23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu amhenyesha Mwanasheria Mkuu

Tundu-LissuNa Elizabeth Hombo, Dodoma

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), juzi alimhenyesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alipohoji ilipo ripoti ya Tume ya kijaji iliyochunguza majaji waliotuhumiwa kwenye sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Lissu ambaye alikuwa akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, alisema Jaji Mkuu Othuman Chande, alipata kunukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa tume iliyochunguza majaji waliotuhumiwa kwenye kashfa ya Escrow ilishakamilisha kazi yake hivyo kilichobaki ni kuweka ripoti hadharani.

“Nataka kuzungumzia sera ya nidhamu ya majaji, katika mchango wangu na hotuba ya kambi ya upinzani tumezungumzia tatizo la nidhamu ya majaji.

“Tuna utaratibu uliowekwa kwenye Katiba juu ya majaji ambao wanatuhumiwa kwa utovu wa maadili, Katiba imezungumzia ambao wanaweza kuondolewa kwa sababu wana tabia mbaya wanatakiwa kuondolewa kwa kuundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji.

“Tangu mwaka 1991 Jaji Mwakibete alivyoundiwa tume na kuondolewa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, hakujawa na tume nyingine ya kijaji kuchunguza matatizo ya kinidhamu ya majaji wetu.

“Bunge hili limepitisha azimio kwamba majaji hawa ambao ushahidi uliletwa bungeni hapa waundiwe tume ya uchunguzi, hatukusema wafukuzwe, hatukusema wafungwe.

“Tumesema  waundiwe tume ya kijaji kuchunguza maadili yao, leo mwaka na nusu hakuna majibu, kwa hiyo Bunge tulikaa hapa kupoteza muda? Kwanini tume ya uchunguzi ya majaji wa Escrow,  Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa, haijaundwa, kama imeundwa ripoti iko wapi, lilikuwa ni azimio la Bunge,” alisema Lissu.

Akijibu hoja hiyo, AG Masaju alisema Bunge siyo mamlaka ya kinidhamu ya majaji na kwamba ibara ya 113 ya Katiba inaeleza kuna Tume ya Mahakama hivyo kama kuna Jaji anatuhumiwa tume hiyo huchunguza na ikiona inafaa kupendekeza kwa rais kuundwa kwa kijaji.

“Kwenye hili Bunge si mamlaka ya kinidhamu kwa majaji, kwenye maazimio yale ilishauri tu Serikali, sisi hatuwezi tukakaa hapa tukajifanya ni majaji, si mamlaka sahihi ya majaji, hilo liko wazi lazima tuheshimu,” alisema.

Majibu hayo ya Masaju yalimwinua tena Lissu ambaye alikariri kauli ya Jaji Mkuu kwa vyombo vya habari kuwa tume ilishaundwa chini ya Jaji wa Mahakama ya rufani, Salum Mbaruku.

“Taarifa ya tume ilishaiva… huyu AG wa wapi? Jaji Mkuu amesema taarifa iko tayari, Bunge lilipitisha nani aliyesema hapa kwamba Bunge linatoa hukumu, Bunge lilisema Rais aunde tume, ndiyo Katiba inavyosema.

“Kwa haya maneno ya AG ndiyo maana wakati mwingine tunakuwa na shaka, hivi viatu vinamtosha kweli? Hakuna mtu ambaye anasema Bunge lihukumu, azimio la Bunge lilikuwa wazi, Rais aunde tume ya uchunguzi ya kijaji ili kuchunguza tuhuma za kupokea miamala ya Escrow ya Sh milioni 400 kila mmoja,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Masaju alieleza kuwa ni lazima utawala wa sheria uheshimiwe na kwamba Katiba inaeleza namna ya kuwachukulia majaji hatua za kinidhamu.

“Lazima tuheshimu sheria, hapa kuna Katiba inasema namna ya kuwachukulia nidhamu majaji. Sasa utawaundiaje tena tume ya uchunguzi, Katiba inachozungumzia ni tume nyingine si hiyo ya Lissu, Rais akiridhika ndiyo itaundwa,” alisema Masaju.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles