NA CHRISTOPHER MSEKENA
MWEZI Aprili mwaka 2011, ulimwengu wa tamthilia na filamu ulimpokea kwa mikono miwili mrembo, Lena Headey baada ya kuonekana kupitia runinga maarufu ya filamu nchini Marekani, HBO, iliyoanza kurusha tamthilia ya Game Of Thrones.
Tamthilia hiyo ambayo katika kipindi chake cha kwanza cha msimu wa nane, uliozinduliwa mwezi Aprili mwaka huu, Game Of Thrones iliweka rekodi ya kutazamwa na watu milioni 17 ulimwenguni kote ndani ya siku moja na hapo ndipo, Lena Headey aliyecheza kama mkuu wa maadui akitumia jina la Cersei Lannister, akazidi kujizolea umaarufu.
Lena au Cersei Lannister, amecheza kama mkuu wa maadui asiye na mbwembwe nyingi kutokana na mwongozo wa tamthilia hiyo iliyonakiliwa katika riwaya ya ‘A Song Of Ice and Fire’, kutoka kwa mtunzi, George Raymond Richard Martin, ukimtaka mrembo huyo kuonekana katika sehemu chache zenye ulazima.
LENA HEADEY NI NANI
Huyu ni raia wa Uingereza, mtoto wa afisa wa jeshi la polisi huko Magharibi mwa Yorkshire, akizaliwa kwenye mji wa Hamilton, Bermuda mwaka 1973, katika familia ya watoto wawili, akiwa na mdogo wake wa kiume anayeitwa Tim.
Alianza sanaa ya uigizaji akiwa na miaka 17 alipokuwa anasoma Shelley Collage. Uwezo na kipaji alichoonyesha kilimpeleka mbali kiasi cha kufanya maonyesho kwenye kumbi kubwa kubwa ukiwamo ule wa Taifa (Royal National Theatre), uliopo jijini London, huku filamu yake ya kwanza ikiwa ni Waterland iliyotoka mwaka 1992.
Filamu hiyo ilimfungulia milango na fursa nyingi za kibiashara kupitia kipaji chake, kwani aliweza kushiriki kwenye sinema kadha wa kadha ikiwamo The Remains Of The Day iliyopata mafanikio ya kuingia mara nane katika tuzo kubwa duniani za filamu, The Oscars.
AINGIZA MAMILIONI KWA DAKIKA
Kama ambavyo nimesema hapo awali kuwa wenzetu hawana mchezo katika suala la kuwalipa vizuri wasanii wao. Lena anaweza kuwa mfano wa mwigizaji anayelipwa mkwanja mrefu ndani ya dakika moja kwani kuonekana kwenye tamthilia ya Game Of Thrones, msimu wa nane uliositishwa Mei 19 mwaka huu alilipwa zaidi ya shilingi bilioni 3 za Tanzania.
Msimu mzima wa tamthilia hiyo yenye jumla ya dakika 434, Lena amecheza dakika 25 pekee. Kumbuka yeye ndiyo mkuu wa maadui lakini hajaonekana kwenye ‘sini’ nyingi.
Hivyo kwa kila dakika moja aliyocheza kwenye Game Of Thrones, Lena alikuwa analipwa shilingi milioni 129, licha ya kutokuwa na makali kama kubwa la maaadui na kufa kizembe kwa kuangukiwa na mawe.
MAFANIKIO
Mrembo huyo mwenye utajiri wa dola za Marekani milioni 9 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 20.6 za Tanzania kwa mujibu wa tovuti ya Celebrity Net Worth May 5, 2019, amejipatia mafanikio mengi kutokana na sanaa yake ya uigizaji.
Mpaka sasa amepata dili za matangazo kutoka kampuni mbalimbali kubwa ikiwamo kupamba kurasa za mbele za majarida maarufu ya filamu na mitindo pamoja na ubalozi wa kampeni ya haki za wanyama kupitia taasisi ya PETA inayofanya kazi nchini Marekani.
Pia, ameshinda tuzo kadhaa za Uigereza na Marekani kama vile Mwigizaji Bora wa Kusaidia kupitia Game Of Thrones ya mwaka 2011), Mwigizaji Bora wa Kike kupitia filamu Aberdeen ya mwaka 2000 na nyingine nyingi ambazo alitajwa kuwania lakini hakushinda.
MAPENZI NA FAMILIA
Mwaka 2007, Lena alifunga ndoa na mwanamuziki wa Uingereza, Peter Loughran na wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume anayeitwa Wylie Elliot aliyezaliwa 2010. Wawili hao waliingia kwenye mgogoro mwaka 2011 uliopeleka kutengana kwa muda na kesi ya kutalakiana ikaunguruma Julai 20, 2012, katika mahakama ya Los Angeles, Marekani iliyopeleka Peter kumpa talaka mwigizaji huyo Disemba 20, 2013.
Baada ya kupokea talaka yake, Lena alihamishia mahaba kwa mwigizaji mwenzake wa tamthilia ya Game Of Thrones, Jerome Fynn mwaka 2014, penzi la siri lililopewa kificho kwa kivuli kwamba ‘wanaigiza’.
Mwaka 2015, Lena alipata mtoto wa pili wakike anayeitwa Teddy, aliyezaa na mwongozaji wa filamu Dan Cadan ambaye ni mwanaume aliyekua naye toka utotoni na waliwahi kuigiza wote filamu ya The Devil’s Wedding na wakafunga ndoa mwaka jana.