25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wapiganaji wanawake, watoto 120 wanaswa msituni

IMG_8159*Walichukuliwa kufundishwa Quran

*Wakamatwa wakifundishwa mafunzo ya kivita

NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam limekamata kikosi cha watu 120 kilichokuwa kikipewa mafunzo ya kivita katika hifadhi ya misitu minene iliyoko Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

Taarifa iliyotolewa juzi kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, ilieleza kuwa kikosi hicho kinaundwa na watoto, wakiwamo wenye umri wa chini ya miaka kumi pamoja na wanawake.

Kamanda Sirro alisema kikosi cha wapiganaji hao 120 waliokuwa katika mafunzo ya kivita kilikamatwa na makachero wa polisi waliokuwa katika doria maalumu ya kusaka wahalifu kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Alisema doria hiyo imekuwa ikifanywa usiku na mchana katika misitu ya Kongowe na Rufiji na kwamba wapiganaji waliokamatwa wamebainika kupatiwa mafunzo ya kutumia silaha za kivita na kujihami kwa kutumia viungo vya mwili.

Mmoja wa wapiganaji hao aliyehojiwa na MTANZANIA  Jumamosi muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni, alieleza kuwa yeye si mkazi wa Dar es Salaam na alichukuliwa nyumbani kwa wazazi wake na mtu aliyemtaja kuwa ni mwanamume ambaye hamfahamu kwa ajili ya kuja kupatiwa mafunzo ya Quran.

Mpiganaji huyo ambaye ni mtoto mwenye umri wa miaka tisa (jina lake tunalihifadhi), alisema baada ya kufikishwa kwenye kambi iliyo kwenye misitu ya Mkuranga alianza kufundishwa Quran, kutumia silaha za kivita na kujihami kwa kutumia viungo vya mwili.

“Nina umri wa miaka tisa, sijawahi kupata elimu yoyote, lakini nilipofikishwa msituni nilianza kufundishwa mafunzo ya dini ya Kiislamu pamoja na kutumia silaha na mmoja wa walimu wangu alikuwa ananifundisha kupigana ngumi, karate na kutumia miguu kujihami na kushambulia.

“Kiongozi wetu wa kikundi alikuwa mbaba, alikuwa anatufundisha kupigana na kutumia silaha, lakini sasa hivi hayupo na hatujui alipokimbilia,” alisema mtoto huyo wa kiume.

Mtoto mwingine wa kike (naye jina lake tunalihifadhi) aliyehojiwa na gazeti hili, alisema ana umri wa miaka 11 na alichukuliwa nyumbani kwa wazazi wake Wilaya ya Kilwa, akieleza kuwa ameletwa mjini kwa ajili ya kujifunza Quran.

“Mimi nina miaka 11, nyumbani kwetu ni Kilwa na aliyetuleta huku sisi hatumjui, tumeletwa kujifunza Quran na hao wenzangu ambao nakaa nao mimi siwajui walipotokea, nimekuja nimewakuta na hapo  ninapokaa ni kwa mwalimu anayetufundisha,” alisema mtoto huyo.

Mbali ya watoto hao, wanawake waliokuwa katika kikosi hicho waliohojiwa na gazeti hili walieleza kuwa walijiunga na kambi hiyo wakiwa na waume zao ambao waliwakimbia baada ya kusikia kuwa kuna msako unaoendeshwa na Jeshi la Polisi unaowalenga.

Akizungumzia uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi kuhusu tukio hilo, Kamanda Sirro alisema imebainika kuwa wanawake waliokamatwa wakiwa katika kikosi hicho walifikishwa kwenye misitu hiyo na waume zao ambao ni miongoni mwa watuhumiwa wa uhalifu wa kutumia silaha wanaosakwa kwa udi na uvumba na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hao wanawake wamekimbiwa na waume zao miezi sita iliyopita na kwa upande wa hao watoto walikatishiwa masomo baada ya kudanganywa wanakuja kujifunza mafunzo ya dini (madrasa), lakini kumbe waliletwa kufundishwa namna ya kutumia silaha na mbinu za kivita.

“Hebu fikiria mtoto wa miaka 10 anaijua SMG (Shot Machine Gun) na anajua mbinu za kivita, tunaomba wananchi pamoja na viongozi wa serikali wanaozunguka kwenye haya maeneo watusaidie kutupa taarifa.

“Ninaamini tutafanikiwa, tutahamia kwenye hii misitu kuhakikisha tunakomesha uhalifu,” alisema Kamanda Sirro.

Aidha, Kamanda Sirro alisema katika tukio jingine polisi wa doria walio kwenye operesheni maalumu ya kusaka wahalifu wamewatia nguvuni majambazi wanane na mganga mmoja waliokuwa wakisakwa kwa kujihusisha na uhalifu.

Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Rajab Abasi, mkazi wa Keko ambaye gari lake lilikuwa la ujambazi, Obeid Awadh, mkazi wa Kiwalani, Ali Makoja, mkazi wa Ubungo, Marko Saule mkazi wa Gongo la Mboto ambaye aliwahi kufungwa gerezani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, Hassan Omary, mkazi wa Ubungo ambaye aliwahi kukamatwa kwa kuhusika na mauaji eneo la Kisarawe, Sadik Mohamed, mkazi wa Mbagala aliyewahi kufungwa kwa kosa la mauaji na Lei Saitoti, Mkazi wa Kimara aliyewahi kuhusika kwenye tukio la uporaji eneo la Mwenge.

Alisema pia polisi wamefanikiwa kumkamata jambazi sugu aliyetambuliwa kwa jina la Deodatus Costa (44), aliyewahi kufungwa kwa kosa la kuiba gari la serikali.

Kamanda Sirro alimtaja mganga aliyekamatwa kuwa ametambuliwa kwa jina la Ally Moigo (35), mkazi wa Kiwalani akiwa na gari aina ya Noah ambayo haijasajiliwa.

Alisema mganga huyo kazi yake ni kutibu majambazi na baada ya kupekuliwa alikutwa na dola bandia za Marekani 150.

“Pamoja na watuhumiwa hao, tumekamata bastola mbili aina ya browning zenye namba 053811-7.65 mm na 9766-6.35 mm maeneo ya Tegeta Nyuki, nyumbani kwa jambazi aliyejulikana kwa jina la Twaha Omary. Huyu aliuawa katika tukio la ujambazi maeneo ya Kinondoni.

“Tumekamata pia SMG mbili zilizokuwa zikitumiwa na majambazi waliouawa katika tukio la ujambazi  huko Pugu Mnadani na Machi 16 majira ya saa 19.45 tulimkamata jambazi sugu maeneo ya Kinyerezi mwisho akiwa na bastola moja na risasi nne,” alisema Kamanda Sirro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles