24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MWENYE DAFTARI LA NYIMBO ZA YAMOTO BAND ANATAMBA

INAWEZEKANA ni aina tu ya utani niliousikia katika onesho mojawapo la ‘stand up comedy’ nililohudhuria lakini baada ya kutoka katika onesho hilo.

Nilitafakari kwa kina nikakubali kuna mashiko ndani yake ndipo nikakumbuka zama zilizopita kwenye muziki hapa Bongo hata kimataifa kwa wenzetu walioendelea kimuziki.

Kwamba katika ‘Back’ hiyo kuna mwanamuziki aliyekuwa katika kundi la The Commodores nchini Marekani, Lionel Richie, ndiye kama alikuwa na daftari la nyimbo za kundi hilo kwani baada ya kutoka si kwamba kundi lilikufa liliendelea kuwepo lakini aling’ara sana na kundi halikusikika kama zamani, kwani alikuwa akifyatua ‘kitu’ baada ya ‘kitu’ na kuhanikiza kiasi cha kupaisha nyota yake huku The Commodores ikififia na kukosa mng’aro wake wa zamani wakati Lionel Richie akiwa kundini.

Mkali huyo naye alipitia madhila kadhaa licha ya kupaa katika ‘Front’ yake kwenye muziki, alifiwa na mzazi wake kisha talaka ikafuatia lakini hayo hayakumfifisha kwenye medani.

Mwanamuziki mwingine ambaye ameondoka na daftari la nyimbo za kundi alilokuwa akilitumikia ni Beyonce Knowles ambaye awali alikuwa na kundi la Destiny’s Child, ambalo katika ‘Front’ aliyoamua kujitenga na kuwa kivyake kimuziki akichana na kufanya kazi na kundi mobu hiyo ya wanyange ikabuma.

Lakini yeye akang’ara na hadi sasa bado anakimbiza  kulinganisha na ‘Back’ hiyo alipokuwa katika kundi na wenzake, ikidhihirsha kwamba yeye ndiye alikuwa roho ya kundi hilo ambalo hata hivyo katika muundo wake halikujiweka katika mfumo wa kinara na wengine kwa kuwa kuna makundi yalikuwa katika muundo huo, mathalan, Kool & The Gang ambapo Robert Kool akiwa ndiye kiongozi na kinara wa kundi.

Destiny’s ikala mweleka Beyonce akakwea kimuziki duniani kama ilivyowahi kutokea hapa Bongo katika kitambo hicho ambacho vijana wa wakati huo walihusudu sana nyimbo za Mamtoni, likiwemo kundi la Boyz II Men.

Miongoni mwa waliofuata nyayo za kundi hilo ni mobu ya Four Crews Flavour ambayo ndani yake alikuwemo Paul Mbena a.k.a Mr Paul, ambaye alipoamua kujiondoa kundini ni kama aliondoka na daftari la nyimbo za kundi.

Ndivyo unavyoweza kulinganisha katika ‘Front’ ya sasa kwa Aslay Isihaka ambaye ni kama awali katika ‘Back’ ya kundi la Yamoto sidhani kama aliwaza kwamba kuna siku hatakuwa katika kundi hilo.

Kwamba yeye ndiye alikuwa roho ya kundi na kwamba kuondoka kwake ni sawa na kuondoka na daftari la nyimbo kwani tangu amekuwa mwenyewe kimuziki ameinuka na kutikisa kwa kiwango kikubwa.

Nyimbo zake zikisikika kila mahala kwenye vyombo vya usafiri kwenye kumbi za burudani na migahawa lakini kikubwa zaidi alichofanikiwa kukitimiza, ni kurudisha masikio ya mashabiki wa Bongo-Fleva kwenye kitambo cha sasa (Front) kwamba si lazima nyimbo ziwe za mdundo wa vurugu za kukimbizana na kucheza tu bila kuzingatia ujumbe.

Kwani alichokifanya katika ngoma zake zinazohanikiza ni kusababisha ladha ya muziki wa kizazi kipya iliyopotea na kuwapoteza wasanii wengi ya muziki wa kusikiliza kurudi upya masikioni.

Inawezekana ni mifano mikubwa kulinganisha mapito yake na magwiji kama Lionel Richie na Beyonce, lakini popote duniani mifumo ya kufanya muziki inalingana tofauti inaweza kuwa wapi muziki unalipa zaidi lakini muundo ni uleule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles