25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

LEMA AVUNJA UKIMYA KUZUIWA MIKUTANO YAKE

Na MWANDISHI WETU

-ARUSHA

JESHI la Polisi mkoani Arusha, limepiga marufuku mikutano ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni maandalizi ya mitihani ya darasa la saba na mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Lema alisema kuzuiwa kwa mikutano yake ni hujuma za wazi za kumdhibiti, ili asiweze kuzungumza na wapigakura wake.

Alisema barua ya kuzuiwa mikutano hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha E.M Tille, ni moja ya mkakati mahususi wa kiongozi huyo kutafuta nafasi ya kupanda cheo.

“Nina masikitiko makubwa sana kuzuiwa kwa mikutano yangu ambayo ni moja ya utaratibu wangu wa kusikiliza kero za wapigakura wangu kabla sijakwenda bungeni.

“Leo nimeletewa barua ya polisi ya kuzuiwa mkutano wangu ambao nilitaka kuufanya kesho (leo) katika eneo la Sokoni.

“Baada ya kupata barua hii nilimpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na kumweleza masikitiko yangu ya kuzuiwa kuzungumza na wapigakura wangu.

“Naye alinitaka niwasiliane na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, ambaye naye hakunijibu kiungwana zaidi ya kunitolea lugha za ukali.

“Licha ya hali hiyo, nilimuuliza mfano kesho (leo) mkutano nilipanga kwenye eneo la soko na si shule, labda aniambie ni uwanja gani ambao wanafunzi hao wa darasa la saba wapo, alishindwa kunijibu zaidi ya kunitolea ukali.

“Ila ninachotaka kusema mbele ya umma ‎na hiki kinachoendelea polisi, ni moja ya mkakati wa kutafuta ‘promotion’ maana wapo wengi kila aliyepambana nami alipanda cheo, akiwemo Andengenye (Thobias) ambaye alikuwa RPC na baadaye akapandishwa kuwa Kamishna wa Polisi, mwingine ni Boaz naye vivyo hivyo.

“Nahisi hata OCD wa sasa naye anatafuta cheo. Ila nataka kuwaambia huu ni mkakati wa kunishughulikia, huwezi ukaniambia kama nikitaka kuendelea na mikutano nisubiri baada ya Septemba 8,” alisema.

‎Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema pamoja na hali hiyo hakuna mkakati utakaofanikiwa dhidi yake, kwani yeye kwa sasa ana kazi aliyopewa na wapigakura wake ya kusimamia maendeleo ya Arusha Mjini.

“Si huyo OCD, hata huko nyuma Gambo akiwa DC tulitofautiana mbele ya Naibu Waziri Selemani Jafo na baada ya muda alipandishwa cheo na kuwa RC ‎wa Arusha.

“Kwa hali hiyo huu ni mkakati ovu dhidi yangu, ila ninawaomba wapigakura wangu wasiwe na hofu na nitakwenda kata zote kama ilivyopangwa,” alisema.

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, kuzungumzia zuio hilo simu yake iliita muda mrefu bila kupokewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles