Kadama Malunde -Shinyanga
MBUNGE wa Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi amekabidhi gari la Wagonjwa lililotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ufadhili wa Global Fund (RSSH) kwa ajili ya kituo cha afya cha Mbika Kata ya Ushetu.
Kwandikwa Alikabidhi gar hilo mwishoni mwa wiki katika hafla fupi ya makabidhiano ambayo imehudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Ushetu pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha.
Alisema gari hilo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli katika kuboresha sekta ya afya ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya.
“Naishukuru serikali kwa kusikia kilio cha wana Ushetu kuhusu changamoto ya gari la wagonjwa lakini pia nimshukuru pacha wangu Azza kwa ushirikiano anaoendelea kuutoa katika jimbo hili na leo tumefanikiwa kupata gari kwa ajili ya wananchi.
“Gari hili linaweza pia kutumika kuhudumia pia maeneo yanayozunguka kituo cha Mbika kama vile Ulowa na Uyogo ingawa kituo chake kikubwa kitakuwa ni hapa Mbika. Naomba gari hili litunzwe na litumike kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Kwandikwa.
Katika hatua nyingine Kwandikwa amekabidhi ndoo 28 za kunawia mikono zitakazogawiwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ushetu, vitakasa mikono ‘ Sanitizers’,sabuni za maji, Barakoa ’Surgical Masks’ kwa ajili ya watumishi wa afya kituo cha afya Mbika.
Pia alichangia Sh milioni moja kwa ajili ya Saccos ya akina Mama Uyogo huku Mbunge wa Viti Maalumu, Azza Hilal Hamad akichangia Sh 300,000 kwa ajili ya Saccos hiyo.
Awali akizungumza, Mbunge Azza Hilal Hamad, aliishukuru serikali kwa kutekeleza ahadi ya kuleta gari kwa ajili ya wagonjwa aliloliomba kwa ajili ya Kituo cha Afya Mbika akieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli inatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.
“Mwaka 2018 wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya ziara katika Jimbo la Ushetu nilimuomba atusaidie kupata gari la wagonjwa, alikubali na leo hii gari limefika katika kituo cha afya cha Mbika ili wananchi wapate huduma. Namshukuru sana kaka yangu Elias Kwandikwa kwa ushirikiano anaotoa kwa wabunge wa mkoa wa Shinyanga katika kuwahudumia wananchi,”alisema Azza.