Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, amevitaka vyombo vya dola kuacha kutumika kuharibu chaguzi mbalimbali nchini kwakuwa vinaweza kuchangia umwagikaji damu.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 13, mwaka huu katika Jimbo la Liwale, ambapo alisema wana uzoefu walioupata katika chaguzi zilizopita hivyo hawatarajii hali hiyo irejee tena.
Alisema kumekuwa na wizi wa kura na kuzuia mawakala wasiwepo vituo vinapofunguliwa jambo ambalo limekuwa linatia shaka na kusababisha wananchi wazawa kumkosa kiongozi sahihi wanayemtaka.
Alisema kukataliwa mawakala kuwepo kwenye vituo vya kupiga kura kabla ya kuanza kupigwa kura ni ishara ya wizi wa kura na kutangaza matokeo ya kupanga.
“Tunatoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhakikisha mawakala wetu wanaingia vituoni vinapofunguliwa na bado tunashangaa kwani mawakala wetu wameapa lakini hawakupewa nakala ya kiapo na tumeomba ufafanuzi wa jambo hili kwa msimamizi wa uchaguzi mpaka sasa hatujapata ufafanuzi,” alisema Prof Lipumba.
Alisema wamebaini mbinu ya wizi wa kura ambao umekua ukifanyika kwa kuwafukuza mawakala kabla ya kutangaza matokeo na kuwanyima nakala ya fomu za matokeo hivyo katika uchaguzi huu hawatakubali.
“Tunatoa wito kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kutumia busara katika uchaguzi ujao kwani ngome hiyo ni ya CUF na wamefanya kosa kumpokea na kumteua Mohamed Kuchauka kuwa mgombea wao kwani hauziki,” alisema Lipumba.
Lipumba alisema kuna taarifa wamezipata za mbinu chafu kuanza kutengenezwa ili kuharibu uchaguzi huo hivyo ni vyema NEC na Serikali ikahakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.
Alisema anahitaji waomboleze miaka 19 ya kifo cha baba wa Taifa kwa amani na si kwa maombolezo na maafa endapo uchaguzi huo utahujumiwa kwani Wangindo wakiamua jambo lao wameamua hawarudi nyuma.