29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Lema kufikishwa kortini leo

ANDREW MSECHU –Dar es Salaam

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike, alisema Jeshi la Polisi mkoani humo limekamilisha taratibu za kisheria na leo linatarajia kumfikisha mahakamani Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Kamanda Njewike alisema jeshi hilo ambalo lilimkamata Lema tangu mwanzoni mwa wiki hii, litamfikisha mahakamani kujibu tuhuma dhidi yake.

“Tayari tunakamilisha taratibu za mashtaka leo (jana) na kesho (leo) tutamfikisha mahakamani, kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema Kamanda Njewike.

Alipoulizwa mwelekeo wa mashtaka dhidi yake kwa mujibu wa taratibu zilizokuwa zikikamilishwa na jeshi lake, Kamanda Njewike alijibu; “kuhusu tuhuma zinazomkabili itajulikana mahakamani.”

Juzi, Kamanda Njewike alisema walimkamata Lema Jumatatu, na tayari walimrejesha mkoani Singida akitoka Arusha kwa mahajiano zaidi na baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, jeshi hilo lilimfungulia jalada la uchunguzi Lema kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kuwa watu 14 wilayani Manyoni mkoani Singida walifariki dunia kwa kuchinjwa katika matukio mbalimbali wakati alipokuwa kwenye mazishi ya Alex Jonas ambaye mwili wake ulikutwa umetupwa na kukatwa katwa sehemu mbalimbali za mwili katika eneo la mbugani wilayani humo.

“Tumemkamata mbunge huyu kutokana na kauli na taarifa aliyoitoa Februari 29, mwaka huu kuwa watu 14 wote waliuawa kwa kuchinjwa wilayani Manyoni, taarifa ambazo sio za kweli,” alisema Kamanda Njewike.

Awali, kabla ya kukamatwa, Kamanda Njewike aliwaambia waandishi wa habari kuwa taarifa iliyotolewa na mbunge huyo ni ya uongo, yenye lengo la kuleta uchochezi na taharuki kwa wananchi kwani matukio yote ya mauaji aliyoyatoa yametokana na wizi, wivu wa kimapenzi na migogoro ya kifamilia.

Kamanda Njewike alisema kufuatia taarifa hizo, Lema alikamatwa Jumatatu jioni mjini Arusha na kisha kusafirishwa hadi Singida mjini.

CHADEMA YALAANI

Katika taarifa yake jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilieleza kuwa baada ya Jeshi la Polisi mkoani Singida kuendelea kumshikilia chini ya ulinzi Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kinyume na taratibu za sheria za nchi – siku mbili mfululizo, kimeamua kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha anapata haki yake, kuachiwa huru kwa dhamana au kufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya polisi kukiuka utaratibu wa kisheria unaowataka kutomshikilia mtuhumiwa yeyote zaidi ya saa 24 bila kumwachia huru au dhamana au kumfikisha mahakamani baada ya kumfanyia mahojiano.

“Jeshi hilo lilimkamata Lema, kumshikilia chini ya ulinzi na kumsafirisha kutoka Arusha hadi Manyoni mkoani Singida, Jumatatu Machi 2, mwaka huu, likatumia siku nzima ya Jumanne kumfanyia mahojiano ambayo yalikamilika jana (juzi) hiyo hiyo.

“Lakini katika hali ya kushangaza, polisi mkoani Singida kupitia kwa RCO, tangu kumalizika kwa mahojiano hayo wameshindwa kumwachia kwa dhamana au kumfikisha mahakamani kama sheria zinavyoelekeza, badala yake wamedai wanasubiri maelekezo kutoka juu,” alisema Makene.

Alisema pamoja na kuagiza hatua hizo za kisheria, Chadema inapinga na kulaani vikali mwenendo huo wa Jeshi la Polisi nchini kuwatendea watuhumiwa, hasa viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema maeneo mbalimbali nchini, kama vile ni wahalifu, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

Makene alisema tukio hilo la kukamatwa na kushikiliwa kwa Lema kinyume na sheria ni mwendelezo wa ukiukaji mkubwa wa taratibu za kisheria za nchi unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia, ikiwa ni sehemu ya kile kinachozidi kujidhihirisha kuwa ni utamaduni wa vyombo vya dola na mamlaka zingine za kiserikali kuendelea kuminya na kukandamiza haki za Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles