25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

KUZAA MFULULIZO KUNAVYOCHANGIA MAMA KUPATA MTOTO NJITI

mjamzito

Na VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

KUZAA watoto wengi ni mojawapo ya desturi zilikuwapo katika jamii nyingi za kiafrika, enzi za mababu zetu familia iliyokuwa na watoto wengi ilipewa heshima ya kipekee katika jamii.

Familia iliyopata idadi kubwa ya watoto ilijiona kuwa bora kuliko zingine na hapo baba mwenye familia husika alijiona kuwa ni shujaa.

Pamoja na kuwa jitihada nyingi zimefanyika kuelimisha jamii umuhimu wa kupanga uzazi, wapo walioipokea elimu hiyo lakini pia wapo wachache ambao wanaendelea kutekeleza desturi ile ya kuzaa watoto wengi.

Wataalamu wanasema mama anayejifungua watoto wengi yupo kwenye hatari ya kuzaa mtoto kabla ya kutimiza muda wake halali wa miezi tisa.

Watoto wanaozaliwa kabla ya muda unaokusudiwa mara nyingi huwa na uzito pungufu, wengi wetu tunawaita watoto hawa ‘njiti’.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto Wachanga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Augustino Masawe, anasema ingawa bado haijajulikana wazi sababu zinazosababisha mama kuzaa mtoto njiti lakini kitendo cha mama kuzaa mfululizo kinatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochochea mama kuzaa mtoto njiti.

“Idadi ya watoto njiti inazidi kuongezeka kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, hapa Muhimbili kwa mfano tangu kuanzishwa kwa kitengo cha kulea watoto hawa katika miaka ya 1990 tulikuwa tukilaza watoto 30 lakini leo hii idadi imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 1,000.

“Zipo sababu nyingi zinazochangia ongezeko hili zikiwamo mama kuzaa mfululizo. Unajua afya ya mama ni ya muhimu mno kuizingatia tangu mtoto akiwa tumboni, akizaliwa na hadi anapokuja kushika mimba.

“Lakini tatizo linakuja kwamba huyu mama mimba yake ililelewa kwa shida na yeye kutokana na umasikini anakuja kubeba mimba na anailea kwa shida na wengi ni katika umri mdogo halafu unakuta mwingine anazaa pasipo kupumzika, hili ni tatizo,” anasema.

MLANGO WA KIZAZI

Anasema mama anayejifungua watoto mfululizo bila kujipa muda wa kupumzika mlango wake wa kizazi huwa katika hatari ya kufungua wakati wowote ikilinganishwa na mama anayezaa kwa kupumzika na kuacha kipindi fulani cha muda kupita.

“Jambo jingine ambalo tunaona linapaswa kufanyiwa kazi ni ujenzi wa afya ya mama. Hapa nchini tunaona kina mama wengi wanaojifungua hii leo ni watoto kwa maana ya kwamba wanajifungua chini ya umri wa miaka 18 unaoshauriwa kitaalamu.

“Hawa ni karibu asilimia 20, mara nyingi hawa huzaa watoto njiti kwa sababu viungo vyao huwa havijakomaa kuweza kuhimili ile hali ndiyo maana inashauriwa familia ziwaache watoto wakue kwanza,” anasema.

Daktari huyo anasema wanawake wengine hujikuta wakizaa watoto njiti au hupoteza mimba zao kabisa kutokana na matatizo mbalimbali ikiwamo upungufu wa damu, malaria za mara kwa mara, shinikizo la damu na magonjwa mengine.

“Pamoja na hayo maisha duni husababisha wengi kuingia katika tatizo zaidi kuliko wale wanaoishi maisha yenye unafuu. Kwa mfano hapa Dar es Salaam unaweza kuona hali hiyo zaidi katika maeneo ya Mbagala au Tandale lakini si maeneo kama Oysterbay.

“Mama mwenye mimba ya pacha naye huwa kwenye uwezekano wa kuzaa mtoto mmoja akiwa njiti, ndiyo maana tunashauri sana jamii izingatie mno kujenga afya ya mama kwani ni muhimu ili aweze kupata mtoto aliye na afya bora katika maisha yake,” anasema.

USHUHUDA WA MAMA

Mariam (si jina lake halisi) ni mmoja wa wanawake ambaye amejifungua mtoto njiti, alilazwa Muhimbili tangu alipojifungua akiwa chini ya uangalizi maalumu.

“Huyu ni mtoto wangu wa pili, wa kwanza nilijifungua salama na alifikisha kilo kamili, lakini huyu alizaliwa akiwa njiti, wakati wa ujauzito wake niligundulika kuwa nina shinikizo la juu la damu.

“Wakati huo mimba ilikuwa imefikisha miezi saba, daktari wangu akanishauri nifanyiwe upasuaji kumtoa mtoto ili kuokoa maisha yake,” anasema.

Anasema alikubali jambo hilo hata hivyo hakuamini macho yake alipoonyeshwa mtoto wake huyo aliyejifungua.

“Alikuwa mdogo mno, niliogopa lakini nilimshukuru Mungu na nikamtunza kwa msaada wa madaktari hapa kitengo cha Kangaroo na leo hii nimeruhusiwa kurudi nyumbani.

“Kulea mtoto njiti kunahitaji umakini mkubwa maana watoto wa aina hii ukikosea kidogo tu ni rahisi kupoteza maisha,” anasema.

HALI ILIVYO MUHIMBILI

Mkuu wa Kitengo cha Watoto Njiti wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Edna Majaliwa, anasema takwimu za hospitali hiyo zinaonesha idadi hiyo imeongezeka maradufu kutoka watoto 30 mwaka 2012 hadi kufikia watoto 1,500 mwaka 2015/16.

Anasema hiyo inamaanisha kuwa kuna ongezeko la watoto njiti katika kipindi cha miaka minne pekee.

VIFO VYA WATOTO

Kwa mujibu wa takwimu za WHO wastani wa watoto milioni 15 huzaliwa njiti ulimwenguni kote kila mwaka.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk. Julieth Magandi, anasema mtoto anapozaliwa njiti huwa ni rahisi kupata madhara mengi hivyo huhitaji kupatiwa uangalizi wa hali ya juu.

“Inakadiriwa hapa nchini asilimia 13 ya watoto huzaliwa wakiwa na uzito pungufu na huchangia kwa takriban asilimia 86 ya vifo vya watoto wachanga.

“Iwapo atapewa uangalizi wa karibu huwa ni rahisi kupoteza maisha, huhitaji kupata joto la kumsaidia kukua na kwa kuwa mapafu yake hayana uwezo mzuri wa kupumua huhitaji msaada wa ziada.

“Uzito pungufu wa kuzaliwa una madhara makubwa na huathiri ukuaji wa watoto wachanga kuishi na kukua,” anasema Dk. Magandi.

Daktari huyo anaongeza; “Asilimia 27 ya vifo vya watoto hao husababishwa na magonjwa yatokanayo na vimelea vya bakteria na matatizo ya upumuaji.

“Tunatumia njia ya kangaroo ambapo mama humfunga mtoto kifuani pake na kukaa naye, hivi karibuni tumeweza kupata dawa ya kukomaza mapafu lakini ni ghali, dozi kwa mtoto mmoja ni Sh milioni 1.2.

“Wale wanaozaa pacha nao mara nyingi hutokea wakapata mtoto njiti, lakini pia asilimia 20 ya wanaojifungua siku hizi nchini ni watoto yaani wapo chini ya umri wa miaka 18 unaoshauriwa, hawa wapo katika hatari ya kuzaa watoto njiti,” anasema.

Dk Magandi anasema hatua ya Muhimbili kuanzisha kitengo cha Kangaroo imesaidia kuokoa maisha ya watoto wengi waliozaliwa wakiwa njiti.

“Katika muongo mmoja uliopita Tanzania ilikuwa kati ya nchi zilizoweza kufikia lengo namba nne la Mpango wa Malengo ya Milenia la kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga.

“Muhimbili kupitia mpango wa Kangaroo tumeweza kupungua vifo vya watoto hawa, wengi wanapona kwa kiwango cha asilimia 90 sasa,” anasema.

Anasema kwa kutumia njia ya kangaroo mtoto huweza kupata joto analohitaji moja kwa moja kutoka katika mwili wa mama yake.

“Njia ya kangaroo husaidia mtoto kupata joto zuri, mama hulazimika kumfunga kifuani kwake kwa hiyo huwa rahisi kwake kufuatilia kwa karibu mwenendo wa afya ya mwanawe.

“Lakini pia afya ya mwanawe ikibadilika ghafla na hata akishindwa kunyonya au akipaliwa na maziwa huwa ni rahisi kugundua, kwa njia hii mama anakuwa muuguzi mkuu, hivyo akiona mtoto anapata shida anaomba msaada wa haraka wa daktari,” anasema Dk. Magandi.

WIZARA

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya ya Uzazi, katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hussein Kidanto, anasema kwa wastani mama wa Kitanzania hujifungua watoto kati ya watano na kuendelea.

“Lakini watu wengi hasa vijana hawajafikishiwa elimu ya afya ya uzazi, ndio maana tunashuhudia ongezeko kubwa la ndoa na mimba za utotoni. Hii inamaanisha kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu ya kuelimisha jamii kwa kushirikiana na wadau kusudi taarifa hizo zifike hadi ngazi ya vijiji, huu ndio wakati mwafaka wa kupeleka elimu hii kwani vijana ni taifa la leo,” anasema Dk. Kidanto.

Anasema iwapo vijana watapewa elimu sahihi ya afya ya uzazi itasaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ujauzito na mimba za utotoni kwani watajua wakati gani hasa wanapaswa kubeba mimba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles