26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu kizimbani kwa uchochezi

Tundu Lissu
Tundu Lissu

* Asomewa mashtaka matano, asema hatazibwa mdomo

* Mbowe asisitiza mapambano kudai demokrasia yanaendelea

Na Patricia Kimelemeta,

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matano, likiwamo la kuandika na kuchapisha habari za uchochezi katika gazeti la Mawio.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliwataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, mchapishaji Kampuni ya Jamana na Ismail Mehboob.

Kadushi alidai mahakamani hapo kuwa Lissu na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 14 hadi 20, mwaka huu katika Jiji la Dar es Salaam, ambayo ni kinyume na sheria ya magazeti.

Alidai Lissu na wenzake wanadaiwa kuandika na kuchapisha katika gazeti hilo taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Wanadaiwa mnamo Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Shtaka la tatu katika kesi hiyo linamkabili mshtakiwa wa tatu, Mehboob, ambaye anadaiwa Januari 13, mwaka huu katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kuwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kisheria ya kiapo kwa msajili wa magazeti.

“Mshtakiwa huyo na wenzake, kwa pamoja Januari 14, 2016‎, jijini Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale, aliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu,” alidai Wakili Kadushi.

Wakili huyo, aliiomba mahakama kuondoa shtaka la kwanza na la tano kwa sababu halijaendana na sharti la kisheria baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kushindwa kutoa idhini kwa mashtaka hayo.

Kadushi pia aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kesi hiyo, kwa sababu washtakiwa wanne walikuwapo mahakamani hapo na upelelezi ulikwisha kamilika.

Katika kesi hiyo, Lissu anawakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambaye aliunga mkono uamuzi wa upande wa Jamhuri kuondoa mashtaka hayo mawili.

Lissu alikana mashtaka hayo na Hakimu Simba alikubaliana na hoja ya upande wa Jamhuri ya kuondoa mashtaka hayo na kubakisha matatu yanayowakabili washtakiwa wote.

Hakimu Simba aliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini bondi ya Sh milioni 10. Walikidhi masharti hayo na kutolewa nje kwa dhamana.

Kesi hiyo imehairisha hadi Julai 11, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.

NJE YA MAHAKAMA

Akizungumza nje ya mahakama jana, Lissu alisema kuwa Serikali ilimfikisha mahakamani baada ya kusema ukweli kuhusu hali halisi ya uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Alisema kitendo hicho kimesababisha kuandikiwa mashtaka ya uchochezi ili waweze kuzibwa midomo na kushindwa kutetea haki za wanyonge ambao ni Watanzania wengi.

“Kauli yangu haikuwa ya kichochezi, bali nilikuwa naangalia mustakabali wa uchaguzi wa marudio Zanzibar, kwa sababu ilionekana kabisa haki ya wanyonge inaporwa na watu wachache, hatuwezi kuvumilia vitendo vya ukandamizaji unaoendelea kuonekana nchini, lazima tuseme,” alisema.

Alisema kumekuwa na matendo ya hovyo hovyo yanayojitokeza na kwamba wakiwa wanasema ukweli, wanafikishwa mahakamani ili washindwe kuzungumza.

“Hatutakubali, tutapambana na Serikali ndani ya mahakama na nje ya mahakama na tunaamini tutashinda,” alisema.

MBOWE NA DEMOKRASIA

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema demokrasia ipo majaribuni kutokana na uamuzi wa watawala.

Alisema kutokana na hali hiyo, taifa linapitia wakati mgumu, ikiwemo watu, vyama vya siasa kufungwa midomo pamoja na Bunge.

Mbowe aliyasema hayo katika futari iliyoandaliwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa, ambayo iliwakutanisha masheikh mbalimbali wa Mkoa wa  Dar es Salaam.

“Hivi sasa nchi inapita katika kipindi kigumu, Bunge, mahakama na hata Serikali vipo ‘under attack’ (chini) ya mtu mmoja ambaye akiamua kufanya lolote linakuwa. Pamoja na hali hiyo, tunajua tutapambana hivyo hivyo.

“Hata kilio cha masheikh kilichotolewa hapa kuhusu sheria kandamizi kwa kile kilichoelezwa eti ugaidi kila mtu anajua, lakini pamoja na hali hiyo, tunayachukua haya na tutayafanyia kazi, kikubwa tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono ndani na nje ya Bunge,” alisema.

Mbowe alisema kupitia umoja wa vyama vinavyounda Ukawa, hivi sasa wanajitahidi kuimba wimbo mmoja wa kuhakikisha demokrasia ya kweli inakuwepo nchini.

Alisema pamoja na misukosuko iliyopo, Ukawa wataendelea kudai demokrasia, licha ya kile alichodai hila za watawala kutaka kuwafumba midomo.

 

SHEIKH BUNGO

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya masheikh wenzake, Sheikh Kondo Bungo ambaye ni mwanaharakati wa Kiislamu, alimtaka Mbowe kuhakikisha anawaunganisha wabunge na kupinga sheria kandamizi dhidi ya Waislamu.

Alisema hivi karibuni, Bunge limepitisha sheria ya ugaidi, ambayo huenda ikageuka kitanzi kwa Watanzania wengi.

Sheikh Bungo alisema kwa sasa sheria hiyo ya ugaidi inaeleza kuwa hata kama utahisiwa wewe ni gaidi utaishia gerezani bila hatia kama ilivyo kwa masheikh waliopo magerezani.

“Ninasema hata sisi wengine tuna vinyongo, hadi sasa magereza mengi yamejaa masheikh, tena wale ambao wanaonekana hawakubaliani na matakwa ya mabwana wakubwa. Wapo masheikh wetu wa Zanzibar ambao sasa ni mwaka wa tatu hakuna dhamana na haijulikani hatima ya kesi yao.

“Tupo kwenye mtanziko mkubwa, na ndugu yetu Lowassa tunakuambia hata masheikh waliokuja hapa kwa mwaliko wako, ni wale ambao hawakubalini na hali ya mambo,” alisema Sheikh Bungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles