MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amekamatwa akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi.
Lema alikamatwa jana saa 12 asubuhi akiwa nyumbani kwake Njiro, mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa alihojiwa dhidi ya matamshi ya uchochezi kabla ya kwenda kupekuliwa nyumbani kwake.
Akizungumza ofisini kwake jana na MTANZANIA Jumamosi, Kamanda Mkumbo alisema Lema atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi pamoja na kuhojiwa dhidi ya tuhuma anazotuhumiwa nazo.
Alisema Lema anatuhumiwa kuwachochea wakazi wa Arusha kuandamana siku ya Septemba mosi kupinga kile ambacho kimekuwa kikidaiwa na Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema) kuwa ni Serikali iliyoko madarakani kutawala kwa mabavu na kuchochea wananchi kuwa tayari kupambana na polisi.
“Ni kweli tumemkamata jana saa 12 asubuhi nyumbani kwake Njiro kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi, bado tunaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na kufanya naye mahojiano na kisha atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Mkumbo.
Aliyataja maneno ya uchochezi ambayo Lema anatuhumiwa kuyasambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni maandishi yanayosomeka; ‘nchi hii itaingia kwenye umwagaji damu, nchi itaingia kwenye hasara kubwa kwa sababu mamlaka yamezidi fikra zao, uwezo wa kufikiri na kama mauti imepoteza utukufu wake hakuna statement (tamko) linaloweza kurudisha nyuma Arusha kuandamana.’
Taarifa za kukamatwa kwa Lema zilianza kusambaa mapema jana asubuhi na muda mfupi baadaye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Bukhay, alizithibitisha.
Akizungumza na MTANZANIA, Bukhay alisema Lema alikamatwa jana asubuhi akiwa nyumbani kwake na hadi saa 4 ilikuwa haijafahamika sababu ya kukamatwa kwake.
“Mpaka sasa hatujajua amekamatwa kwa tuhuma zipi, tupo hapa kituoni tunasubiri kwa sababu bado hawajaanza kumhoji,” alisema Bukhay.
Mkewe Lema anayefahamika kwa jina la Neema, ambaye jana alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam, naye alithibitisha kukamatwa kwa mumewe kwa kueleza kuwa taarifa za tukio hilo amezipata kutoka kwa wasaidizi wa kazi wa nyumbani kwake.
“Ni kweli nimepigiwa simu muwe wangu amekamatwa na askari polisi, wamemshambulia na kumsababishia usumbufu mkubwa. Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya KK naye walimshambulia baada ya kuwataka askari hao wajitambulishe.
“Mlinzi alitaka ufafanuzi wa ujio wao. Lakini pia saa 7 mchana huu tunavyozungumza hapa askari polisi wapo nyumbani wameenda kufanya upekuzi pamoja na Lema. Cha ajabu pia wamezuia mwanangu asiingie ndani ya nyumba baada ya kushushwa na gari la shule.
“Namwombea kwa Mungu mume wangu azidi kuwa jasiri katika kutetea ukweli,” alisema Neema.
Juzi akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ambako Diwani wa Kata ya Sombetini (Chadema), Alli Bananga, alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za uchochezi na kupewa dhamana, Lema alisema diwani huyo hakuwa na makosa ya kufikishwa mahakamani.
Lema alisema Bananga alikamatwa kwa maelekezo ya vyombo vya dola ambavyo alivitaka kuacha woga.
“Septemba mosi, mwaka huu maandamano ya Ukuta yapo palepale, tutapambana na polisi siku hiyo na kama hili ni kosa nawaomba waje kunikamata. “Lakini ningependa Diwani Bananga angeenda mahabusu siku 14 ili atusaidie kuhamasisha maandamano huko gerezani. Tupo tayari kwa ajili ya mauti na si magereza,” alisema Lema.
Wakati huo huo Mwandishi wetu kutoka Bariadi mkoani Shinyanga anaripoti kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalim na wenzake watatu, jana walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Simiyu na kusomewa mashtaka ya uchochezi.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, John Nkwabi, Wakili wa Serikali, Mafuru Moses, alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 23 mwaka huu katika Kijiji cha Ndutwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Renatus Nzemo na Oscar Kaijage ambao pia ni viongozi wa Chadema.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Nkwabi alieleza kuwa amepokea hati ya kiapo kutoka Jeshi la Polisi iliyowasilishwa na Mkaguzi wa Polisi, Msoforo Kasurura, ikiomba washtakiwa wote wasipewe dhamana.
Wakili wa upande wa utetezi, Martin Sabini, alipinga wateja wake kunyimwa dhamana kwa kueleza kuwa mashtaka yanayowakabili yana dhamana.
Hakimu Nkwabi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30, mwaka huu ambapo upande wa mashtaka utatakiwa kujibu maombi ya dhamana ya upande utetezi hivyo washtakiwa walipelekwa Gereza la mahabusu la Wilaya ya Bariadi.
Naye Samwel Mwanga kutoka wilayani Maswa anaripoti kuwa viongozi 17 wa Chadema wa wilaya hiyo jana walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujaribu kushawishi wenzao kutenda makosa ya uchochezi.
Waliofikishwa mahakamani ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Maswa, Peter Shiyo (39), Katibu wa Chadema wa Wilaya, Flora Msuka (31), Katibu wa Bawacha wa Wilaya, Elias Matondo (37) na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Maswa Mashariki, Waziri Peter (46).
Wengine ni wanachama wa chama hicho, Bundala Baya (30), Edward Makoye (63), Silivester Ngwege (60), Frank Makaranga (31), Selemani Kombe (39) na Mapambano Jackson (37).
Wamo pia Nkuba Magwila (40), Ndebile Paul (27), Edga Ngasa (32), Lucas Nkuba (39), Laurenti Mahembo (36) na Mwajuma Said (40).
Makada hao wa Chadema walisomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa, Tumaini Marwa na mwendesha mashtaka wa polisi, Mkaguzi Swedy Nassibu.
Nassibu alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kinyume cha sheria, sura 19 ya kanuni ya adhabu kifungu cha 380 na 390 mnamo Agosti 25, mwaka huu saa 7:00 mchana katika Ofisi ya Wilaya ya Chadema iliyoko eneo la Mnadani.
Washtakiwa wote walikana mashtaka na kuiomba mahakama kuwapatia dhamana.
Hakimu Marwa aliamuru washtakiwa hao kupelekwa rumande baada ya kukubaliana na ombi la upande wa mashtaka kuwa iwapo watadhaminiwa wanaweza kusababisha kufanyika kwa maandamano na mikutano iliyopewa jina la Ukuta ambayo inalenga kuhatarisha amani na utulivu.
Hata hivyo, mahakama ilikubali maombi ya mshtakiwa, Flora Msuka ambaye ni mjamzito na pia anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 2 mwaka huu ambapo mahakama iliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi.