28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Tahadharani ya corona makanisani, misikitini

FARAJA MASINDE na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM

SERIKALI imeagiza taasisi zote za dini nchini, ofisi za umma na shule kuhakikisha wanaweka sehemu maalumu za kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Agizo hilo limetolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipokuwa akifungua mafunzo kwa viongozi wa dini nchini, yaliyolenga kujifunza jinsi ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vinazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.

Alisema tangu mlipuko wa corona uanze katika nchi ya China Desemba mwaka jana, watu walioambukizwa wamefikia 90,870 kutoka nchi 72 huku vifo vikiwa 3,112.

Ili kukabiliana na virusi hivyo, nchi mbalimbali zimekuwa zikichukua hatua za kupunguza maambukizi hayo, ikiwamo Italia ambayo imetangaza kufunga shule na vyuo.

Kwa upande wa Korea Kusini ambayo ndiyo yenye waathirika wengi baada ya China, mkuu wa kanisa moja nchini humo ameomba msamaha baada ya kubainika kuwa mkusanyiko kwenye kanisa hilo ulifanya watu wengi zaidi kuambukizwa virusi hivyo.

 Korea Kusini hadi juzi ilikuwa na vifo 28 na watu 4,335 wenye maambukizi ya virusi hivyo.

Kiongozi wa Shincheonji Kanisa la Yesu, Lee Man-hee, alipiga magoti na kuinama akiomba radhi wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Takribani asilimia 60 ya maambukizi ya watu 4,000 nchini humo ni washirika wa kanisa hilo.

Jana Ummy alisema; “katika hili la kuhakikisha kuwa tunakabiliana na magonjwa haya ya mlipuko, natoa maelekezo kwa taasisi za dini, taasisi za umma, maofisi na mashule ya Serikali na binafsi kuweka sehemu maalumu ya kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria ili kuepuka maambukizi yatokanayo na bakteria.

“Mtu anatakiwa anawe mikono, awe anaingia iwe kanisani au msikitini na ofisi nyingine zote, tunawaomba viongozi wa dini mwende mkatoe elimu kwa waumini wenu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi na pia kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua ambaye ana historia ya kusafiri nje ya nchi.

“Maana takwimu hizi zinatuonyesha kuwa ugonjwa huu unaendelea kusambaa duniani, hivyo kama nchi tunahitaji kuongeza nguvu na kushirikiana na viongozi wa dini katika kuhakikisha tunakabiliana na ugonjwa huu.

“Katika nchi zilizoathirika na ugonjwa huu, tunamshukuru Mungu ni nchi nne tu za Afrika zimeripotiwa kuwa na corona ambazo ni Algeria wagonjwa watano, Nigeria mmoja, Senegal mmoja na Misri wawili, tuendelee kumwomba Mungu na kuchukua tahadhari ili corona tusiione nchini,” alisema Ummy.

Aidha, katika hatua nyingine Ummy alitoa saa tano hadi kufikia jana saa 10, kwa kila halmashauri kutenga sehemu maalumu ya kumuweka mshukiwa wa ugonjwa wa corona na kufanya utaratibu wa uchunguzi na kutoa taarifa haraka Wizara ya Afya.

“Ninatoa muda mpaka saa 10 jioni vituo vyote vya afya vya umma nchini viwe vimetenga sehemu maalumu ya kuweka mshukiwa wa virusi vya corona na kuripoti haraka iwezekanavyo katika Wizara ya Afya kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki,” alisema Ummy.

Alisema hadi sasa Tanzania ni salama, na kwamba hakuna mshukiwa wa COVID-19, lakini Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini, ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali zikiwamo za dini.

Ummy alisema wizara yake haijalala, timu yake ina zaidi ya wiki nne sasa ipo kazini usiku na mchana kuhakikisha inawalinda Watanzania dhidi ya virusi hivyo vya corona.

 Alisema kutokana na mwingiliano uliopo, hasa wa kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na nchi za bara la Asia na Ulaya, anawakumbusha wananchi kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwa kitambaa au nguo safi.

“Tunawaomba watu wasubiri na wajiepushe na safari zisizo za lazima kwenda katika maeneo yaliyoathirika, na inapolazimu kusafiri, basi wapate maelezo ya kitaaluma kabla ya kuondoka na baada ya kurudi nchini kuzingatia uvaaji wa ‘mask’ kwa ajili ya kujikinga wakati watakapokuwa wanatembea katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo,” alisema Ummy.

Alisema kama Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imeshasambaza vielelezo vya uelimishaji kwa njia ya redio, runinga na machapisho ili kuhakikisha asilimia kubwa ya jamii inapata ujumbe muhimu kuhusu magonjwa ya ebola na corona.

“Pia Serikali imeendelea kununua, kusambaza vifaa vya kujikinga na vile vya maabara ya kuchukulia na kusafirisha sampuli pamoja na kuhimiza kufuata kanuni za huduma za afya wakati wa kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa yanayohusiswa kuwa ya milipuko,” alisema Ummy.

Alisisitiza kuwa nchi ya Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Afrika na duniani kwa ujumla ipo katika tishio la kupata virusi vya corona, hivyo harakati na maandalizi ya kuchukua tahadhari zimekuwa zikifanyika kwa njia mbalimbali ili kudhibiti jambo hilo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Ketsela Mengestu, alisifu mpango huo wa Serikali kwa kusema kuwa kitendo cha kuwakutanisha viongozi wa dini na kuwapa elimu ni cha kipekee na cha kuigwa na mataifa mengine.

“Uamuzi huu wa Serikali kukutana na kuwaelimisha viongozi wa dini ni wa kuigwa, kwani kama tunavyotambua kuwa viongozi hawa ndio wanaoongoza waumini wao, hivyo itakuwa ni rahisi kuweza kutoa elimu kutokana na kuheshimika kwao katika jamii.

“Lakini pamoja na kwamba kumeendelea kuripotiwa kwa kesi mpya za washukiwa wa virusi hivi, lakini hatuna haja ya kupaniki, kwani tunafahamu ni kwa namna gani jamii imekuwa na hofu.

“Ndiyo, na hii ni kutokana na kwamba ugonjwa huu ni mpya ambao umeshindwa kufahamika tiba yake hadi sasa, hivyo jambo la msingi linalopaswa kufanyika kwa sasa ni kuhakikisha kuwa maandalizi yanafanyika kadiri inavyowezekana, hivyo WHO itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania,” alisema Dk. Mengestu.

Naye Sista Maria Manirakiza ambaye ni mwenyeji wa Rwanda anayefanya kazi mkoani Kigoma, alisema kuwa kulingana na maelekezo yatakayotolewa kwa viongozi wa dini ikiwamo ya kutoshikana mikono, wataweza kutekeleza agizo hilo.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto Duniani (Unicef) hapa nchini, Rene Dongen alisema anaipongeza Wizara ya Afya na jukwaa la viongozi wa dini kwa kuwezesha ushirikiano huo, ambao ni nguzo muhimu katika kuimarisha elimu kuhusu hatari ya magonjwa yanayoathiri afya ya jamii.

Alisema Tanzania inaendelea kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya ebola na corona, hivyo njia mahususi ya kujikinga na kudhibiti magonjwa hayo ni kuzingatia tabia za usafi binafsi kama vile kunawa mikono na sabuni mara kwa mara.

MADAKTARI NA ELIMU YA CORONA

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala  za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya), Josephat Kandege,  amewataka madaktari kutoa elimu kwa jamii kuhusu  ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona ambao umekuwa tishio duniani.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa kufunga maadhimisho ya Siku ya Madaktari Duniani, Kandege pia aliwataka wananchi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Ummy. 

“Naomba tuzingatie wito uliotolewa na Waziri wa Afya, kwa kipindi hiki tuache kusalimiana kwa mikono, tuache kukumbatiana, kuepuka kugusana na sisi Serikali tunaiomba MAT (Chama cha Madaktari Tanzania) itusaidie kutoa elimu kwa jamii kwani hili ni janga la kimataifa,” alisema Kandege.

Tayari Waziri Ummy alishatangaza jinsi Serikali ilivyojiweka tayari kupambana na virusi hivyo, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo maalumu kwa matibabu, wataalamu na vifaa.

Pia alisisitiza wananchi kukata bima ya afya ili waweze kupata matibabu ya uhakika kutokana na gharama za juu za matibabu.

“Kila mtu ahakikishe ana bima ya afya kwani ukiwa na bima hata magonjwa yanakuwa yanakukimbia, ukiangalia watu wenye bima huwa hawaumwi mara kwa mara, lakini usipokuwa nayo ni tatizo.

Kandege alisema ni bora watu wakazingatia mfumo bora wa maisha, ikiwemo aina ya ulaji na kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, saratani, presha, ugonjwa wa moyo ndiyo yanayoongoza na kusababisha vifo vingi vya watu, hivyo Serikali imeendelea kuhamasisha na kutoa elimu wananchi wazingatie hilo,” alieleza Kandege. 

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati alisema mkutano walioufanya na Rais Dk. John Magufuli umekuwa wa mafanikio makubwa katika sekta ya afya.

“Kuajiri madaktari 1,000 kwa wakati mmoja ni jambo kubwa sana na pia ametupa jengo kwa ajili ya kufanya shughuli zetu.

“Sisi tunamshukuru Rais na tutaendelea kuwa pamoja na Serikali katika kutoa matibabu bora kwa wananchi,” alisema Dk. Osati.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles