Na Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Mamlaka ya Udhibithi wa Usafiri Ardhini (LATRA) mkoani Kilimanjaro imekamata gari lenye namba za usajili T 571 BHQ kwa kujitengenezea chati yenye gharama za nauli kinyume na zilizopangwa na Serikali.
Akizungumza katika Mkutano na Wadau wa Usafirishaji kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya LATRA Mkoa wa Kilimanjaro, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo mkoa, Paul Nyello amesema kuwa katika ukaguzi wa nauli kwenye magari ya Marangu wamefanikiwa kukamata gari hilo kwa kukiuka utaratibu huo uliowekwa na Serikali.
“Tumekamata gari hilo na tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya wahusika hao ambapo amewataka wamiliki wa magari na madereva kufuata sheria na taratibu za usafirishaji,” alisema Nyello.
Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani wameendelea na oparesheni maalum ya kukamata kosta zinafanya safari za usiku za Moshi- Dar es Salaam kinyume cha utaratibu na kuvunja sheria za leseni za usafirishaji.
Nyello amesema baadhi ya wamiliki wa magari gari hayo wamekuwa wakifanya biashara hiyo ya kusafirisha abiria nyakati za usiku jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha ya watu.
Amesema kuwa Kosta hizo zimekuwa zikipakia abiria kwa kificho ikiwemo kuwafuata abiria majumbani mwao.
Amesema Kosta hizo zimesajiliwa kwa ajili ya huduma za kukokidishwa kwa safari maalum ili kutoa huduma katika barabara za Arusha Moshi.
“Tumekuwa tukizikamata na kuzipiga faini lakini bado wamekuwa wakikuka na kurudia makosa hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa maderava hao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwemo abiria kujifunga khanga kwa madai ya kwenda kwenye msiba.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabara mkoa wa Kilimanjaro, Pili Misungwi ametaka wasafirishaji kufuata utaratibu na kutoa ushirikiano ili kudhibiti tatizo hilo .
Amesema kuwa wamekuwa wakifanya doria za usiku na kwamba tayari wameweka kizuizi cha polisi eneo la Mwanga.
Baadhi ya wasafirishaji wameiomba LATRA mkoa Kilimanjaro kuzifutia usajili kosta hizo kutokana na kwamba wamekuwa wakiwaharibia biashara wafanyabiashara wa mabasi makubwa ambao wanalipa kodi za Serikali.
Rodriki Urono amesema kosta hizo zimekuwa zikiwaharibia biashara wamiliki wa mabasi kwa kuwafanya wakose abiria.