KATI ya nyota wa kigeni waliokuwa na wakati mgumu mara baada ya kusajiliwa katika kikosi cha Yanga ni Obrey Chirwa raia wa Zambia na mchezaji ghali katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) akitokea Platinum ya Zimbabwe.
Mkali huyo alisajiliwa kwa dola za Kimarekani 100,000 sawa na Sh milioni 200, mara baada ya kuridhishwa na ofa hiyo iliyokuwa imewekwa mezani na klabu ya Yanga.
Nyota huyo alikutana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga, waliokuwa wakitaka kuona uwezo wake wa kufunga na kuipaisha klabu hiyo katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Presha hiyo ilimfanya nyota huyo ashindwe kung’aa na kuitwa garasa, huku wengine wakiilaumu klabu kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumsajili mpachika mabao huyo wa zamani wa FC Platinum ya Zimbabwe.
Mabao nane katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara si haba, anaonyesha ni mshambuliaji wa daraja la juu, ila hakupewa muda wa kujifunza na kujipanga.
Tayari mshambuliaji huyo hatari amefungua akaunti yake ya mabao katika Kombe la FA ambapo mabingwa hao watetezi wametinga hatua ya robo fainali kwa kishindo, wanatarajia kushuka uwanjani kuwakabili maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.
Mabingwa hao watetezi wametinga katika hatua hiyo baada ya kuibugiza mabao 6-1 Kiluvya United ya mkoani Pwani inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Anachokifanya Chirwa hivi sasa ni kama kuwajibu mashabiki wa klabu ya Yanga kwa vitendo, kuonyesha uwezo wa hali ya juu na kuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji.
Awali klabu ya Yanga ilikuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji raia wa Burundi, Amissi Tambwe, ambaye alikuwa akimweka benchi Mzambia huyo aliyekuwa katika kipindi kigumu.
Chirwa ameanza kuandika rekodi yake ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kufunga mabao manne katika mashindano ya Kombe la FA, ambayo yalianza kufanyika mwaka jana ambapo Yanga walitwaa taji hilo.
Uwezo wa staa huyo umekuwa juu na kuwaziba midomo mashabiki wote wenye maswali waliokuwa wakimbeza kuwa ameishiwa na hana jipya.
Chirwa ni kama amezaliwa upya, amekuwa na mchango mkubwa hivi sasa na kuwa tegemeo kwa Mzambia, George Lwandamina, ambaye amekuwa akimpanga katika kikosi cha kwanza kutokana na mchango wake.
Nauliza hivi kuna mtu bado ana swali juu ya uwezo wa Chirwa ambaye ametoka kuwa adui wa mashabiki hadi kuwa kipenzi cha mashabiki wa mitaa ya Twiga na Jangwani.
Karibu Chirwa, karibu tena unapaswa kuwazoea mashabiki wa Tanzania ambao wapo kushangilia pekee hawajui kuwa kuna siku za kulia.