JOHANES RESPICHIUS Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kikishirikiana na viongozi wa vyama vya siasa wamemuomba Rais Dk. John Magufuli kuruhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
Wamesema Katiba Mpya itaweka misingi itakayomsaidia Rais Dk. Magufuli katika juhudi zake za kuleta utawala bora.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam jana, wakati wa semina ya viongozi wa vyama vya siasa ya kujadili hatma ya mchakato wa kupata Katiba Mpya uliokwama kwa muda sasa.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuwajengea Uwezo Vijana (YPC), Israel Ilunde alisema Katiba Mpya itamsaidia Rais Dk. Magufuli na Serikali yake.
“Ni dhahiri ili kupata Katiba Mpya kunahitajika utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi kuanzia kwa rais mwenyewe na wengine kuwa na nia na utayari wa kukamilisha mchakato huu,” alisema Ilunde.
Alisema vyama vya siasa vishirikiane na Serikali kutafuta muafaka wa kitaifa ili kurahisisha upatikanaji wa Katiba Mpya kwa wakati na kuepusha misuguano inayoweza kuzuilika.
“Umefika wakati wa wabunge na asasi za kiraia kuendeleza utetezi na ushawishi wa kupatikana kwa Katiba Mpya ili mazuri anayoyafanya rais na Serikali yawe msingi wa kila kiongozi atakayeingia madarakani,” alisema Ilunde.
Alisema ni vema kukwepa kuchanganya uchaguzi na mchakato wa Katiba Mpya ili kuepuka hofu ya uchaguzi.
Naibu Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Felix Makuwa yeye alikiomba Kituo cha Haki za Binadamu na Utawala Bora (LHRC) kushirikiana na Baraza la Vyama vya Siasa kuwezesha kuundwa kwa kamati maalumu ya kumshawishi rais juu ya kumalizwa kwa mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya na kuingizwa kwa maoni ya wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Richard Lyimo alisema iwapo sheria ya mabadiliko ya Katiba itakapofanyika, iruhusu maboresho ya Katiba inayopendekezwa kwa kuingizwa maoni muhimu ya wananchi yaliyoachwa.
Naye Mkuu wa Idara ya Dawati la Katiba kutoka LHRC, Anna Henga alisema semina hiyo ina lengo la kujadili namna ya kwenda mbele katika mchakato wa kupata katiba mpya.