28.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lipumba awavua uongozi wakurugenzi sita

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akitoa taarifa ya kutengua nyadhifa za  baadhi ya wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa chama hichokwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana.Kushoto ni Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Kapasha Kapasha.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akitoa taarifa ya kutengua nyadhifa za baadhi ya wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa chama hichokwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana.Kushoto ni Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Kapasha Kapasha.

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametangaza kutengua uteuzi wa wakurugenzi na manaibu  wakurugenzi sita  akiwemo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Ismail Jussa Ladhu, kutokana na kile alichodai kuwapo kwa changamoto zinazokikabili chama hicho kwa sasa.

Mbali na  Jussa, wakurugenzi wengine waliotenguliwa uteuzi ni Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Abdallah Mtolea ambaye pia ni mbunge, Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha, Joran  Bashange, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Mustafa Wandwi, Mkurugenzi wa Sheria, Kulthum Mchuchuli na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Shaweji Mketo.

Profesa Lipumba alitangaza uamuzi huo jana katika Ofisi ya Cuf iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa ameufanya kwa mujibu wa mamlaka na majukumu aliyopewa na Katiba ya CUF  ya mwaka 1992  toleo la 2014  ibara ya 90(1)(f).

Alisema vifungu hivyo vya sheria ya Katiba ya CUF vinamwelekeza mwenyekiti kuteua viongozi wa kushika nyadhifa hizo  kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa au wanachama wajasiri wa chama.

Profesa Lipumba alisema katiba hiyo  inaelekeza uteuzi ufanyike  baada ya kushauriana na makamu mwenyekiti na baadaye kuufikisha  mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kuthibitishwa.

“Niliteua wakurugenzi na manaibu wakurugenzi baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Juni 2014 kunichagua kuwa Mwenyekiti wa Taifa, kwa kuzingatia changamoto zinazokikabili Chama chetu hivi sasa nimeamua kutengua uteuzi wa wakurugenzi na manaibu wakurugenzi hao,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema viongozi hao ambao hawakuwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kabla ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo, baadhi yao watasita kuwa wajumbe wa baraza hilo baada ya kuonekana kusita kushika nyadhifa hizo.

Alisema kutokana na hali hiyo leo atatangaza viongozi wapya wa kushika nafasi hizo ambao watakaimu nyadhifa hizo mpaka watakapothibitishwa.

Alisema utaratibu wa kuteua majina mapya ya kujaza nafasi hizo ulipaswa umshirikishe  Makamu Mwenyekiti, Juma Duni Haji, ambaye alihama chama.

“Katiba inanielekeza kuwa ninapoteua wakurugenzi nishauriane na makamu mwenyekiti. Hivi sasa Chama chetu hakina makamu mwenyekiti baada ya Juma Duni Hajji kuhama chama na kujiunga na Chadema,” alisema Profesa Lipumba.

Mbali na hilo, Profesa Lipumba pia amewavua ujumbe wa Baraza Kuu la Uongozi  wajumbe wanne  wa baraza hilo ambao ni Jussa, Bashange,Wandwi na Mtolea kwa kutumia ibara ya 84(1)(b) ya Katiba ya CUF.

“Katiba inaelekeza; Pale ambapo mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ambaye kabla ya kuteuliwa kwake hakuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, ataacha kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa sababu yoyote ile, basi atasita mara moja kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa,” alisema Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba aliwataka watendaji wote wa ofisi kuu ya chama hicho ambao wanafanya kazi kwa kujitolea kufika katika ofisi za CUF, Buguruni kesho bila kukosa.

“Kama wana sababu zozote za kutofika watume taarifa kwa maandishi kwenye Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara. Watakaoshindwa kufika au kutoa taarifa watahesabiwa wamejiuzulu nafasi zao za kujitolea na nafasi hizo zitatangazwa kwa wanachama wengine wanaotaka kujitolea,” alisema Profesa Lipumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles