27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU: NI TUKIO LA MAUAJI YA KISIASA

NA MWANDISHI WETU, Nairobi

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema  anaamini tukio lake la kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana lililotokea Septemba 7, mwaka jana, ni la kisiasa.

Akizungumza mjini hapa jana na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, Lissu ambaye pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kesho anatimiza miezi minne tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Nairobi kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi nyumbani kwake eneo la Area D, mjini Dodoma, alidai kuwa kilichofanyika siku hiyo lilikuwa ni jaribio la mauaji aliyoyahusisha na masuala ya siasa.

“Mimi si mfanyabiashara kusema nimemrusha mtu fedha zake na huwa sipigani baa, lakini tangu mwaka 2010 nimekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Tanzania na kuanzia mwaka 2015 nimekuwa mkosoaji mkubwa wa sera na matendo ya Serikali,” alisema.

Kwa mujibu wa Lissu aliyezungumza katika eneo la bustani ya hospitali hiyo baada ya kuruhusiwa kwenda kutibiwa katika moja ya nchi za Ulaya ambayo hakuitaja, alisema Jeshi la Polisi halijawahi kutoa taarifa rasmi kuhusu shambulo hilo.

Pia alisema jeshi hilo halionyeshi ushirikiano wa kuhitaji kujua wahusika wa tukio hilo kwa kuwa chama chake kilishaomba kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu suala hilo, lakini hawakuruhusu.

“Mimi na dereva wangu kwa vyovyote vile ndiyo mashahidi wa kwanza lakini hadi sasa ninavyoongea hatujahojiwa, hakuna mpelelezi kutoka sehemu yoyote ambaye amekuja kuniuliza Lissu eleza umeshambuliwaje, polisi hawapelelezi kwa sababu wanajua ni shambulio la kisiasa,” alisema.

Pia alisema ofisi ya Bunge nayo imeshindwa kuwajibika kwa kuwa hadi sasa haijatoa fedha kwa ajili ya gharama za matibabu yake kama inavyoelekeza katika Sheria ya Bunge iliyotungwa mwaka 2008.

“Mimi ni mbunge na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Bunge limetunga sheria mwaka 2008 ya uendeshaji wa Bunge inayosema, mbunge anayeumwa atahudumiwa matibabu yake iwe nje au ndani ya nchi na Bunge, gharama za matibabu, chakula kwa mbunge husika na atakayemhudumia zitakuwa chini ya Bunge.

“Hadi leo Bunge la Tanzania halijatoa hata senti kumi ya gharama ya matibabu yangu, wala kwa wale ambao nimekuwa nao kwa miezi minne sasa wananiuguza wakati sheria ipo wazi,” alisema.

Licha ya ndugu zake kuandika barua rasmi ya kuwataka kulipa gharama za matibabu, alisema lakini Ofisi ya Bunge imekuwa ikipiga chenga na kushindwa kuweka wazi kama watalipa ama hawatolipa.

Pia alisema hakuna kiongozi wa juu wala ofisa yeyote wa Bunge aliyefika hospitalini hapo kumuona (lakini Desemba 15, mwaka jana Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitoa sababu ya kutokwenda Nairobi kumtembelea Lissu kuwa hawezi kwenda kama wanavyoenda wabunge wengine kwa kuwa anapoenda lazima kuwapo na taarifa rasmi za Serikali za kibunge na kupokelewa rasmi, pia alisema aliwatuma wabunge wawili ambao ni wajumbe wa Kamisheni ya Bunge au Tume ya Huduma za Bunge kwa niaba ya Bunge kwenda Nairobi kumtembelea ambao ni Marry Chatanda kutoka Bara na Faharia Shomari kutoka Zanzibar).

Katika hatua nyingine, Lissu alisema  hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa mpango huo wa shambulizi umepangwa bila kuwa na mpango wa pili, kwa kuwa wahusika hawakujua kama ataumwa na kushindwa kuandaa mazingira ya kujiuguza.

“Nasema tena hii ni political assassination imefeli, Mungu mkubwa, Waswahili wanasema Mungu si Athumani na mimi Mungu wangu siku hiyo alikuwa macho kweli kweli, namshukuru kuendelea kuwa macho hadi sasa,” alisema.

Kwa habari zaidi nunua nakala yako leo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles