23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Watanzania wanalishwa ‘sumu’

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Awaonya wafanyabiashara wa sukari wanaoendesha mchezo huo kuacha mara moja la sivyo atawafungia maisha,

* Asema shehena iliyofichwa itagawiwa bure kwa wananchi

 

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari wasio waadilifu wakiwemo wale wanaoleta nchini sukari iliyoharibika jambo alilodai linasababisha wananchi kupata  magonjwa yasiyoeleweka.

Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Manyara na Singida baada ya kusimamisha msafara wake uliokuwa ukitokea Dodoma kuelekea Arusha jana, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa ambao wanaenda kuchukua sukari iliyoisha muda wake nje ya nchi  na kuja kuiuza jambo ambalo si sawa.

“Kuna tabia moja ya ajabu inafanywa na wafanyabiashara wenye tamaa ya fedha  wanaokwenda nchi za nje kama  Brazil na maeneo mengine yanayouzwa sukari, wanachukua sukari inayokaribia ku-expire (kuisha muda wa matumizi) wanakuja kuziweka katika vifungashio wanaziuza halafu baadaye watu wanapata magonjwa yasiyojulikana,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wafanyabiashara hao wanatumia mwanya wa nchi hizo ambazo zina utaratibu wa kumwaga sukari zinazokaribia kuharibika baharini  na kuja kuziuza nchini.

Alisema Serikali kwa sasa inajipanga kudhibiti sukari zinazoingizwa kutoka nje kiholela kwakuwa mbali ya kusababisha matatizo ya magonjwa pia zinachangia kuharibu soko la bidhaa hiyo.

“Unalima miwa haiwezi kwenda kutengeneza sukari kwa sababu kuna sukari ya magendo, kwa sasa tunajipanga kudhibiti biashara hiyo,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli pia ameviagiza vyombo vya dola kuwafuatilia wafanyabiashara wote walioficha sukari na kuhakikisha wanazichukua na kuzigawa bure kwa wananchi.

Pamoja na hilo Rais Magufuli amesisitiza kuwa wafanyabiashara hao hawatakuwa na ruhusa ya kufanya biashara nchini maisha yao yote.­­­

“Nimeshaagiza vyombo vya dola vifuatilie wafanyabiashara wote walioficha sukari, wale ni wahujumu uchumi kama wengine, tutaichukua sukari ile tutaigawa bure na hawatafanya biashara maishani hapa Tanzania, kwa hiyo kama kuna wafanyabiashara wananisikia ambao wanataka kucheza na Serikali hii wanacheza na maisha yao, waitoe sukari kwa wananchi wakaiuze kama walivyopanga wasije wakanilaumu.

“Natoa wito  kwa waliokuwa  na sukari  na wameficha kwenye ‘godown’ (maghala), kuna mmoja alienda kununua Kilombero zaidi ya tani 3,000 akaacha kuichukua ipo imetulia, kuna mwingine nimepata taarifa leo (jana) ana godown  kule Mbagala lina  tani 4,000 hataki kuzitoa ili wananchi wakose sukari, nataka niwaambie sukari huwezi kuificha kama sindano,” alisema Rais Magufuli.

Alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wafanyabiashara wote walioficha sukari ili wananchi wahangaike dawa yao anayo.

 

Alisema tatizo  la sukari ni dogo na  litadumu kwa  muda mfupi katika Serikali yake kwasababu hashindwi kununua sukari na kuiuza kwa wananchi kwa bei nafuu.

“Sukari hata iwe mabehewa ya elfu ngapi Serikali ya Magufuli haishindwi kununua, nimeshamwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tunapanga mipango tutaleta sukari ya kutosha watu watapata kwa bei ya chini,” alisema Rais Magufuli.

Machi mwaka huu Rais Magufuli alipokutana na wafanyabiashara alipiga marufuku uagizwaji holela wa sukari kutokana na wafanyabiashara hao kujinufaisha wao binafsi.

Baada ya tamko hilo siku chache baadaye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari nchini, Henry Semwaza, alitangaza bei elekezi ya bidhaa hiyo ambapo wafanyabiashara nchi nzima walipaswa kuhakikisha wanauza Sh 1,800 kwa kilo moja.

Hata hivyo, hali ilianza kubadilika baada ya bei ya sukari kupanda huku wafanyabiashara hao wakituhumiwa kuificha.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakijadili bajeti ya ofisi yake alisema Serikali itaagiza kiasi kidogo cha sukari ili kufidia nakisi iliyopo nchini kwa lengo la kuepusha mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo huku akieleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaficha bidhaa hiyo na kusubiri ipande.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi wa  miji ya Katesh, Babati, Dareda na Magugu mkoani Manyara kuhusu kukosa maeneo ya kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

Kutokana na malalamiko hayo alimwagiza  Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera na wakuu wa wilaya za mkoa huo kukamilisha mchakato wa kumpatia  taarifa ya mashamba yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake wawasilishe taarifa ili afute hati za umiliki wa mashamba hayo na kuamuru wagawiwe wananchi.

“Kero kubwa katika maeneo haya pamekuwa na mashamba makubwa ambayo yalichukuliwa na wenye pesa, halafu yale

mashamba hawayaendelezi na wanapoacha kuyaendeleza wanawachukua wananchi masikini na kuanza kuwakodisha

kwa kukusanya fedha, mniachie hili ndugu zangu nitalishughulikia,” alisisitiza Rais Magufuli.

Mjini Babati, Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi waliodai kudhulumiwa haki zao na kujikuta wakipoteza mali ikiwemo nyumba za kuishi na mazao na amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupanga siku za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Rais Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Dodoma kwa njia ya barabara na kesho anatarajia kutunuku kamisheni kwa maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi Monduli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles