Na JANETH MUSHI-ARUSHA
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amesema hana kinyongo wala uadui na mtu yeyote kuhusu hatua ya Serikali kumweka mahabusu kwenye gereza la Kisongo kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana.
Kutokana na hali hiyo amesema anamwachia Mungu kwani katika kipindi chote alichokuwa mahabusu ameliombea Taifa, Rais Dk. John Magufuli, Bunge, Mahakama, DPP pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipokuwa akizungumza katika ibada ya kwenye Kanisa la Winners Chaple, ambapo alitoa sadaka na shukrani kwa Mungu na waumini wa kanisa hilo.
Alisema amefurahi kwa sababu Mungu alimpa likizo muhimu kwa kumpendelea kwa kuwa mbunge wa kwanza kula Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya akiwa gerezani.
“Nimeomba sana, nimewaombea sana nikiwa gerezani na sikuwa najua nina uwezo wa kuomba masaa manne ila nimemhubiri Mungu sana gerezani nimeombea Taifa, viongozi, Bunge, Mahakama, Ofisi ya DPP na Rais Dk. Magufuli,” alisema na kuongeza
“Ukweli kabisa sina adui kwenye jambo hili na sina kinyongo kwenye jambo hili, ni mara ya kwanza nilimwona mke wangu akiniletea gerezani kwa hiyo mimi nilipendelewa kuliko ninyi na hamtakaa mlie Krismasi gerezani, mkimjua Mungu alivyonibadilisha kupitia gereza mtatamani muende gerezani,”
Lema aliwaeleza waumini hao kuwa Yusuph alisema wao walimkusudia mabaya lakini Mungu alimkusudia mema huku akinukuuu andiko lake la shukrani kutoka katika Biblia kitabu cha Luka 6: 27-28 na kusema kuwa hakuna mbegu dhalimu inayopandwa itakayovuna rehema.
“Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia wapendeni adui zenu,watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikini ambao wanawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wanawaonea ninyi,” alinukuu kitabu hicho.
WEMA, BAWACHA WAMTEMBELEA
Mara baada ya kutoka katika ibada hiyo Msanii wa filamu nchini Wema Sepetu na viongozi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Mkoa wa Arusha, wilaya na viongozi wengine kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Manyara walifika nyumbani kwa mbunge huyo eneo la Njiro, kumpongeza baada ya kutoka gerezani.
Akizungumza na viongozi hao, alianza kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kudai kuwa kiongozi huyo anafanya kusudi la Mungu la kukisambaratisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ninamshukuru Makonda na wanaomlaani Makonda walaaniwe kwa sababu Makonda anafanya kusudi la Mungu la kukisambaratisha CCM na mzigo wa Taifa hili ni CCM.
“Makonda amesababisha nyumba hii tumekata maua kweli kwa sababu tulipoanza kusikia habari ya dawa za kulevya sisi tuliozungusha miti na maua, tuliogopa mtu asirushe bangi au lolote hasa kwa sisi tunaopigana na Serikali kila siku,” alisema.
Akimzungumzia msanii hiyo, Lema alimweleza kuwa ameingia kwenye kazi yenye thawabu lakini kazi ambayo atakabiliana na changamoto nyingi na kumtaka asikate tamaa wala kuyumbishwa na jambo lolote.
"Wema una marafiki na wafuasi wengi ukiamua kuhamisha watu wako wakaingia kupigania mageuzi kwelikweli kwa pamoja tutaenda kuokoa taifa hili na njia sahihi ya kukabiliana na hofu ni kufanya kile kinachokutia hofu, usijali wamesema nini kuhusu wewe, kulala mahabusu ambayo ni baraka na inafanya watu watambue jela anaweza kuingia mwanamke na akatoka na nywele zake,” alisema Lema.
Mbunge huyo alimtaka msanii huyo kutengeneza mkakati wa kuleta wanawake na wasichana ndani ya Chadema kwani kwa sasa upinzani unakuwa katika mateso na si kwenye raha.
Alisema Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Raila Odinga alikaa magereza kwa miaka tisa lakini hivi sasa nchi hiyo ipo kwenye demokrasia huku Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandelea ambaye naye alikaa gerezani kwa miaka 27 na sasa wananchi wake wanajitawala wenyewe.