29.1 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

LIGI KUU BARA ILIVYOANZA KIBABE, MABAO KIDUCHU

Na WINFRIDA MTOI – DAR ES SALAAM


JUMLA ya mechi 10 za raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa timu zote 20 zinazoshiriki ligi hiyo zilipigwa kwenye viwanja tofauti.

Ligi hiyo imeonekana kuanza kwa msisimko wa aina yake kuliko wengi walivyotarajia kwa sababu kila timu ilionekana kujipanga kwa matokeo mazuri bila kujali hadhi ya wapinzani waliokutana nao.

Hali hiyo inadhihirishwa na matokeo yaliyopatikana katika mechi hizo na kushuhudia michezo mizuri ya kuvutia na kuwakosha mashabiki wa soka nchini.

Katika ligi hiyo iliyoanza Jumatano ya wiki hii, hamasa ya mashabiki uwanjani ilionekana ni kubwa tofauti na matarajio ya wengi kila mmoja akisapoti upande wake.

Hata hivyo, matokeo yaliyopatikana katika mechi hizo yamedhihirisha wazi kuwa hakuna mteremko kwenye ligi ya msimu huu kwa sababu ushindani unaonekana utakuwa wa hali ya juu.

Mfano matokeo ya mechi ya Simba na Tanzania Prisons, yaliwafanya wapenzi wengi wa soka hasa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hao ambao waliamini ubora wa wachezaji na maandalizi ya kikosi chao, wangepata ushindi wa mabao mengi.

Lakini hali ilikuwa tofauti katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, kwani Prisons waliwabana Simba walioambulia ushindi wa bao 1-0, lililopatikana dakika ya pili ya mchezo, hivyo kuwafanya wacheze zaidi ya dakika 90 bila bao.

Ikumbukwe msimu uliopita, Simba ilianza ligi kwa kufanya kufuru kwa kuifunga Ruvu Shooting mabao 7-0, katika uwanja huo.

Timu nyingine ambayo haikutarajiwa kupata matokeo mazuri kulingana na aina ya kikosi walichocheza nacho ni  Biashara United iliyowafunga Singida United bao 1-0, ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Biashara United ilipewa nafasi ndogo ya ushindi kwa sababu ni timu ngeni kwenye ligi hiyo, ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza msimu huu.

Kitendo cha Singida United kukubali kipigo kutoka kwa Biashara, tena ikiwa uwanja wake wa nyumbani, imeendeleza rekodi mbaya ya kufanya vibaya katika mechi za kwanza za Ligi Kuu.

Msimu uliopita pia Singida United walianza kwa kipigo kutoka kwa Mwadui FC baada ya kufungwa mabao 2-0, katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Matokeo mengine yaliyokuwa gumzo ni Yanga kuifunga Mtibwa mabao 2-1, kwa sababu kati ya timu zilizobezwa tangu zinafanya maandalizi ni Yanga, hakuna aliyetarajia kuwa itaanza na ushindi wa aina hiyo.

Kutokana ubora wa kikosi cha Mtibwa Sugar na aina yake ya kucheza hasa inapokutana na timu kubwa, iliwafanya hata mashabiki wa Yanga kwenda uwanjani kwa wasiwasi.

Zilizopanda zashindwa kuonyesha makeke

Kati ya timu zilizopanda msimu huu ni Biashara United pekee imefanikiwa kuibuka na ushindi, zilizobaki zimeambulia sare na kufungwa.

Timu hizo ni African Lyon, ilifungwa bao 1-0 na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, JKT Tanzania walisuluhu na KMC, Uwanja wa Meja Jenerali, Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Coastal Union ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati Alliance ilifungwa bao 1-0 na Mbao FC, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Derby ya Mwanza ilivyonogeshwa na vituko

Msimu huu kutakuwa na mechi nne za derby ambapo moja tayari imechezwa kwa kuzikutanisha Alliance na Mbao FC za jijini Mwanza.

Mechi hiyo ilikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na upinzani wa timu hizo, kwani kulikuwa na vituko vingi vilivyopambwa na mabango yenye ujumbe tofauti.

Mashabiki wa Mbao FC ndio walikuwa zaidi wanarusha vijembe kwa wenzao baada ya kuibuka na ushindi na shabiki mmoja wa kikosi hicho alionekana ameandika ujumbe kwenye tumbo lake unaosema:  ‘Haa! kumbe wanafunzi? Chapa bakora 3+3=Moto’.

Wachezaji walioweka rekodi

Salum Ije wa Mwadui FC, anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la kwanza katika msimu wa 2018/19, alilofunga dakika ya tisa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba walipokutana na Kagera Sugar iliyoshinda 2-1.

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, anaingia kwenye rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi dakika ya pili ya mchezo, walipoibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Kagera Sugar yakaa kileleni kwa saa

Timu ya Kagera Sugar ilikuwa ya kwanza kufunga bao zaidi ya moja baada ya kuifunga Mwadui mabao 2-1, hivyo kukaa kileleni kabla ya kushushwa na Azam FC, iliyoifunga Mbeya City mabao 2-0.

Idadi ya mabao yapungua

Baada ya mechi zote kumalizika kwa timu zote ishirini kucheza, idadi ya mabao iliyofungwa ni 15, tofauti na msimu uliopita, timu zilikuwa 16 lakini mechi za kwanza yalifungwa mabao 17.

Hata timu zilizoibuka na ushindi hakuna aliyefunga mabao zaidi ya matatu, wakati msimu uliopita Simba iliweza kufunga mabao saba katika mechi yake ya kwanza.

Wageni wazing’arisha Simba, Yanga

Majina ya wachezaji wa kigeni wa Simba na Yanga, Kagere aliyefunga bao pekee la timu yake na Heritier Makambo, ndiyo yaliyotawala mtaani kutokana na viwango walivyoonyesha.

Vikosi vilivyoanza na makocha wapya

Tofauti na Simba na Yanga, timu nyingine zilizoanza msimu na makocha wapya ni Azam FC inayonolewa na Hans va de Pluijm, KMC chini ya Etienne Ndayiragije.

Nyingine ni Lipuli FC, inayonolewa na Samwel Moja, Mbao FC yupo Amri Said, African Lyon inafundishwa na Mfaransa, Soccoia Lionel, Singida United inafundishwa na Hemed Morocco.

Matokeo ya jumla yalivyo  

Yanga   2-1 Mtibwa Sugar

Azam FC 2-0 Mbeya City

Kagera Sugar 2-1 Mwadui FC

Stand United 1-0 African Lyon

Simba      1-0 Tanzania Prisons

Ruvu Shooting 0-1 Ndanda FC

Singida United 0-1 Biashara United

Alliance FC     0-1 Mbao FC

Coastal Union 1-1 Lipuli FC

JKT Tanzania 0-0 KMC

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles