25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BIASHARA YA WASICHANA UGANDA INAYOWANEEMESHA MAWAKALA

Waganda waishio Marekani wakiandamana kupinga biashara ya binadamu
Waganda waishio Marekani wakiandamana kupinga biashara ya binadamu

NA JOSEPH HIZA,

WALANGUZI wanaochuuza binadamu husafirisha wasichana wa Uganda kupitia Kenya kwenda mataifa ya Mashariki ya Kati na Afrika Kusini wamejiimarisha mno; uchunguzi umebainisha.

Gazeti la Sunday Monitor la Uganda linaripoti kuwa walanguzi hawa wamejenga mtandao unaohusisha maofisa wa polisi, maofisa wa usalama na wafanyakazi wa uhamiaji kutoka Uganda na Kenya.

Mtandao huo wa siri huwalaghai wasichana wa Uganda wasio na ajira kwa ahadi ya malipo manono Mashariki ya Kati, mchakato wa hati za kusafiria, usafiri kutoka mipaka ya mashariki mwa Uganda hadi wanakokusudia.

Uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara hao haramu hutumia waendesha wa bodaboda na mawakala wa usafiri kuwasaidia wasichana kuvuka mpaka kuingia Kenya kupitia maeneo halisi ya mipakani kama vile Busia na Malaba.

Wakati mwingine hutumia mwanya wa uwapo wa njia nyingi za panya zisizo na ulinzi wa kutosha kutoroka. Ni biashara nono kwa wahusika.

Uchunguzi wa gazeti hilo pia umebaini kuwa mtandao huo unakamilika kwa kuhusisha maofisa wateule katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), ambao huhakikisha wanaruka kutoka Kenya kwenda maeneo husika salama salmin.

Uchunguzi huo umetokana na taarifa zilizotolewa na wasichana waliokamatwa nchini Kenya wakati wakijaribu kupanda ndege kwenda mataifa yaliyokusudiwa Mashariki ya Kati.

Wengine waliosaidia taarifa hiyo ni wakuu wawili wa wilaya wa Uganda, wazazi wa wasichana, mawakala na afisa mmoja wa uhamiaji wa Kenya na waandaa nyaraka za safari.

Baadhi ya wasichana waliishia Afrika Kusini, mataifa ya Mashariki ya Kati kama vile Oman, ambako ndiyo maarufu zaidi katika kesi hizo.

Mamlaka zinaamini baadhi ya wasichana na wanawake wadogo huuzwa na kuingia katika utumwa wa ngono huko waendako.

Kuonesha kuwa biashara hii inalipa vyema, mwendesha bodaboda hujipatia kati ya Sh100,000 za Uganda sawa na Sh 60,200 za Tanzania na  Sh200,000 za Uganda sawa na Sh 120,000 za Tanzania kwa kumvusha salama msichana kuingia mpaka wa Kenya.

Kwa kawaida safari hiyo, iwapo ingefanyika kihalali ilipaswa kugharimu si zaidi ya Sh 3,000 za Tanzania.

Haikuweza kufahamika kiasi, ambacho wakala hutengeneza iwapo atafanikiwa kumfikisha msichana wa Uganda kufanya kazi Oman.

Lakini kabla ya hapo waajiri walikuwa wakiwalipa mawakala huku baadhi ya wasichana wa Uganda wakitakiwa kuwapa mawakala hao kati ya Sh 800,000 sawa na Sh 485,000 za Tanzania na Sh milioni 1.5 za Uganda sawa na Sh 900,000 za Tanzania.

Fedha hizo huwezesha wasichana kuvuka mipaka, kugharimia malazi, stempu bandia na kuhonga maofisa pale JKIA.

Katika baadhi ya kesi, wasichana waliokuwa wakitenda kufanya kazi za ndani hawakuhitaji kulipa fedha zozote.

Mtandao unaosafirisha wasichana kupitia Kenya umekuwapo kwa miaka mingi, lakini umeonekana kuimarisha zaidi mbinu baada ya Kenya kupiga marufuku upelekeji wafanyakazi wa ndani Mashariki ya Kati.

Hali hiyo imezifanya Uganda na nchi jirani kama vile Burundi na DR Congo kuwa vyanzo vikuu vya kupata wasichana hao.

Uwanja wa JKIA ni maarufu zaidi kuliko ule wa Entebbe nchini Uganda katika shughuli hizo.

Walanguzi hawa hukumbana na upinzani mdogo hasa wanapokutana na maofisa wengine wanaowahesabu kuwa wanoko au kushindwa kuhonga uwanjani hapo kulinganisha na Entebbe, ambako si rahisi kufanikiwa.

Wafanyabiashara hawa wana mawakala wao mjini Kampala, ambao husaidia wasichana na wanawake kupata hati za kusafiria kwa muda mfupi.

Wasichana na wanawake wanaosafirishwa huanzia miaka 16 na 35 huku wa kundi la umri wa miaka 16 hadi 25 likiwa na soko zaidi.

Mmoja wa wasichana, ambaye hakuwa tayari kutajwa kwa sababu bado yu mikononi mwa mmoja wa mawakala, anasema alisafirishwa kutoka Kampala kupitia Mbale hadi Lwakaka ambako alivushwa kuingia Kenya.

“Ilitupasa kuvuka mto kwa mguu. Iwapo nisingesaidiwa kushikiliwa ningesombwa na maji. Niliingiwa na woga na maji yalikuwa baridi mno,” anasema.

Kivuko kingine hatari ni Mto Malaba. Wakati kiwango cha maji kinapopungua, ndipo wasichana husafirishwa kwa miguu.

Baadhi ya walanguzi hawa wa binadamu hutumia boti ndogo na mitumbwi kuvusha wasichana mpakani.

Baada ya kuvuka mpaka kuingia Kenya, hati za kusafiria za wasichana hushikiliwa na wasichana kupandishwa katika mabasi kwenda Nairobi.

Mjini Nairobi, huwekwa katika makazi ya walanguzi hao wakati nyaraka zao zikifanyiwa kazi. Baadhi ya walanguzi hawa hulazimika kutengeneza stempu bandia katika hati za kusafiria ili kuwezesha safari za wasichana hawa.

Baadhi ya makazi, ambayo wasichana huwekwa kwa muda wakisubiri safari ni pamoja na vitongoji vya Nairobi vya Kasarani na Kayole.

Miongoni mwa majina maarufu yanayowezesha safari hizi ni Dosco katika mpaka wa Busia.

Walanguzi huwalinda wasichana kwa saa 24 hadi ndege zinazowachukua zinaporuka kulekea ughaibuni.

Wakati msichana anapowasili kunakohusika Mashariki ya Kati, mlanguzu husika hupokea malipo yake ya kwanza ya hundi.

Huendelea kupokea mirahaba kipindi chote cha uwapo wa msichana huyo huko ughaibuni kutegemeana na mpangilio wa makubaliano baina yao na familia mwenyeji, biashara au mtu binafsi.

Kuwaondoa hofu baadhi ya wasichana, walanguzi hurekodi mawasiliano na wale wasichana waliobahatisha kufanya vyema huko waliko Mashariki ya Kati.

Huonesha mawasiliano hayo, picha za wasichana hao waliopo ughaibuni na hata kupigia simu mbele ya wasichana wanaolaghaiwa.

Kwa kusikia ‘live’ mazungumzo ya wasichana wenzao waliko ughaibuni wakisimulia uzuri wa maisha, wasichana hawa masikini huingia mtegoni.

Walanguzi hawa pia huhakikisha wanajiweka kwa karibu na familia za wasichana hata baada ya kukamatwa na wakati mwingine huzikomba fedha zaidi.

Mama wa msichana mmoja, ambaye karibuni alikamatwa nchini Kenya, awali alikubali kuzungumza na wanahabari, lakini akabadili mawazo baada ya kuzungumza na wakala aliyemchukua bintiye.

“Nimebanwa na shughuli, sijui namna alivyosafiri kwenda Kenya. Hili ni suala dogo, nawaamini watu waliomchukua na nimezungumza na wasichana wengine wana furaha huko waliko,” aliwjibu waandishi wa habari mara baada ya kuzungumza na wakala aliyemsafirisha binti yake.

Wakati mwandishi alimpotaka mama huyo wakutane kwa mazungumzo, aliishiwa kudanganywa kuhusu anakoishi hadi akakata tamaa kufuatilia.

Mmoja wa wasichana waliosafirishwa kutoka Kampala lakini akakamatwa kabla ya kuwasili Oman, anasema kwamba mama yake alilipa dola 200 sawa na Sh 440,00 za Tanzania kwa mwanasheria tapeli.

Mwanasheria huyo alipaswa kumwakilisha katika mahakama ya JKIA, lakini hakujitokeza mara zote mbili ambazo msichana alionekana mahakamani peke yake.

Mwanamke mwingine anasema wakala wake alijaribu mara mbili kumsafirisha kwenda Oman kupitia JKIA na mara zote alikamatwa.

Mara ya kwanza afisa mmoja wa uhamiaji wa Kenya aliyemkamata alimtaka wakala kulipa Sh 50,000 za Kenya sawa na milioni moja za Tanzania kwa kila msichana atakayeruhusiwa.

Lakini wakala huyo hakuwa na fedha hizo hivyo aliishia kutoa Kshs1,000 sawa na Sh 20,000 za Tanzania kwa kila msichana ambaye hakukamatwa.

Katika jaribio la pili msichana hakuwa na bahati kwani alikamatwa na kuzuiliwa kabla ya kuachiwa. Hadi sasa msichana huyo yuko nchini Kenya akifanyiwa jaribio la tatu la kutoroka.

Wale wanaoishia kutiwa hatiani hulipishwa faini nene ya Ksh 200,000 sawa na Sh milioni nne za Tanzania vinginevyo kwenda jela katika gereza la wanawake lenye ulinzi mkali la Lang’ata. Kumna waganda 44 waliozuiliwa gerezani humo na kwingineko.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles