Janeth Mushi, Arusha
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), leo amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akikabiliwa na shitaka moja la kuamsha hisia kwa wananchi kwa njia isiyo halali.
Mapema leo asubuhi, mbunge huyo aliachiwa huru katika mahakama hiyo katika kesi ya uchochezi dhidi Rais John Magufuli, aliyokuwa anakabiliwa nayo baada ya upande wa jamhuri kushindwa kufikisha ushahidi na kasha kufunguliwa kesi hiyo mpya ya kuamsha hisia kwa wananchi.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nestory Barrow, Wakili wa Serikali Rose Sule amedai mbunge huyo alitenda kosa hilo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara Oktoba 22, mwaka 2016 ambapo alitoa maneno yaliyochochea hisia hasi kwa jamii ya Watanzania wa ngazi tofauti katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambapo alidhaminiwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya dhamana ya Sh Milioni tano.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, mwaka huu itakapotajwa tena kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.