27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kutana na Toby Waller, mvulana anayeishi bila kula vyakula

JOSEPH HIZA NA MITANDAO

NI miaka mitatu sasa, Toby Waller hana ufahamu kabisa na ladha ya chakula chochote kile ilivyo, hali inayomfanya asiweze kula kwa njia ya kawaida.

Tangu azaliwe hajawahi walau kutafuna biskuti, keki au kipande cha chokolate wala kula chakula kingine chochote kile, yote hayo yakisababishwa na mzio wa vyakula vyote.

Hali hiyo hufanya koo la Toby, kuhisi mwako mkali wa moto na huvimba umio kila anapomeza aina yoyote ya chakula.

Mama yake Suzanne, 37, anasema: “kuna wakati nilimtengenezea keki kwa ajili ya sherehe yake ya kwanza ya kuzaliwa – watoto wote waliililia wakati nilipoileta mezani isipokuwa Toby.

“Baadaye wakati watoto wengine wakila sandwichi na vipande vya chokoleti, Toby alibakia kuvikodolea macho tu.

“Pamoja na kuwa alikuwa na umri huo mdogo, alijua fika ataugua iwapo atakula chakula chochote kilichokuwa kwenye sherehe yake hiyo.”

Muda mfupi kabla ya sherehe yake ya kuzaliwa Toby aligundulika kuwa na tatizo lijulikanalo kwa kitaalamu ‘eosinophilic oesophagitis’ (EO).

Ni hali ya nadra inayoathiri mtoto mmoja kwa kila watoto 2,500 na hutokea wakati mfumo wa kinga mwilini unaposhambulia kimakosa vitu vigeni au vimelea vinavyoingia mwilini – kitu ambacho mfumo huo hudhani ni vitu visivyotakiwa.

Hali hiyo, husababisha mfumo wa juu wa mmeng’enyo wa chakula kuvimbiwa na kusababisha mtapiko, tindikali kurudi umioni, kizunguzungu na chakula kugeuka karaha.

Toby pia ana mzio kwa maziwa, mtama, soya, vumbi na kundi kubwa la vitu – vitu ambavyo ‘eosinophils’ yake, aina ya chembe chembe nyeupe ya damu, hudhani vimekuja kuushambulia mwili wake.

Chembe chembe hizo kwa kawaida hupatikana katika mfumo wa damu lakini kwa Toby hali ni tofauti kwani zipo tumboni pia.

Awali Suzanne alidhani tatizo litakaloisha lijulikanalo kwa kitaalamu kama ‘reflux’, ambalo binti yake Lily alikumbana nalo alipokuwa mdogo.

Hali hiyo husababisha vyakula kutoyeyushwa vyema au maji maji kugeuka mcheuo na kurudia katika umio. Na kwamba kama ilivyokuwa kwa Lily, Toby atakapozidi kukua ataondokana na tatizo hilo hasa atakapomwanzisha vyakula vigumu.

Lakini kwa mshangao wake, mambo yalizidi kuwa mabaya. “Akiwa na umri wa wiki 16, Toby akaanza ghafla kupiga mayowe. Angeweza kufanya hivyo huku akirusha rusha miguu na mikono kwa saa hadi mbili.

“Kila wakati nilipomlisha, angeanza tena kupiga mayowe makali. Na wakati nilipomkimbiza hospitali, nilikuwa nimechanganyikiwa sana.

Kilio chake kikubwa kilielezwa kuwa kilitokana na maumivu ya tumbo. “Wakati alipokuwa na umri wa miezi mitano nilijaribu kumzoesha vyakula vigumu lakini angepiga chafya kali na kuvitapika.”

Wataalamu wa afya katika Hospitali ya Watoto ya Sheffield nchini Uingereza walimpima kiwango cha tindikali katika tumbo la Toby kipindi cha saa 24, ambacho kilibainisha ana matatizo ya reflux.

Lakini madaktari walisema wanahisi kuna matatizo zaidi katika mwili wake mdogo.

Vipimo zaidi vilionyesha kwamba ana kiwango kikubwa cha chembe chembe za eosinophils katika umio lake na tumboni pamoja na katika eneo la mkondo wake wa damu ambamo ndimo zinamokaa.

Suzanne alitishika mno wakati alipoelezwa kwamba hali hiyo ilimfanya Toby akumbwe na hali ya mwako mkali kooni mwake na kumfanya kuwa mgonjwa au kuhara.

Anakumbushia: “Nilipata ahueni kiasi kuwa hatimaye tulibaini tatizo lakini kadiri ya miezi ilivyopita hadi kufikia siku yake ya kwanza ya kuzaliwa, hakuweza kutambaa wala kugeuka geuka na nilijua hali hiyo imetokana na kukosa nguvu.

Mei 2010, madaktari walimwekea bomba la kudumu tumboni, ambalo humlisha dozi ndogo ya maziwa maalumu kila baada ya saa nne nyakati za usiku.

Mchanganyiko huo maalumu wa maziwa huondoa vitu ambavyo husababisha mzio na una virutubisho.

Mlo wake wa kila siku kwa sasa ni mchanganyiko wa matunda kwa ajili ya kifungua kinywa, kwa chakula cha mchana hupata mlo wa watoto kama vile mtama au wenye protini na chai yake ni ya kawaida na dawa anazopata kwa siku ni 14.

“Pamoja na yote hayo, ni mzuri, mcheshi na mwenye furaha sana na ambaye kila mmoja anayekutana naye hawezi kujizuia kumsifia,”alisema.

Pamoja na kwamba hali ya Toby haina tiba, madaktari wana matumaini tatizo lake litazidi kupungua kwa kadiri ya anavyokua kiumri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles