MKATABA STIEGLER’S KUSAINIWA MWEZI UJAO

0
874

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM


SERIKALI imesema mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge uko mbioni kukamilika na mkataba utasainiwa mapema Septemba na mradi kuanza rasmi Desemba.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alipofanya ziara katika Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, inayozalisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa na Dimba.

“Naomba kuwatangazia tu wakati wowote kuanzia sasa mradi huu utaanza, sasa tupo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kusaini mkataba na mkandarasi, tunatarajia kusaini mkataba  Septemba, mkandarasi atakayefanya kazi hiyo tutamtaja tutakapokuwa tunasaini,” alisema Dk. Abbas.

Alisema baada ya kusaini mkataba wa mradi huo utakaotekelezwa ndani ya miaka mitatu, Serikali itampa mkandarasi miezi mitatu ya maandalizi ambayo yatahusisha kukusanya mitambo na rasilimali zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi na baadaye Desemba mwaka huu  kazi ya ujenzi itaanza rasmi.

Alisema Serikali inatekeleza mradi huo ambao uliasisiwa miaka ya 70 na 80 na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, ambapo awali utekelezaji wake ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali.

Alisema Serikali imeshafanya tathmini mbalimbali ambapo tathmini ya kwanza ilifanywa na wataalamu kutoka nchi za Scandinavia wakishirikiana na Watanzania miaka ya 80.

Alisema kabla mkandarasi hajaenda kuanza kazi katika mradi huo, kazi ya kwanza ilikuwa ni kufanya usanifu ambao ulieleza mradi huo utakavyokuwa.

“Kazi ya usanifu imekamilika na tumethibitishiwa kitaalamu tunaweza kutengeneza megawati 2,100, kwenye sayansi ya umeme wataalamu wanasema zinaweza kuongezeka megawati tano ama 10 au kupungua tano au 10.

Sasa kwa megawati hizi huu ni mradi mkubwa tangu tupate uhuru, tangu tupate uhuru mpaka sasa miradi ya umeme tuliyofanya inazalisha megawati 1,500,” alisema Dk. Abbas.

Alisema kazi nyingine iliyofanyika kwenye mradi huo ni tathmini ya mazingira ambapo alidai wataalamu waliofanya kazi hiyo wamesema hakuna athari kubwa ya mazingira itakayosababishwa na mradi huo.

“Kitaalamu hakuna mradi ambao  hautaathiri mazingira kwa hivyo wataalamu wanaangalia je, athari yake itakwenda kuathiri vizazi? Kisayansi wamesema hata kuchimba nguzo moja tu zinaathiri, hata ukiweka tofali kuna madhara kwa sababu utaondoa udongo pale na vitu vingine, hivyo zipo athari ndogo lakini ni ndogo.

“Pia kuna hatua ambazo wamezipendekeza ili kudhibiti hali hiyo, kwa mfano wanasema kuna eneo litachimbwa bwawa litakusanya maji mengi kwa hiyo hilo eneo maana yake litakuwa na maji mengi, pia lazima uangalie ukate miti katika eneo hilo ama uizamishe.

“Kisayansi wanasema ukizamisha miti chini inaoza kwa muda mrefu kwa hiyo inachukua oksijeni nyingi kwa hiyo inaathiri viumbe wengine kama samaki hawawezi kuwepo, kutokana na hilo wakaamua tukate miti, wataalamu waliangalia kila kitu kama kuna eneo lina wanyama wanaangalia watachukuliwa kwa namna gani wahifadhiwe pengine,” alisema Dk. Abbas.

Alisema eneo lote litakalotumiwa kwa ajili ya mradi huo ni asilimia 1.8 tu ya hifadhi yote ya Mbuga ya Selous, jambo ambalo kwa namna nyingine litasaidia kulinda hifadhi hiyo kutokana na miundombinu ya ulinzi itakayowekwa.

Alisema pia bwawa litakalochimbwa kwa ajili ya kuweka maji lina urefu wa kilomita za mraba 100 na kwamba mbali na kuhifadhi maji ya kuzalisha umeme litakuwa pia kwa ajili ya uzalishaji wa samaki.

“Faida nyingine ni kuwa litasaidia kuvutia utalii, kwa sababu kwenye lile eneo yale maporomoko yana mvuto wake, maporomoko yale yamechimba karibu mita 100 chini kile chenyewe ni kivutio,” alisema Dk. Abbas.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here