kweli, alisema suala hilo litajulikana Jumamosi, Mei 30 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Alisema hapo atatoa hotuba ya kuanza kwa safari ya matumaini huku akisisitiza ana uhakika na anakichofanya na hana mpango mwingine mbadala isipokuwa wa mafanikio.
Akizungumzia tetesi ambazo zimekuwa zikisambaa kwa muda mrefu sasa kuhusu kulegalega kwa uhusiano wake na Rais Jakaya Kikwete, Lowassa alieleza kushangazwa na hilo na kuhoji msingi wa baadhi ya watu kuzungumzia urafiki binafsi kati yake na Kikwete.
Alisema tangu alipojiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu 2008, amesikia mengi yakisemwa kwa uzuri na ubaya kumuhusu yeye, likiwamo la kulegalega uhusiano wake na Kikwete, lakini aliamua kuwa kimya kwa sababu kunyamaza ni hekima.
Alisema mbali na taarifa hizo alizoziita za upotoshaji kuhusu uhusiano wake na Rais Kikwete kuzorota, zipo nyingine nyingi za aina hiyo ambazo zimekuwa zikiibuliwa na kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa sababu za uhasama na chuki za siasa.
“Tangu nilipoondoka kwenye uwaziri mkuu, nimekuwa kimya kwa sababu wakati mwingine kunyamaza ni hekima. Niliamua kuwa kimya kwa vile niliogopa upotoshaji. Siasa zetu hapa nchini zimekuwa za chuki, uhasama na kusingiziana na inatupa shida kweli, nikaamua kunyamaza.
“Sasa wanaozusha kuwa uhusiano wangu na Rais Kikwete umezorota wamepata wapi? Hili suala la urafiki wangu na rais acheni kulipotosha,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alizungumzia pia minong’ono ambayo imekuwa ikimuhusisha na kujilimbikizia mali pamoja na ushiriki wake katika harambee hususan anazoalikwa kwenye nyumba za ibada na kiwango cha fedha anachochangia.
Alisema wote wanaodhani amejilimbikizia mali kwa njia za ufisadi wafuatilie jambo hilo kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Akifafanua hilo, alisema amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 20 na kwa mujibu wa mila na utamaduni wa jamii yake, kiongozi lazima awe na mali hasa ng’ombe na nyumba.
“Nina mali, nina nyumba na ng’ombe kati 800 na 1,200, mwenye shaka na mali zangu aende kamati ya maadili. Lakini katika jamii yangu kiongozi ni lazima uwe na mali na mimi nachukia sana umaskini na Watanzania tusikumbatie umaskini. Utajiri si dhambi na mimi natafuta uongozi ili kuuondoa umaskini wa Watanzania,” alisema Lowassa.
Kuhusu ushiriki wake katika harambee na kiasi cha fedha anazochangia, alisema utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo umesaidia jamii nyingi za watu katika maeneo mbalimbali duniani kufanikisha malengo yao,
Alisema kwa kutambua hilo amekuwa mstari wa mbele kushiriki na kuhamasisha watu kuchangia.
“Jirani zetu wa Kenya, wamefanikiwa sana katika baadhi ya mambo yao kwa sababu ya harambee za aina hii na ndiyo maana mimi pia nimekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu kuchangia shughuli zao za maendeleo.
“Sina fedha kama hizi zinazosemwa lakini nina marafiki. Hawa ndiyo ninaowatumia kufanikisha malengo ya harambee ninazoshiriki ingawa hili nalo limekuwa likipotoshwa kama ilivyotokea juzi juzi hapa watu wakasema nimeita watu 300 na kuwakaribisha hapo mlipokaa ninyi. Angalieni wenyewe eneo hili mlipo kweli wanaweza kuingia idadi hiyo ya watu?” alisema Lowassa.
AFYA YAKE
Akizungumzia suala la afya yake, Lowassa alisema yuko fiti kwa chochote kile na amekiomba chama chake kuweka utaratibu wa kuwapima afya makada wake wote wanaoutaka urais.
“Niko fiti, wanaosema naumwa ni wazushi, siasa zimekuwa za uhasama, kusingiziwa na kutafutana hata nikikimbia kilomita 100 watasema Lowassa mgonjwa. Nilikimbia kilomita tano ikaandikwa nimekwimbizwa Ujerumani kutibiwa.
“Mimi nakiomba chama kiweke utaratibu wa watu wote wanaotaka urais wapime afya zao, niko fiti na niko tayari kwa chochote, tukutane kwenye uwanja wa mapambano,” alisema.
UWAZIRI MKUU
Alipoulizwa kama angeendelea kuwa waziri mkuu hadi leo Serikali ya awamu ya nne ingekuwaje, Lowassa alisema hali ingekuwa tofauti kabisa na anaamini kamwe asingekuwa na kazi ya kuomba kura kwa sababu angepita bila kupingwa.
“Nadhani tungekuwa tunaongea mambo mengine leo wala nisingeomba kura, ningepita barabarani na kupunga mkono tu,” alisema.
TATIZO LA AJIRA
Kuhusu tatizo la ajira nchini, mbunge huyo wa Monduli alisisitiza kuwa ni bomu na lisiposhughulikiwa mapema litalipuka.
“Vijana wengi kujiingiza kwenye biashara ya bodaboda ni kielelezo cha ukosefu wa ajira, suala hili kwangu ni kipaumbele namba moja, mbili na tatu,”alisema.
NGUVU YA UPINZANI
Kuhusu nguvu ya vyama vya siasa vya upinzani nchini, alisema upinzani umeanza kupata nguvu mijini na vijijini, hivyo chama tawala kisibweteke wala kufanya mchezo na upinzani.
“Hata hivyo,Rais Kikwete amejitahidi kutekeleza ilani ya chama kwa kiasi kikubwa, hilo linaweza kukisaidia chama,”aliongeza.
SAKATA LA RICHMOND
Kuhusu suala la Richmond, Lowassa alisema hakuna haja ya kulizungumzia suala hilo kwa sababu limeshasemwa na kuandikwa sana, ingawa anaamini hakukuwa na makosa kwenye mkataba wa mitambo hiyo na hata Rais wa Marekani,Barack Obama na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hilary Clinton walisema mitambo hiyo haina shida.
“Suala la Richmond sioni haja ya kulizungumzia zaidi, limeshasemwa na kuandikwa sana lakini mnapaswa kujua ubishi ule umerigharimu taifa Dola za Marekani bilioni 120, hata hivyo nilijua tatizo si Richmond, tatizo lilikuwa ni uwaziri mkuu,” alisema.
VIPAUMBELE
Kwa upande wa vipaumbele vyake, alisema kwake elimu kwanza, kilimo baadaye na kwamba hakubaliani na mpango wa Kilimo Kwanza.
“Mataifa mengi yaliyoendelea yaliwekeza zaidi kwenye elimu, ukiwekeza kwenye eneo hilo ni rahisi kuendelea.
“Nawaambieni kweli tukiwekeza kwenye elimu tutaibadili nchi hata tatizo la ajira litakwisha.
VISASI
Kuhusu visasi, Lowassa alisema hana kisasi na mtu, hata dini yake haimruhusu na inamtaka kusamehe saba mara sabini.
“Sina kisasi na mtu na sina mpango wa kufukua makaburi, naomba tuchape kazi na kujenga nchi yetu.
Tangu alipojiuzulu uwaziri Mkuu mwaka 2008 Lowassa hakupata kujitokeza hadharani kuzungumza na vyombo vya habari.
Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa katika kipindi cha takriban miaka saba sasa, kujitokeza mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kujibu na kutoa ufafanuzi wa mambo ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake.
Majibu ya Lowassa aliyoyatoa jana kwa wahariri kuhusu tuhuma na madai mengi ambayo yamekuwa yakimuandama, yamekuwa mjadala kwa kipindi chote cha takriban miaka saba ya ukimya wake na yamekuwa yakitafsiriwa kwa namna tofauti tofauti na mashabiki na wapinzani wake wa siasa.