24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI RAILA AMESHINDWA?

 

 

Raila ambaye aligombea nafasi ya urais kwa mara ya kwanza mwaka 1997 na kushika nafasi ya tatu kabla hajarejea tena ulingoni mwaka 2007, 2013 na mwaka huu, kushindwa kwake huko kumeelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa kunatokana na sababu kadha wa kadha.

Sababu kubwa inayoelezwa wachambuzi hawa ni pamoja na kitendo cha kurudia kwake  mikakati na kukubali kucheza ngoma ya wapinzani wake.

Wachambuzi hao wa masuala ya kisiasa nchini Kenya wanasema, Odinga ameponzwa na uamuzi wa kumchagua kwa mara ya pili mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hilo ni kosa kubwa kiufundi kwani kuliwapa urahisi wapinzani wake kushughulika na madhaifu waliyoyaona katika uchaguzi uliopita ambao walisimama pamoja.

Wanasema, wanasiasa hao waligombea kwa pamoja katika uchaguzi wa mwaka 2013, hivyo kitendo hicho wamerudia tena mwaka 2017.

Wachambuzi hao wanasema, Odinga alitakiwa kuwa na mgombea mwenza mpya mwenye mawazo mapya zaidi.

Kuhusu kukubali kucheza ngoma ya mgombea wa Jubilee Uhuru Kenyatta, wanasema Raila alipaswa kusimamisha chama chake cha ODM bila kufuata mkumbo wa kuunganisha vyama kama ule wa Jubilee.

Wanasema ODM ni chama chenye nguvu ambacho kingeweza kusimama peke yake katika siasa za Kenya.

Kwa sababu hiyo wanasema, hakikupaswa kuungana na vyama dhaifu kama Wiper, Ford-Kenya, Chama cha Mashinani na ANC.

Wanasema hata kuanzisha NASA kulionekana wazi kumuwia vigumu Raila hususan akiwa jukwaani kuwapigia kampeni wagombea wa ODM na wale wa vyama vingine.

Tofauti na wapinzani wake wa Jubilee wachambuzi hao wanasema Raila alifanya hivyo kwa kujidanganya anaweza kudhibiti  ile dhana iliyokuwa ikitumiwa na wapinzani wake hao ya ‘6-piece suit’ yani kura zote za Rais, Gavana, Seneta, Mbunge, Mwakilishi wa Wanawake na Mjumbe wa Baraza ya Kaunti zipigiwe chama kimoja.

Mfano mzuri ni Kaunti ya Mombasa ambapo katika kinyang’anyiro cha ugavana NASA ilipata wakati mgumu kuchagua nani kati ya Hassan Joho wa ODM na Hassan Omar wa Wiper.

Joho alipopanda jukwani alishangiliwa wakati Omar alizomewa hivyo idadi za kura za Kenyatta kuongezeka kulitokana na wafuasi wa Omar kwa ‘hasira’, kumpigia kura ya urais Kenyatta na za gavana kuelekeza kwa Omar.

Kwa makosa kama hayo baadhi wanaamini Raila alipaswa ajilaumu yeye mwenyewe na si kulalamika kuibiwa kura au kuporwa ushindi kama ilivyokuwa mara zote alizogombea.

Pamoja na hayo yote wapo wanaoamini  mwanasiasa huyo ambaye ni mtoto wa mmoja wa waasisi wa Taifa hilo Jaramong Odinga anatajwa kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa nchini Kenya, hivyo kushindwa kwake si jambo linaloweza kuchukuliwa kirahisi rahisi.

Raila ambaye miongoni mwa wakenya na mashabiki wake anajulikana kwa majina ya Agwambo, Tinga, Baba, RAO na Jakom amegombea urais mwaka huu akiwa na umri wa miaka 72 jambo ambalo wengi wanaliona kama kipindi chake cha mwisho.

Amewahi kupata misukosuko mingi tangu akiwa shule ikiwamo kuwekwa kizuizini baada ya kuhusishwa na jaribio la kumpindua aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi mwaka 1982 amekuwa mwanasiasa ambaye haiba yake imekuwa ni vigumu kuileza bayana miongoni mwa Wakenya.

Aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1997 dhidi ya Rais Daniel Arap Moi, akitumia tiketi ya chama cha National Development Party na kupata kura 667,886.

Mwaka 2007 aligombea dhidi ya Mwai Kibaki na kupata kura 4,352,993 sawa na aslimia 44.07.

Mwaka 2013 aligombea dhidi ya Uhuru Kenyatta akapata kura 5,340,546 sawa na asilimia 43.70.

Mwaka 2017 amegombea dhidi ya Uhuru Kenyatta na kushindwa kwa mara ya nne mfululizo.

Kenyatta aligombea mara ya kwanza mwaka 2002 dhidi ya Mwai Kibaki akashindwa. Mwaka 2013 aligombea dhidi ya Odinga akashinda. Mwaka 2017 ametetea tena kiti chake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles