Maregesi Paul, Dodoma na Grace Shitundu, Dar
WABUNGE wa vyama vya upinzani jana waliungana kulilaani Jeshi la Polisi nchini kutokana na jinsi lilivyoshiriki kumpiga Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake jijini Dar es Salaam.
Wakichangia kauli ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kuhusu suala hilo, wabunge hao kwa nyakati tofauti walilaani tukio hilo huku wakitaka walioshiriki kwa namna yoyote, wachukuliwe hatua.
Aliyekuwa wa kwanza kulishambulia jeshi hilo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ambaye alisema Serikali na jeshi hilo wana mfumo wa kifashisti unaowakandamiza viongozi wa vyama vya upinzani.
“Kwanza kabisa napingana na huyu mrithi wa Werema (akimaanisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju) anayetaka tusijadili jambo hili eti kwa sababu liko mahakamani.
“Halafu nakupinga wewe mheshimiwa Spika unayesema tuchangie kwa dakika tatu tatu wakati ukijua kanuni inasema tuchangie kwa dakika zisizozidi 15.
“Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika nakwambia mimi nitachangia kwa dakika 15 kama kanuni inavyosema na siyo dakika tatu unazotaka wewe.
“Mheshimiwa Spika, katika nchi hii wapinzani tunakamatwa na kufunguliwa kesi bila sababu. Katika nchi hii, Serikali na Jeshi la Polisi wana ‘element’ za kifashisti zinazotukandamiza kila siku. Yaani ile kauli ya Waziri Mkuu ya ‘wapigwe tu’ ndiyo inatekelezwa sasa.
“Polisi walimuua Mwangosi (Daudi, mwandishi wa habari wa televisheni ya Channel 10) kule Iringa, wanachama wetu wameuawa Arusha, wameuawa Morogoro na wengine wameuawa Nzega. Juzi Profesa Lipumba alipigwa na polisi bila sababu na dunia nzima iliona, kwa hiyo nawaambia sasa imetosha.
“Kwa hiyo, Waziri Mkuu, IGP, Chikawe, Chagonja na Kaniki, wawajibike na pia tukubaliane hapa ili Bunge liunde tume ya kuchunguza matukio yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyowahi kufanywa na Jeshi la Polisi nchini,” alisema Lissu.
Pamoja na hayo, Lissu aliwakumbusha viongozi walioko madarakani kukumbuka kuwa Tanzania ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) yenye makao makuu Uholanzi.
MBOWE
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema kama Jeshi la Polisi halitabadilisha utendaji wake wa kazi linaweza kusababisha machafuko nchini.
Kwa mujibu wa Mbowe, polisi walimpiga Profesa Lipumba kwa maagizo ya viongozi wa juu na kwamba alipata taarifa hizo kupitia kwa maofisa wa polisi aliokuwata katika kituo kikuu cha polisi Mkoa wa Dar es Salaam alipokwenda kumdhamini Profesa Lipumba.
Alisema wakati wa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kalenga, Mbunge wa Viti Maalum, Rose Kamili (Chadema), alipigwa na wana CCM kwa msaada wa polisi.
“Katika nchi hii polisi wanatunyanyasa na mfano halisi ni jinsi Mheshimiwa Rose Kamili alivyopigwa kule Iringa na sasa Serikali imeshatumia Sh milioni 106 kumtibu kule India,” alisema Mbowe.
Masoud Salim
Akichangia mjadala huo Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), alisema kwa muda mrefu Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikiwaua raia wasiokuwa na hatia jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.
“Kila mwaka CUF huwa tunafanya maandamano lakini cha kushangaza hata Waziri amesema uongo hapa bungeni. Barua polisi ilikwenda Januari 22 na si 26 kama alivyodai.
“Tangu huko nyuma baada ya mauaji mwaka 2001, Profesa Lipumba alisema tunasamehe lakini hatutasahau,” alisema Masoud.
MBATIA
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema polisi wanatumia nguvu kubwa kuwakandamiza wapinzani kama walivyofanya kwa Profesa Lipumba na wafuasi wa CUF.
“Sasa umefika wakati wa kubadili sheria zetu kila siku viongozi wa upinzani wamekuwa wakipigwa na kudhalilishwa. Hii ni nchi yetu wote na hatutakiwi kujadili hili jambo kwa ushabiki wa siasa,” alisema Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wakati wabunge wa upinzani wakililaani Jeshi la Polisi, wabunge wa CCM walionekana kulitetea wakisema lilikuwa sahihi kutumia nguvu kukabiliana na wafuasi wa CUF.
Waliolitetea jeshi hilo ni pamoja na Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu, Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, Mbunge wa Chwaka, Yahaya Kassim Issa, Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde na Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis.
SHEKIFU
Akichangia hoja hiyo, Shekifu aliwashukuru wabunge wa CCM kwa jinsi walivyoonyesha utulivu na ukomavu tangu suala hilo lilipoibuliwa bungeni juzi.
Kwa mujibu wa Shekifu, nchi inatakiwa kuwa na amani na Watanzania pia wanahangaikia amani na kwamba CCM ndiyo imeifanya nchi iwe na amani.
“Mimi sitaki kutetea maovu, lakini nitatea yale yaliyo na haki na ambayo yanasimamia ukweli, hakuna nchi isiyo na polisi duniani na hakuna nchi isiyo na jeshi duniani.
“Mara nyingi vurugu zinatokana na kuvunja kanuni na sheria za nchi. Duniani kote matatizo yanatokea kwa sababu ya watu kukiuka sheria na kutotii utawala wa sheria na mimi binafsi nilishawahi kuwa mkuu wa mkoa na nilisimamia amani.
“Mama Kamili (Rose Kamili, Mbunge wa Viti Maalum Chadema) ananifahamu vizuri sana kwa nia njema tulifanya kazi vizuri na alikuwa mtiifu kwa sababu ukimwambia usifanye hili anaacha.
“Hakuna uongozi wowote duniani ambao ukiambiwa usifanye jambo kwa mujibu wa sheria na wewe unaendelea kufanya hakuna serikali itakayokuvumilia,” alisema.
LUSINDE
Mbunge wa Mtera Lusinde alisema pamoja na Mungu kumuumba binadamu pia aliweka adhabu kali ukiwamo moto wa milele.
“Mheshimiwa Spika, kiti chako kinayumba, akizungumza mbunge wa CCM wabunge wa upinzani wanazomea na wewe umekaa kimya tu kwani sisi hatuna midomo ya kuzomea?
“Kuhusu hilo suala la kupigwa Profesa Lipumba, kama kuna siku niliyowahi kuwapongeza polisi ni walipompiga Profesa Lipumba. Kwa hiyo nawaomba polisi kuanzia sasa wawe wanawapiga wahusika wenyewe na si wafuasia wao kwa sababu kila nchi ina utaratibu.
“Leo mnasema Rose Kamili alipigwa wakati anaendelea kula ugali, kuna mwenyekiti wa mtaa alichinjwa kama kuku, haiwezekani.
AG MASAJU
Awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alitaka Bunge lisijadili suala hilo kwa kuwa limekwisha kufikishwa mahakamani.
“Mheshimiwa Spika, jana (juzi) wakati jambo hili linaletwa hapa, Profesa Lipumba alikuwa hajafikishwa mahakamani lakini jana hiyo hiyo alifikishwa mahakamani na kufunguliwa shitaka la jinai.
“Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 64 ya Katiba yetu, Bunge haliwezi kujadili jambo lililo mahakamani kwa sababu katika nchi hii tuna mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Serikali na mahakama.
“Mihimili hii inatakiwa kufanya kazi bila kuingiliana, kwa hiyo mimi kama mshauri wa masuala ya sheria, naomba jambo hili lisijadiliwe kwa kuwa tayari liko mahakamani,” alisema Masaju na kuwafanya wabunge wa upinzani wasimame na kumpinga.
Kauli ya Serikali
Awali akitoa kauli ya Serikali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, aliagiza idara ya malalamiko wizarani hapo, kuchunguza tukio la polisi kumpiga Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba na wafuasi wengine wa chama hicho.
“Mheshimiwa Spika, tarehe 26 mwezi huu, Jeshi la Polisi Dar es Salaam lilipokea barua kutoka CUF yenye kumbukumbu namba CUF/OK/DSM/PF/0027/12A/2015/1 iliyoandikwa Januari 22 mwaka huu.
“Barua hiyo ilikuwa ikitoa taarifa ya maandamano na mkutano wao waliotaka kuufanyia katika Viwanja vya Zakhiem Mbagala Januari 27 mwaka huu.
“Lengo la mkutano na maandamano hayo lilikuwa ni kuadhimisha vifo vya wenzao vilivyotokea Januari 27 mwaka 2001 kule Zanzibar. Yale maandamano yao yalipangwa kuanzia Temeke Sudan kupitia Kichangani hadi Mbagala Zakhiem ambako yangepokewa na Profesa Lipumba.
Juma Duni aibuka
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Juma Duni Haji alisema chama hicho kinapinga udhalilishaji aliofanyiwa Profesa Lipumba na wanachama wa CUF.
Alisema CUF inalaani kitendo cha polisi nchini kutumika kisiasa kuzuia shughuli halali za vyama vya upinzani na kuiruhusu CCM kufanya inayotaka bila kubughudhiwa na vyombo vya dola wala visingizio vya sababu za kiintelijensia.