24.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 15, 2024

Contact us: [email protected]

Waghushi nyaraka na kujichotea mamilioni NSSF

Na Elias Msuya
MAOFISA wawili wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce) wamefikishwa katika bodi ya chuo hicho wakituhumiwa kuchukua kiinua mgongo chao wakati wakiendelea na kazi.
Taarifa kutoka kwa chanzo chetu ndani ya chuo hicho zinamtaja Yobu Msigwa na Telesphory Nkembo, wanaofanya kazi katika Ofisi ya Rasilimali Watu ya chuo hicho wakidaiwa kughushi sahihi na kutumia mihuri ya chuo kujipatia fedha za mafao ya kiinua mgongo kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Msigwa alifanya kosa hilo mwaka 2012, lakini aliendelea na kazi hadi alipogundulika mwishoni mwa mwaka 2014.
“Katika barua yake ya kuomba mafao alidanganya na kuandika kuwa alikuwa ni mfanyakazi wa mkataba na mkataba wake ulikwisha na kwamba alifanya kazi katika mradi wa Benki ya Dunia ambao ulikwisha kwa kipindi hicho. Pia alifanikiwa kujihamisha mfuko wa hifadhi ya jamii kutoka NSSF na kwenda LAPF kinyume cha sheria,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa Nkembo, naye anadaiwa kughushi sahihi na kutumia mihuri ya chuo ili kutaka kujipatia kiinua mgongo chake kinyume cha sheria mwaka 2014.
“Ili apate kiinua mgongo chake aliwaandikia NSSF barua kuwa kaacha kazi Mkwawa (Resignation letter), ikionesha kuwa anaomba apewe kiinua mgongo chake kwa kuwa hakuwa mfanyakazi tena wa Mkwawa. Jambo hili lilipofuatiliwa na NSSF waligundua kuwa maofisa hawa waliandika uongo ili wajipatie fedha kinyume cha sheria,” kiliongeza chanzo hicho.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Bernadetta Kiliani, alikiri kuwepo kwa maofisa hao, akisema kuwa Msigwa alishapata fedha zake, huku Telesphory akiwa bado anasubiri. Hata hivyo, hakutaja kiasi cha fedha walizopata.
“Hizo taarifa ni za kweli, lakini Nkembo alikuwa bado hajapata. Hilo jambo kwa sasa liko kwenye vikao vya kamati ya nidhamu. Lilipelekwa kwenye bodi ya chuo lakini haikuridhika na sasa limerudishwa kwenye kamati ya uteuzi. Hata kesho (leo) tuna vikao vya kuwajadili…” alisema Profesa Kiliani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, naye alikiri kufahamu suala hilo:
“Ni kweli kuna madai hayo, kesi yao inashughulikiwa na vyombo vya nidhamu vya chuo. Walileta mapendekezo kwenye bodi Januari 21, lakini haikuridhishwa na adhabu walizopewa,” alisema Profesa Mukandala na kuongeza:
“Mimi sikuwepo kwenye kikao hicho, ila nilipata taarifa. Lile ni kosa kubwa, lazima hatua pia ziwe kubwa kwa kufuata sheria,” alisema.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Magheke MJ, alikiandikia chuo hicho barua Mei 28, 2014 yenye kumbukumbu namba NSSF/IRI/203/VOL.XXI/117 yenye kichwa cha habari:- RE: TERMINATION/RESIGNATION LETTER WHILE STAFF ARE STILL IN SERVICE, ambayo iliuomba uongozi wa chuo kukomesha mchezo huo mchafu wa kuomba mafao kwa maofisa wa rasilimali watu kwa kusema uongo huku wakiwa bado wameajiriwa.
Barua hiyo imetaja kifungu cha sheria ya NSSF Na. 28. ya mwaka 1997 ambayo inazuia mfanyakazi kuomba mafao huku akiwa bado ameajiriwa na sheria ya Mamlaka ya kudhibiti Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) Namba 8 ya mwaka 2008, inayozuia wanachama wa mfuko mmoja kuhamia mfuko mwingine. Barua hiyo iliuomba uongozi wa chuo kuchukua hatua na kulifuatilia suala hili kwa kina, jambo ambalo halikufanyika.
Mbali na barua hiyo, NSSF Iringa siku hiyo hiyo ya Mei 28, 2014, walileta barua nyingine kwa Mkuu wa Chuo ya kuonyesha nia ya kuwashtaki maofisa hao, Msigwa na Nkembo, yenye Kumb: Na. NSSF/IRI/203/VOL.XXI/118 ambayo inaonesha wamevunja sheria ya NSSF Na.28 ya 1997 Kifungu 72(1) (a) na sheria ya SSRA na.8 ya 2008 kifungu na.29 (3)(a) kinachokataza mteja wa mfuko mmoja kuhamia mfuko mwingine.
Kutokana na uvunjifu huo wa sheria, NSSF imeonyesha nia ya kuwashitaki watumishi hao.
“Pamoja na kuvunja sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii, bado wana makosa ya kuvunja sheria za utumishi wa umma (Public Relations Act na. 6 ya 2004),” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilisema maofisa hao wametiwa hatiani kwa makosa ya kutaka kujipatia na kujipatia fedha kinyume cha utaratibu, matumizi mabaya ya ofisi ya umma, rushwa, kutokuwa waaminifu, waadilifu, kuandika na kusema uongo pamoja na kughushi.
Hata hivyo, Profesa Kiliani hakufafanua kwa nini maofisa hao hawakuchukuliwa hatua tangu walipojulishwa na NSSF, Mei 28, 2014, jambo linaloashiria mazingira ya kulindana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles