24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO DAWA ZA KULEVYA WAJA NA MBINU MPYA

*Wafanyabiashara wadakwa na dola, waathirika wasimulia


Mtzd DEBBY Friday.inddNa WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa dawa za kulevya nchini, wameibuka na mbinu mpya ya kuingiza dawa hizo.

Mbinu hiyo ni kuingiza vibashirifu (kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kifua) aina ya ephedrine,  ambavyo huvitumia kutengenezea dawa za kulevya aina ya cocaine na heroin.

Akizungumza na MTANZANIA mapema wiki hii, Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela, alisema wamebaini mbinu hiyo mpya na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamejipanga kila kona ya nchi kudhibiti dawa hizo.

Kamanda Msikhela alisema wafanyabiashara hao huzisafirisha kemikali hizo kutoka Bara la Asia.

“Kikosi cha kupambana na dawa za kulevya tunapambana na kila njia ili kuweza kuliokoa Taifa. Na katika hili tunawaomba Watanzania wote tushirikiane kwa kukataa matumizi ya dawa za kulevya.

“Vibashirifu aina ya ephedrine hutumika kutengeneza dawa za kifua, lakini hawa wafanyabiashara haramu wanabadilisha mfumo wake. Wanachofanya ni kuchanganya na kemikali nyingine na kutengeneza heroin na cocaine,” alisema Kamanda Msikhela.

Alisema wafanyabiashara hao hununua kemikali hizo bila kuwa na kibali cha Serikali na hudanganya kuwa zinatumika kutengeneza dawa za kifua.

Alisema kwa kipindi cha mwaka jana, kikosi chake kiliwakamata watuhumiwa sita wakiwa na vibashirifu hivyo kilo 22,009. Walikwishafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema wanaoingiza vibashirifu wanatakiwa kufuata taratibu za kisheria, ikiwamo kupata kibali kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

 

TAKWIMU DAWA KULEVYA

Kamanda Msikhela alisema takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa kilo 17.33 za dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na mwaka 2015 zilipokamatwa kilo 7,696.

Kuhusu heroin, alisema kilo 31.77 zilikamatwa mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2015 ambao zilikamatwa kilo 69,346.

 

WAATHIRIKA WA DAWA

Matumizi ya dawa za kulevya hivi sasa yameteka kundi kubwa la vijana, wakiwamo wasanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu.

Kutokana na matumizi ya dawa hizo, baadhi ya watumiaji ambao awali walikuwa na ukwasi wa mali, sasa wamejikuta wakiangukia katika umasikini wa kutupwa.

MTANZANIA ilifanya mazungumzo na baadhi ya watumiaji wa dawa hizo katika vituo vya ushauri nasaha kwa waathirika wa dawa hizo (Sober House).

Akizungumza namna alivyoanza kutumia dawa za kulevya, mmoja wa waathirika ambaye yupo katika Kituo cha Padref of Wisdom kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam, Fatma Hussein, alisema alikuwa mmoja wa wauzaji wa dawa hizo akishirikiana na kigogo mmoja anayeishi Oysterbay, Dar es Salaam.

“Mimi nilikuwa naletewa mzigo na pusha (mfanyabiashara), nami nauchukua naugawa kwa vijana wangu kama watatu hivi, ambao walikuwa wakiusambaza maeneo mbalimbali kama Tandale, Manzese, Magomeni na hata Tandika.

“Nimeendelea na biashara hiyo kwa muda wa miaka kama mitano na kufanikiwa na kuwa na maisha mazuri na niliweza kununua nyumba.

“Siku moja alikuja pusha akaniambia hivi unauzaje biashara bila kujua ubora wake, basi akaniambia nionje kidogo kwa kunusa.

“Sitoisahau siku ile, maana nilitapika sana. Lakini baadaye nikapitiwa na usingizi na kuona raha sana, basi nilikuwa nakunywa bia, lakini nikaona haina starehe nzuri kama unga, ndipo nikajikuta nauza nyumba na magari yangu, hata fedha sijui nilivyotumia,” alisema Fatma.

 

APONZWA NA SIGARA

Kwa upande wake Witness Paschal, alisema alianza kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya kupitia rafiki yake aliyekuwa mkoani Geita.

“Nilitoka hapa Dar es Salaam na kwenda kwa rafiki yangu Geita kutafuta kazi, nilifanikiwa nilipata, lakini siku moja ‘boy friend’ wa rafiki yangu alikuja pale nyumbani na kuniambia nijaribu kuvuta sigara.

“Baada ya kuvuta nilipata usingizi mzito, basi kila siku nikawa natamani sana kuivuta, ikaendelea hivyo, ufanyaji kazi wangu ukazorota na kujikuta nikiacha kazi kabisa.

“Kwa kuwa yule bwana wa rafiki yangu alikuwa Mhindi, kwa hiyo upataji wa unga kwake haukuwa tatizo, mwisho nikaanza kuiba na hata kuonekana kama mtu aliyechanganyiwa mbele ya jamii,” alisema Witness ambaye ni mmoja wa waathirika wa dawa za kulevya.

 

MWANAJESHI ATUMBUKIA

Ally Zongo ambaye alikuwa mwanajeshi, alitumia dawa za kulevya kwa miaka 10, lakini sasa ameacha na amekuwa akiwasaidia wenzake walioathirika katika kituo cha Padref of Wisdom.

 

‘TEJA’ WA ZAMANI ALIYEOKOA ‘MATEJA’ 300

Akizungumza katika kipindi cha Kidani kinachorushwa na Azam Tv, Mkurugenzi wa Kituo cha Padref of Wisdom, Nuru Salehe, alisema yeye ni mmoja wa waathirika wa dawa za kulevya ambaye alijikuta akiingia katika matumizi hayo kwa miaka 12 baada ya kuolewa na mume wake ambaye alikuwa akizitumia.

Alisema pamoja na wao kuanzisha vituo hivyo, lakini bado anapata shida na namna dawa za kulevya zinavyoingia licha ya vyombo vya dola kulinda mipaka ya nchi.

“Mimi niliathirika na dawa za kulevya na nilipelekwa hadi kwa waganga na wazazi wangu, wakihisi labda nimerogwa, lakini nilikwenda kuacha dawa Zanzibar Sober House na wakati wote nilikuwa na ndoto ya mimi siku moja kuwa na kituo kama hiki, na sasa zaidi ya watu 300 wameacha kupitia hapa.

“Nilianza na wanaume na sasa wapo hadi wanawake ambao tumekuwa tukitoa huduma ya uraghibishi kwao ili waweze kuachana na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Nuru.

Mkurugenzi huyo alisema pamoja na hali hiyo, ni lazima Serikali ije na majibu madhubuti kuhusu kuingia kwa dawa za kulevya nchini, licha ya kuimarishwa ulinzi hadi viwanja vya ndege na maeneo ya bandari.

Alisema licha ya watu wanaohusika na biashara hiyo kukamatwa kwenye baadhi ya maeneo, lakini kasi hiyo inatakiwa kuongezwa kwa kwenda sambamba na utoaji elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuhusu dawa za kulevya.

 

NANDO ASIMULIA

Kwa upande wake, aliyekuwa mshiriki wa shindano la Big Brother Africa, Ammy Nando, akizungumza katika moja ya kipindi kilichorushwa na Clouds Tv, mwishoni mwa mwaka jana, alisema kuwa yeye ni mvutaji wa bangi na sigara ingawa pia anatumia unga.

Alisema akiwa katika nchi za Marekani na Afrika Kusini alitumia sana unga.

“Mimi si mpenzi wa unga kivile, mimi nimesafiri sana na kuona madaraja ya unga A, B… mfano class A unapatikana Los Angeles na class B unapatikana Colombia, kwa hiyo zote ukishazi-test (ukijaribu), ukija huku Afrika unaziita mchanga tu na si unga.

“Nawashauri wasivute unga, mapafu yataishia ‘kunyeka’ au kuwa mateja. Uteja unatokana na kuvuta lakini si ‘kusnifu’ na ukisnifu huwezi kuwa teja. Kwangu mimi nilikuwa situmii sana, mimi ni mwanamichezo, sina muda wa kutoa 3,000/- yangu nikapate kete moja.

“Kinachochangia ni kuwa ‘bored’ sana, mtu kama Chid Benz alitakiwa kutafuta kitu kama michezo, maana ukiruhusu tu hiyo, akili yako itakuwa ndiyo vile tu,” alisema Nando.

 

VIJANA 400,000 WAATHIRIKA 

Inaelezwa kwamba vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa sasa wanafikia 200,000 hadi 400,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Arusha na Tanga.

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu, kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee vijana zaidi ya 30,000 wameathirika.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa asilimia 30 wanaotumia dawa hizo kwa kujidunga sindano, wako hatarini kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Pamoja na hali hiyo, 20,000 waliotharika na dawa za kulevya wamekuwa wakipatiwa matibabu nchini.

 

TAARIFA YA WAZIRI

Akitoa taarifa ya athari za dawa za kulevya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, alisema kuwa watu milioni 200 duniani wameathirika na utumiaji wa dawa za kulevya.

Alisema kwa Zanzibar watu 10,000 wameathirika na utumiaji wa dawa huku 3,200 wakitumia kwa njia ya kujidunga sindano.

 

UTAFITI WA UN

Utafiti za hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa (UN) unaonyesha kwamba kuna ongezeko kubwa na la kutisha katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin na kwa njia ya kujidunga katika nchi za Kenya, Libya, Mauritius, Shelisheli na Tanzania.

Ripoti mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na uhalifu (UNODC), imetamka bayana kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika Mashariki na Tanga ukitajwa kama mkoa hatari zaidi.

Jumla ya tani 64 za dawa za kulevya aina ya heroin zilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania kati ya mwaka 2010 na 2013.

 

WALIOFUNGWA CHINA, BRAZIL

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2006 hadi Juni 2015, Watanzania 178 ambao wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya wamekamatwa nchini China.

Kutokana na sheria za China, wakitiwa hatiani na mahakama watakuwa hatarini kupoteza maisha.

Sheria za China mtu anayekutwa na hatia ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya hunyongwa.

Na kwa upande wa nchi ya Brazil, waliofungwa ni 113.

Kwa upandewa Hong Kong kuna zaidi ya Watanzania 200 wenye kesi za dawa za kulevya. Kesi 130 zimeshatolewa hukumu na 70 zinaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles