Hadija Omary, Lindi
Serikali mkoani Lindi imetangaza bei elekezi ya ya ufuta kwa msimu mpya wa mwaka 2018/19 ambao tayari umeshaanza sanjari na kutambulisha mfumo mpya wa kuuza zao hilo.
Bei hizo Sh 1,651 na Sh 1,764 kwa kilo moja huku mfumo utakaotumika katika ununuzi wa zao hilo ukifanyika kwa njia ya minada.
Ofisa Kilimo, Uchumi na Uzalishaji mkoani Lindi, Majid Mnyao amesema hayo leo n akuongeza kuwa mfumo huo mpya wa kukusanya na kuuza ufuta kwa njia ya mnada utakuwa ni wa kwanza kutumika kwa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.
“Tumeamua kuuza ufuta kwa mfumo huo baada ya kukutana na changamoto nyingi za ununuzi wa zao hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo katika vikao vilivyopita mkoa uliazimia kuuza ufuta katika mfumo huo,” amesema Mnyao.
Mnyao alizitaja baadhi ya changamoto zilizosababisha kukwamisha maamuzi yao ya kuuza ufuta katika mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa ni pamoja na Mkoa wa Lindi pekee ndiyo utakaotekeleza mfumo unaopendekezwa hali ambayo itasababisha kuwepo kwa mianya ya utoroshaji wa ufuta na kusababishia halmashauri hasara.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni mfumo wa stakabadhi ghalani uliopendekezwa ulikuwa umenakiliwa kutoka katika zao la korosho wakati changamoto za uzalishaji na uuzaji wa mazao hayo haufanani, kutofanya maandalizi ya kutosha yatakayotumika katika mfumo huo, wakulima kutofikiwa na elimu ya kutosha ya mfumo uliopendekezwa.