32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kumekucha Z’bar

hg3*CCM, CUF watangaziana jino kwa jino

*Mpigapicha wa Mtanzania atiwa msukosuko

* Mwandishi DW atoweka kitatanishi uwanja wa ndege

 

WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM NA ZANZIBAR

HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar imezidi kuwa tete baada ya vyama viwili vyenye wanachama na wafuasi wengi kutangaza kutovumiliana.

Vyama hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kwa nyakati tofauti wiki hii vimetangaza kujibu mapigo katika matukio ya aina yoyote yenye mwelekeo wa kusababisha vurugu dhidi ya wanachama au wafuasi wao ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa marudio.

Sambamba na hayo, vyombo vya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar jana vilimkamata mpiga picha wa Gazeti hili, Silivan Kiwale, wakati akitekeleza majukumu yake ya kikazi na kumwamuru kufuta picha zote alizokuwa amepiga katika eneo la bandari ya Zanzibar.

Aidha, mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani na pia mwakilishi wa Gazeti la Mwananchi visiwani Zanzibar, Salma Said, jana alikamatwa akiwa uwanja wa ndege.

Katika mlolongo wa matukio hayo, jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamisi, aliandika katika ukurasa wake wa facebook akieleza kuwa CCM imewachoka CUF na kuwataka vijana wa chama hicho kujibu mapigo yao.

Ujumbe huo ulijibiwa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi (JUVICUF), Hamidu Bobali, alipokuwa akisoma maazimio ya kikao cha jumuiya hiyo kilichoketi kwa siku mbili ofisi za makao makuu Buguruni aliyeeleza kuwa andishi la Sadifa katika ukurasa wake wa facebook linaonyesha ni maelekezo kutoka ngazi za juu hivyo vijana wa CUF wanapaswa kujiandaa na wasikubali kuonewa.

“Hii kauli ya Sadifa inamaanisha ni maelekezo kwa vijana wa CCM walipize kisasi kwa vijana wa CUF, sisi tunawaambia vijana watulie lakini wasikubali kupigwa maana ukikubali kupigwa hata kwa Mungu ni dhambi na hayo ndiyo maamuzi ya kikao,” alisema Bobali.

Alisema kauli hiyo ya Sadifa inaonyesha kuwa matukio yanayoendelea sasa Zanzibar ya kupigwa kwa wanachama wa CUF na kuchomwa moto kwa ofisi na makazi ya watu yanatekelezwa na wanachama wa CCM.

Mwenyekiti huyo aliyataja matukio hayo kuwa ni ulipuaji mabomu ambayo wananchi wa kawaida hawawezi kuyatekeleza hivyo yana dalili za kupangwa na vyombo vya usalama pamoja na CCM.

“Polisi wanahangaika kukamata viongozi wa CUF kila siku wakiwahusisha na matukio yanayoendelea Zanzibar wakati Sadifa katoa kauli ya kichochezi bado yupo mtaani,” alisema Bobali.

Bobali aliutumia pia mkutano huo kuzungumzia hali ya afya ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni ya kuridhisha tofauti na ambavyo imekuwa ikizungumziwa.

Alisisitiza kuwa msimamo wa CUF ni kutoshiriki uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika kesho na kuwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kupumzika nyumbani badala ya kwenda kupiga kura.

Wakati CCM na CUF vikitoa matamshi hayo yenye mwelekeo wa kulipiza visasi, maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama Zanzibar jana walimtia nguvuni mpigapicha wa gazeti hili, Silivan Kiwale muda mfupi baada ya kuwasili katika bandari ya visiwa hivyo kwa shughuli za kikazi.

Kiwale alitiwa nguvuni wakati akipiga picha katika eneo la bandari ya Zanzibar na kuamuriwa na wana usalama hao kufuta picha zote alizokuwa amepiga katika eneo hilo kisha akapewa tahadhari ya kuwa makini na nyendo zake wakati wote atakaokuwa visiwani humo.

Baada ya kufuta picha hizo na kuachiwa, Kiwale alijikuta akikamatwa kwa mara ya pili wakati akifuatilia kitambulisho maalumu cha kazi kinachotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambapo baada ya kuhojiwa aliachiwa.

Katika tukio jingine mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani na Mwakilishi wa Gazeti la Mwananchi visiwani Zanzibar, Salma Said, jana alikamatwa na maofisa usalama akiwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Salma alikamatwa saa 08:05 mchana  muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia tukio hilo, mume wa mwandishi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ali, alisema wakati ndege ndogo aliyokuwa akitarajiwa kusafiri nayo Salma aina ya Auric ikijiandaa kuruka, abiria walitangaziwa kwamba ndege hiyo itasubiri kwa muda kabla ya maofisa usalama kuingia na kumkamata.

“Ndege imecheleweshwa karibu nusu saa, abiria wakaelezwa ndege inasubiri kwanza na ndipo walipokuja polisi na kumchukua,” alisema Ali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis, alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa mwandishi huyo alisema hana taarifa hizo.

Salma amekamatwa ikiwa ni siku chache tu baada ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi, kutoa kauli kwamba polisi ina orodha ya watu 31 wakiwamo waandishi wa habari ambao itawaita kwa kuwahoji kuhusiana na matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani Zanzibar yakiwamo ya ulipuaji wa mabomu katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba

Tayari polisi wamekwishawahoji Mkuu wa Mikakati wa CUF, Eddy Riyami na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Nassor Mazrui, huku wakiendelea kumshikilia Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad Masoud.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles