25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Lema amshambulia Polisi Chagonja

Paul Chagonjapg6Na Maregesi Paul, Dodoma

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), jana alimshambulia kwa maneno makali Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, kuwa anaweza kuwa anashirikiana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi na kupora silaha.

Lema alitoa maneno hayo makali ya kumshambulia Chagonja bungeni jana, wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Akichangia hoja hizo, Lema aliliambia Bunge kuwa Chagonja anaweza kuwa anahusika katika matukio ya ujambazi katika vituo vya polisi kwa sababu anataka kudhoofisha utendaji kazi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.

Katika maelezo yake hayo, Lema alilifananisha taifa na chumba kinachotumiwa na vijana wa kihuni kuishi ambacho hakina utaratibu unaoeleweka wa muda wa maakuli na malazi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, geto ni mahali ambapo watu wanaishi bila kufuata utaratibu, yaani katika geto, wakati wa kulala anayewahi ndiye anayelala kitandani.
Geto chakula kinapopikwa kinaweza kuliwa hata kama hakijaiva, kwa hiyo nchi hii naifananisha na geto kwa sababu watu wanaiba fedha za umma kama wanavyotaka.

“Katika ripoti za Bunge zilizosomwa hapa jana (juzi) zimejaa wizi, kila ukurasa wa taarifa ya Zitto ni wizi tu, wizi tu, hivi huu wizi utakwisha lini? Hata zile bunduki zinazoibwa katika vituo vya polisi zinaweza kuwa ni ‘sabotage’ (hujuma), zinazofanywa na Chagonja dhidi ya IGP,” alisema Lema.

Alisema amefanya uchunguzi wake binafsi uliobaini kuwa Jeshi la Polisi limegawanyika na kwamba haamini kama Rais Jakaya Kikwete amekwishafanya mabadiliko ya uongozi ndani ya jeshi hilo.
Lema alizungumzia pia utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri na kueleza kuwa baadhi yao hawajui wajibu wao na alitoa mfano wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akimshutumu kwa kusafiri kila mara kwenda Ulaya.

“Nchi hii ina-suffer financially, nchi hii haina fedha, lakini utashangaa fedha zinaibwa kila siku. Kwa kuwa nchi hii mnaiendesha mnavyotaka ndiyo maana hata ‘mamodo’ wanaanza kufikiria kuwa wanaweza kuwa marais wa Tanzania.

“Baraza la Mawaziri linapokutana mnajadili mambo yasiyofaa, yaani utashangaa mawaziri siku hizi wanashinda kwenye instagram, wanashinda kwenye facebook na wengine wanashinda kwenye mitandao ya kijamii na wengine kazi zao ni kupiga picha tu.

“Kwa mfano, huyu Waziri wa Maliasili na Utalii, yeye kazi yake ni kusafiri tu nje ya nchi na anadiriki kusafiri na Aunt Ezekiel, yaani mbuga za wanyama ziko Tanzania yeye anashinda uwanja wa ndege, nawaambia kama Mungu akiamua kutunga amri ya 11 katika zile amri kumi, hiyo amri atakayoiongeza itakuwa Usiwe CCM,” alisema Lema.

Alisema ikitokea mawaziri wa Tanzania wakapelekwa nchini Tunisia wangeishachukuliwa hatua kali kwa sababu Serikali ya nchi hiyo haiwavumilii wabadhirifu wa fedha za umma.

Mbunge mwingine aliyechangia hoja hiyo, Tundu Lissu wa Singida Mashariki (Chadema), alisema wizi unaoripotiwa bungeni kila mwaka umeanza kuwafanya wananchi wapende kusikia taarifa mbaya badala ya taarifa nzuri.

“Tatizo kubwa lililoko serikalini ni ‘impunity’, yaani watu wanakula fedha za umma hawachukuliwi hatua. Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa nini wizi huu haukomi, kwa nini hauishi.”

Lissu alisema umefika wakati mawaziri wanaosimamia wizara zinazotajwa kuhusika na wizi wachukuliwe hatua na wabunge kwa sababu wanawamudu na wakilitekeleza hilo wezi watakoma.

Naye Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM) alipopata fursa ya kuchangia mjadala huo alieleza kutoridhishwa na wizi wa fedha za umma, lakini aliwakosoa wanaoishambulia serikali kwa kuwataka wawe na busara, kwa kuwa katika baadhi ya maeneo imejitahidi kufanya vizuri.

Shekifu alitaka ufanyike uchunguzi wa kina katika halmashauri zote nchini ambao utawabaini wabadhirifu na majina yao yatajwe bungeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles