Newcastle wampa jeuri Frank Lampard

0
1107
Frank Lampard

LONDON, ENGLAND

BAADA ya timu ya Chelsea juzi kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle, kocha wa timu hiyo Frank Lampard ameanza kutamba kuwa na uwezo wa kuifunga timu yoyote watakayo kutana.

Mchezo huo wa juzi ulipigwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge, lakini Chelsea hawakupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na kile walichokifanya Newcastle katika mchezo wao dhidi ya Manchester United wiki mbili zilizopita.

United walishindwa kutamba mbele ya Newcastle na badala yake walikubali kichapo cha bao 1-0, jambo ambalo liliwapa matumaini wachezaji wa timu hiyo kujua wanaweza kushinda dhidi ya timu kubwa zilizipo mbele yao.

Katika mchezo huo wa juzi Chelsea walifanikiwa kupata bao katika dakika ya 73, lililowekwa wavuni na Marcos Alonso, lakini mchezo huo ulianza kubadilika baada ya kuingia kwa nyota wao Christian Pulisic.

“Kikubwa nimevutiwa na kiwango kizuri kilichooneshwa na Christian Pulisic, naweza kusema aliweza kuusoma vizuri mchezo huo wakati yupo nje, lakini wachezaji wengine wote walikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu.

“Kila mchezaji alikuwa kwenye kiwango chake hadi kuweza kufanikisha ushindi huo, kikubwa ilikuwa ni kuhitaji pointi tatu kwa kuwa hata wapinzani walikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu.

“Kutokana na ubora wao hakuna ambaye alikuwa anaamini tungeweza kushinda mchezo huo, lakini tulikuwa bora zaidi na ndio maana tumefanikiwa kushinda, hivyo kwa sasa tupo tayari kupambana na timu yoyote iliyopo mbele yetu,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo ushindi huo unaifanya Chelsea kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza jumla ya michao tisa. Kesho kutwa kocha huyo atakuwa na kibarua kizito kwenye mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Ajax, kabla ya kukutana na Burnley mwishoni mwa wiki hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here