30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KUTOELEWEKA SERA YA MADINI KIKWAZO KWA WACHIMBAJI

Na Amina Omari


TANZANIA ni miongoni mwa nchi yenye hazina kubwa ya madini yakiwemo madini adimu kama ya vito na metali, ambapo mchango wa sekta ya madini ni muhimu  katika ukuaji wa uchumi.

Sekta hiyo ni mojawapo ya fursa zinazosaidia kutengeneza  ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi na kwa kuwawezesha wananchi kupata kipato pamoja na Serikali kwa ujumla.

Hata hivyo, mikakati ya Serikali ni kuhakikisha rasilimali hiyo ya madini inalinufaisha Taifa na watu wake kwa kuweka mipango madhubuti ambayo itawezesha kufikia lengo hilo.

Moja ya hatua ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kuchukua ili kudhibiti ulanguzi wake ni pamoja na kutoruhusu malighafi za madini hayo kusafirishwa nje ya nchi. Ikiwemo kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini na kufuatilia maduhuli yatokanayo na madini ili kuongeza mapato ya Serikali.

Wakati Serikali ikiweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wa madini kunufaika na rasilimali hiyo, nao wadau mbalimbali wameanza kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.

Hivi karibuni Taasisi ya Best Dialogs ya nchini Marekani waliendesha utafiti kuhusu changamoto zilizoko kwenye sekta ya madini nchini ili kushirikiana na Serikali.

Hivyo utafiti huo ulilenga kuleta majibu ya changamoto zilizoko katika  sekta hiyo hasa wanawake ambao katika shughuli za umiliki wa migodini na uchimbaji  ni wachache.

Baadhi ya mambo yaliyobainika katika utafiti huo ni kutoeleweka kwa sera ya madini kwa wachimbaji wenyewe na baadhi ya watendaji wa Serikali, mitaji midogo, ushiriki mdogo wa wanawake katika shughuli za uchimbaji na umiliki wa migodi.

Pamoja na upandaji wa tozo ya leseni ya mara kwa mara ambayo imesababisha kupungua kwa maombi ya leseni, kwa mtazamo wangu upunguaji huu wa maombi inaonyesha tayari kuna wachimbaji ambao wameendesha shughuli zao isivyo rasmi.

Hali ambayo inaweza kuleta madhara zaidi kwani mara nyingi shughuli za uchimbaji kwa baadhi ya maeneo zimekuwa zikifanyika katika maeneo ambayo si rasmi, hivyo huchangia uharibifu wa mazingira.

Hivyo, kutokana na matokeo ya utafiti huo, ipo haja kwa Serikali kuitafsiri sera ya madini kwa lugha nyepesi ili iweze kueleweka kwa urahisi na wadau wote wa sekta hiyo bila ya kubagua kiwango chao cha elimu.

Kwani sera ndio kama dira na mwongozo wa utekelezaji wa jambo lolote kwa ufanisi, hivyo kama haitaweza kueleweka na wadau wenyewe itachangia kuleta matatizo katika utekelezaji wa jambo husika.

 

Hivyo, kwa mtazamo wangu naamini sera hiyo itakapoeleweka kwa ufasaha na wachimbaji hususani wadogo, basi itasaidia kupunguza migogoro ambayo imekithiri kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi baina ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wenye kumiliki migodo mikubwa.

Pengine kuwepo au kukithiri kwa  migogoro katika maeneo yenye madini inatokana na wachimbaji kutoelewa taratibu za umiliki wa maeneo au watendaji wameshindwa kutoa elimu sahihi kwa walengwa.

Hivyo, ni muhimu ili kumaliza changamoto ya migogoro katika maeneo ya madini, wadau wakiwemo wasimamizi wa sekta hiyo wakafanya jitihada za makusudi kuhakikisha sera inawafikia wachimbaji na kuielewa.

Vilevile ipo haja sera hizo zikawafikia watendaji ngazi za chini ambako ndiko yaliko maeneo wanakoendeshea shughuli za uchimbaji.

Kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro lakini wanaoendesha shughuli za uchimbaji wataweza kujua taratibu za uchimbaji na kuzifuata bila ya kushurutishwa na mtu au Serikali.

Kwa mtazamo wangu, ipo haja kwa Serikali kuona namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo mitaji  ili kuondokana na uchimbaji duni kama ilivyo sasa.

Na hali hiyo itapunguza uchimbaji wa kutumia dhana duni ambao unachangia kushusha thamani ya madini wanayoyachimba, hivyo kuishia kupata faida kiduchu na Seriklai kukosa mapato yake yanayostahiki.

Vilevile kuainisha maeneo rasmi ambayo yanafaa kwa shughuli za uchimbaji wa madini, badala ya sasa ambapo shughuli hizo hufanyika hadi katika vyanzo vya maji ambapo hupelekea madhara zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles