23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Malaika; Kama huna mkwanja, kaa pembeni!

Malaika
Malaika

 

SWAGGAZ RIPOTA,

MARA chache mno msanii mkubwa kuweka imani kwa msanii mchanga na kuamua kumpa mamlaka kamili kwenye ngoma yake anayoitegemea.

Licha ya unadra huo, Bongo tumebahatika kuwa na msanii wa namna hiyo ambapo alifanikiwa kuwa staa muda mfupi tu mara baada ya kushirikishwa kwenye Uswazi Take Away, ngoma ya msanii Chege. Huyu ndiyo Malaika Exavery au Malaika.

Kama ilivyo kawaida ya jarida hili kukuletea mastaa mbalimbali wa Bongo leo tupo na mrembo huyu, mkali wa ngoma kama Mwamtumu, Sare Sare, Zogo na Ralua inayofanya poa hivi sasa.

MALAIKA NI NANI

Anasema yeye alizaliwa huko Bukoba kwenye kijiji kinachoitwa Ibwela na baadae akahamia Arusha na kukulia huko. Alisoma shule ya msingi hapa Dar es salaam lakini elimu ya Sekondari alikwenda kuimalizia tena Arusha.

“Wakati nipo shule tayari mambo ya urembo yalinitawala hivyo nikashindwa kufanya vizuri mtihani wangu wa mwisho kitu ambacho familia yangu pia ilikishangaa mno.

Nilirudi Dar kuanza kutafuta mkwanja na kwenye harakati zangu nikakutana na Adam Juma ndiyo nikapata dili la kuwa ‘Make up Artist’ wake, ”.

Nilisoma kozi fupi na nikawa keshia pale RITA, ambako sikukaa sana nikaajiriwa kwenyetaasisi zingine kisha nikasafiri kwenda China na baadae India, wakati huo Uswazi Take Away niliyofanya na Chege ilikuwa inafanya poa na ni kama nilikuwa nimepishana na bahati sababu wengi walitaka kunifahamu ila mimi sikuwapo nchini,” anasema.

MAAJABU YA MWAMTUMU

BAADA ya kurejeanchini akitokea India, Malaika alirekodi ngoma yake ya Mwamtumu. Wimbo huu ulimshangaza kwani licha ya kumuingiza kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za KTMA, tena kwenye kipengele kigumu cha Msanii Bora wa Kike, Mwamtumu ilipendwa zaidi Ulaya na Marekani kuliko hapa Bongo.

“Nilipotoa Mwamtumu kwa hapa nyumbani haukufanya vizuri ila huko Texas, Marekani na nchi zingine za Ulaya ulifanya vizuri sana kwa hapa Bongo haukufanya vizuri ila nilipotoka Sare sare ndiyo watanzania waliuelewa,” anasema Malaika.

SHOO KIBAO ANAFUNIKA ILA HII ALIZINGUA

Malaika anasema kabla hajafanya shoo huwa anatetemeka kwa uoga ila akishapanda jukwaani hofu inapotea na anapiga shoo yenye ubora mkubwa na akishuka tena jukwaani huanza tena kutetemeka.

Licha ya kufanya shoo kali na classic kuna siku alizingua siku hiyo alitambua kuwa aliharibu.

“Kuna shoo niliifanya Zanzibar, nakumbuka nilikuwa nimetoka safari nje ya nchi, ile nimetua tu na ndege nikaenda Arusha harafu nikapitiliza mpaka Zanzibar. Nilichoka sana pia watu ambao huwa wananiandaa kabla ya shoo walikuwa hawajaweka sana baadhi ya vitu hiyo ikafanya nitumbuize chini ya kiwango.

SIRI YA KULAMBA MASHAVU SERIKALINI, BALOZI

UNAWEZA ukashangaa kwanini idadi ya wasanii wanaoonekana kwenye hafla za serikali na zile za balozi za nchi mbalimbali ni ndogo.

Heshima pamoja na nidhamu ni kigezo moja wapo kinachompa msanii shoo za kiserikali na zile zinazoandaliwa na balozi ambazo mkwanja wake ni mrefu tofauti na zile za kwenye klabu.

“Kama msanii umezoea kuvaa vichupi huwezi kupata dili za matangazo kwenye Serikali, balozi na taasisi za heshima ila huko kwenye kampuni zinazotengeneza nguo za ndani utapata,

Siri kubwa ya mimi kutumbuiza kwenye shunguli za kiserikali na kwenye balozi za nchi kama Uingereza, Ujerumani, Burundi, Norway na nyingine ni profile yangu nzuri kwa jamii,” anasema Malaika”.

UGENI WA JPM NYUMBANI KWAKE

February 18 mwaka huu, Malaika anasema hawezi kuisahau siku hiyo kwa kuwa alitambua kuwa muziki wake una thamani kubwa duniani mara baada ya Rais John Pombe Magufuli (JPM), kumtaja kama msanii anayemkubali alipowaalika wasanii pale Ikulu ya Magogoni.

“Nilifurahi mno kutajwa na Rais ila nilisikitika kwa kuwa sikuhudhuria. Nilikuwa kwenye Tv naangalia. Siyo hivyo tu aliwatuma watu wake waje nyumbani kwetu kuchukua CD za nyimbo zangu.

Imagine unaona magari ya Ikulu yamekuja kwenu kutaka kazi yako ambayo Rais ameagiza ipelekwe kwake. Kwangu mimi ni kitu kikubwa hata leo akitokea mtu akisema sijui kuimba nitamdharau mno,” alisema Malaika.

TUKIO LILILO MUUZIZA

MOJA ya kitu ambacho hawezi kukisahau na kilimuumiza ni pale alipoambiwa yeye siyo mtanzania na maafisa wa usalama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere.

“Majina yangu naona yaliwazuzua na wakadhani mimi siyo mtanzania. Nilizuiliwa kusafiri mpaka nilete udhibitisho wa vyeti vyangu vya kuzaliwa ili wathibitishe kama mimi ni raia wa Bongo. Niliwaletea ila hata waliponiruhusu kuondoka nilikuwa nimechelewa michongo niliyotaka kwenda kuifanya”.

ACHOMESHWA MAHINDI AIRPORT CHINA

Malaika, anasema kuna siku aliwahi kukaa masaa 16 kwenye uwanja wa ndege nchini China, mara baada ya kuhisiwa amebeba dawa za kulevya. Simu na mizigo yake ilichukuliwa ili ikakaguliwe na kwa muda huo mtu aliyetakiwa kumpokea, alikata tama na kuamua kuondoka kitu ambacho kilimpa msukosuko kwenye nchini hiyo ukizingatia yeye ni mgeni.

KAMA WEWE NI MASIKINI HUWEZI KUMNASA

Miezi miwili iliyopita alimuacha mpenzi wake na kuamua kuwa singo ili awekeze nguvu kwenye kutafuta mkwanja zaidi. Malaika anasema hajawahi kufikiria kutoka kimapenzi na mtu masikini labla masikini huyo awe na mipango ya kutengeneza fedha.

“Kwa sasa sipo tayari kuwa na mpenzi. Ila sifa za mwanaume ambaye anaweza kuwa na mimi ni yule mwenye uelewa wa mambo mengi awe muelewa wa mambo mengi na kingine huwa sidili kabisa na mwanaume masikini labla akitokea awe na mipango ambayo itaweza kutuingizia fedha,” alisema.

UTATA SKENDO YA KUWA FREEMASON

Amekuwa akihusishwa kuitumikia jamii ya siri ambayo inasemekana humuabudu shetani ‘Freemason’. Swaggaz lilitaka kufahamu kama ni kweli au laa na kama siyo kweli yeye huwa anasali au anaswali

“Hivyo vyote mimi sifanyi ila namuamini Mungu. Unajua huwenda kuna watu uliokuwa unakula nao chipsi za jero na ice cream za mia mia sasa wameona maisha yako yamebadilika tena ghafla ndiyo wanaanza kuongea maneno hayo ila itafika muda nitalizungumza kwa kina jambo hili kwa sasa sipo tayari,” anasema.

IMEANDIKWA NA JOHANES RESPICHES NA CHRISTOPHER MSEKENA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles