LIVERPOOL, ENGLAND
MSHAMBULIAJI wa timu ya Liverpool, Sadio Mane, amedai kupigiwa kura ya uchezaji bora na nyota wa soka duniani Lionel Messi ni jambo la kujivunia katika maisha yake.
Mane alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliokuwa kwenye orodha ya kuwania uchezaji bora wa dunia wa FIFA mwaka huu huku Messi akitwaa tuzo hiyo dhidi ya wapinzani wake Cristiano Ronaldo na beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk.
Mane alikuwa miongoni mwa wachezaji tano waliokuwa wanawania tuzo hiyo na Messi alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliomchagua Mane kuwa kwenye orodha ya wachezaji bora, lakini hakuweza kuingia katika wachezaji watatu bora.
Kura ya Messi ilikwenda kwa Mane, Ronaldo pamoja na mchezaji mpya wa Barcelona ambaye anacheza nafasi ya kiungo, Frenkie de Jong, lakini Mane alikuwa namba moja kati ya wachezaji hao ambao aliwachagua Messi.
“Ni jambo kubwa sana kwangu kuona Messi ananipigia kura, ina maana kubwa kwangu nikiangalia wapi nilikotoka, bila ya kuwa kwenye Academy kwa kipindi kirefu lakini niweze kufika hapa.
“Kitu ambacho ninaweza kukisema kwa wachezaji chipukizi dawa ni kujituma tu, kwa kufanya hivyo unaweza kutimiza malengo,” alisema Mane.
Hata hivyo kwa upande wake Mane alimtaja Messi kuwa ni mchezaji bora duniani japokuwa kuna wengine kama vile Van Dijk.
“Kwa upande wangu Messi ni mchezaji bora, samahani rafiki yangu Van Dijk, ukweli ni kwamba nikiambiwa nichague nitaanza na Messi alafu Van Dijk atashika nafasi ya pili,” aliongeza mchezo huyo.
Mane mbali na kufanya vizuri msimu uliopita katika Ligi Kuu nchini England huku akiwa mmoja kati ya wafungaji bora baada ya kupachika jumla ya mabao 22 sawa na mchezaji mwenzake Mohammed Salah pamoja na mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, nyota huyo anaendelea kufanya vizuri msimu huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 tayari amefanikiwa kufunga mabao matano ya Ligi Kuu huku akifunga bao kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.