NA FESTO POLEA, Zanzibar
“BABA yangu aliwahi kufanya filamu huku Afrika tena alikuwa akitusimulia kuhusiana na Zanzibar, maeneo mbalimbali ya Kenya na uzuri wa Zanzibar kwa jumla wakati alipofanya filamu yake ya ‘My Love’,” Kunal Kapoor anaanza kusimulia namna Zanzibar na Afrika ilivyo katika maisha yake.
Huyu ni prodyuza mashuhuri nchini India, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Tamasha la 19 la Kimataifa la Filamu kwa Nchi za Jahazi, Zanzibar.
Licha ya kusifia uzuri na namna baba yake alivyotengeneza filamu yake visiwani hapa, ameonesha nia ya kufikiria kucheza na waigizaji wa filamu wa Tanzania pindi atakapopata nafasi ya kufanya hivyo.
‘‘Nafikiria kucheza na waigizaji wa Tanzania ingawa siwajui lakini sijui lini labda nikipata muda wa kufanya hivyo, hilo jambo ni zuri kwangu na kwao kibiashara,’’ anaeleza.
Kapoor anasema Tanzania imebarikiwa mandhari nzuri, upendo na utulivu pamoja na lugha nzuri ya Kiswahili yenye mvuto – vitu vinavyoweza kuchangia waigizaji wa nchi nyingine kuja kufanyia filamu zao hapa lakini kikubwa ni kwamba serikali lazima ione umuhimu wa kuendeleza sekta ya filamu.
“Kuna mambo mengi yanatakiwa kuangaliwa na kuboreshwa lakini kwanza serikali iwekeze ipasavyo ili kujenga mazingira rahisi ya miundombinu thabiti ya kuwezesha kufika bila changamoto kubwa katika mandhari zitakazotaliwa.
Anasema kinachotakiwa kufanyika ni kupunguza gharama za usafiri, kodi kama zifanyavyo Afrika Kusini na Kenya katika masuala ya filamu jambo ambalo linalowavutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
“Naweza kuja kutumia mandhari ya hapa ama kuigiza na wasanii wa hapa na kushawishi wengine wa India kuja Zanzibar, kama hayo yatafanyika nina hakika hata mataifa mengine jirani zetu ikiwemo Sirilanka, Bangladesh, Pakistan, Asia yatatumia fursa hiyo kuongeza pato la taifa kupitia filamu.
Kapoor anasema Afrika Kusini na Kenya wanatoa punguzo la kodi ili kuhamasisha thamani ya kibiashara kwa watengeneza filamu na Tanzania ikifanya hivyo itakuwa imepiga hatua kubwa ya ushawishi kwa maprodyuza, waigizaji na wadau wa masuala ya filamu kuja kufanya kazi Tanzania.
Anaongeza kwamba kwa India kwa sasa kufanya filamu ni gharama kubwa kuliko maeneo mengine hivyo huwa bora kwake kwenda kufanya filamu nchi nyingine kwenye gharama nafuu anayoweza kupata atakacho hata akiwa na idadi kubwa ya vifaa vyake vya kazi.
OFISI YA TANZANIA, INDIA
Mwakilishi wa masuala ya filamu Zanzibar nchini India, Jilesh Babla anasema kutokana na sababu mbalimbali za kukuza utalii wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla ndiyo maana ofisi hiyo imeanzishwa nchini India.
“Tumeanzisha ofisi hiyo nchini India kwa kuwa ni njia muhimu ya kufikia mafanikio ya kitalii kupitia filamu zetu, pia tunatumia ofisi hiyo kuhamasisha matamasha mbalimbali ya filamu, kujumuisha waigizaji na kubadilishana mambo mbalimbali yahusuyo filamu,’’ anasema Jilesh.
MAISHA YA FILAMU
Kunal Kapoor amecheza filamu nyingi ikiwemo ya ‘Siddhartha’ iliyorekodiwa mwaka 1972 iliyotumia Kiingereza, mwaka 1978 alicheza filamu ya Junoon, ‘Ahista Ahista’ (1981) na ‘Vijeta’ (1982).
Filamu nyingine alizocheza ni pamoja na filamu ya sanaa ya ‘Utsav’ na mwaka 1984 pia amecheza filamu ya ‘Trikal’ kisha akapumzika kwa miaka 30 bila kuigiza filamu.
Akiwa amepumzika kucheza filamu mbalimbali mwaka 1987, alianzisha kampuni yake ya Adfilm-Valas akawa mtayarishaji na mwongozaji wa filamu pamoja na matangazo ya biashara.
Kupitia kampuni yake hiyo amefanya vizuri katika uandaaji wa filamu ya ‘City of Joy’ na filamu ya Kifaransa ya ‘Le Cactus’ iliyotoka mwaka 2005 kisha ‘Fire in Paradise’.
Alipumzika kuigiza kwa miaka 30 hadi alipoibuka tena mwaka 2015 na filamu ya ‘Singh is Bling’ akicheza kama baba wa Amy Jackson.