Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
MALIASILI nchini ni chanzo kikubwa cha ustawi wa maisha ya wananchi na ni uti wa mgongo wa sekta kuu za uzalishaji kama vile kilimo, utalii, uvuvi na madini.
Uhusiano baina ya ukuaji wa uchumi na usimamizi wa mazingira na maliasili umetiliwa mkazo katika sera ya Taifa ya Mazingira na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA).
Ili sekta yoyote iweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi, ni lazima iwe na utaratibu uliojiwekea katika kuendesha shughuli zilizopangwa ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Moja ya taratibu zilizowekwa ni pamoja na sera, sheria na kanuni zake ambazo hutoa mwelekeo thabiti wa kutunza mazingira na kuenzi rasilimali nchini.
Maliasili ni sekta pana inayojumuisha sekta mbalimbali kama kilimo, ufugaji, afya, madini, viwanda, nishati, maji, utalii, misitu, uvuvi, pamoja na wanyamapori ambazo pia zina sera, sheria na kanuni zake.
Ofisa Miradi wa Taasisi ya Utunzaji Mazingira (Agenda), Fatma Msuya anasema kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa ashiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira kulingana na sheria zinavyoelekeza.
“Faida ya moja kwa moja tunayopata kwa kutunza mazingira vizuri ni kuongeza umri wa kuishi katika ulimwengu huu tulionao.
“Maisha yetu yamekuwa mafupi kwa sababu tumeharibu mazingira. Kuna uhusiano mkubwa kati ya umri wa maisha yetu na uhifadhi wa mazingira,” anasema Fatuma na kuongeza kuwa maisha yetu yanakuwa mafupi kwa sababu tuna kula vitu visivyo na ubora na ambavyo havijengi mwili bali kuharibu mwili.
Fatuma anasema kuwa vyakula hivyo havina ubora kwa kuwa ardhi inayotoa hayo mazao imeharibiwa na shughuli za binadamu.
Naye Ofisa Miradi Mwandamizi ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa AGENDA, Haji Rehani anasema ufuatiliaji ni nyenzo muhimu katika kuweka kumbukumbu za matatizo yanayotokea kwenye jamii.
Rehani anasisitiza jamii na kamati za mazingira pamoja na maafisa watendaji wa kata na vijiji, kuwa na mazoea ya kufunya ufuatiliaji wa maliasili zao na mazingira ili kubaini ukubwa wa matatizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Mazingira wa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Carlos Mbuta anasema hatuna budi kutekeleza sheria na kanuni zake katika kuendeleza rasilimali za nchi yetu kwa kuzielekeza kwenye programu sahihi za hifadhi ya mazingira.
“Elimu, uhamasishaji na matumizi ya sheria ni njia zenye nafasi kubwa katika kuinua kiwango cha mafanikio ya shughuli za hifadhi ya mazingira, hivyo ni muhimu zisimamiwe na viongozi wote.
“Maafisa mazingira katika ngazi mbalimbali ni watendaji wakuu wanaosimamia mazingira na ni tegemeo la Serikali na wananchi kwa ujumla katika kuitekeleza sheria na kuwa na mazingira bora kwa kila Mtanzania,” anasema Mbuta.
Akizungumzia hali ya utunzaji mazingira na maliasili iliyoko Visiwani Mafia, Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Mafia, Gideon Zakayo anasema visababishi vya uharibifu wa mazingira viko vingi ikiwamo uharibifu wa matumbawe, mikoko, uchafuzi, maeneo ya ukanda wa pwani na bahari, bionuwai za bahari utokanao na uvuvi usio endelevu.
“Uharibifu huo pia umeikumba hadi viumbe wa baharini walio hatarini kutoweka kama kasa, pomboo nguva na silikanti,” anasema Zakayo.
Zakayo anatoa mifano ya maeneo yenye athari za wanyapori katika wilaya hiyo, akisema Mafia kwa sasa inasumbuliwa na viboko ambao pia wako hatarini kutoweka kwa kasi zaidi katika visiwa hivyo.
Mwaka jana, jumla ya viboko watatu wameuawa katika vijiji vitatu tofauti ambavyo ni Kirongwe, Ndagoni na Dongo.
Viboko hao walikuwa wakivamia mashamba ya watu. Hivyo, kujikuta ndani ya miaka 3 jumla ya viboko sita wameuawa.
Kwa Wilaya ya Mafia, viboko wanapatikana katika vijiji vya Ndagoni, Chunguruma na Kirongwe na katika vijiji hivi kuna mabwawa ya asili zaidi ya 40 ambayo maji hayakauki na yamekuwa makazi mazuri kwa bioanuai.
Hadi sasa, hakuna sensa iliyofanyika kujua idadi ya viboko waliopo Mafia hata hivyo, ukiachana na suala la viboko, pia uchomaji moto misitu katika visiwa vya Mafia umekithiri ambapo uchomaji huo ni kwa ajili ya maandalizi ya mashamba inayoleta athari kubwa kwa mazingira na mali za watu kushika moto.
Ofisa uvuvi wa Halmashauri ya Mafia, Subira Muya anasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kila kijiji kuwa na sheria ndogondogo ili kuhakikisha usimamizi salama wa mazingira na maliasili kwa vizazi vijavyo.