Na Tunu Nassoro, Dar es Salaam
Madiwani wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wamemchagua diwani wa kata ya Vingunguti Omary Kumbilamoto kuwa Meya wa Manispaa hiyo.
Pia wamemchagua diwani wa Ilala, Saad Kimji kuwa Naibu Meya. Kumbilamoto ameshinda nafasi hiyo kwa mara ya pili bila kupingwa baada ya madiwani wote 54 kutoka kata 36 kuwa ni wa Chama cha Mapinduzi ambapo Chama hicho kimewasilisha jina moja.
Akizungumza jana Desemba 10, baada ya kuchaguliwa, Meya Kumbilamoto amesema wengi wanashindwa kwa kupitia nyota ya Rais Dk. John Magufuli kwa kuwa wananchi wanaimani kubwa naye.
Amesema atahakikisha anawaunganisha madiwani wote kuwa kitu kimoja na kusimamia ahadi walizotoa kwa wananchi zinatimizwa.
“Kutokana na wengi wetu kuwa wageni tutaanza na kutoa semina elekezi kwa madiwani waweze kujua majukumu yao na kuisimamia kikamilifu manispaa,” amesema Kumbilamoto.
Amesema vipaumbele alivyojiwekea kuanza navyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba cha maiti katika hospitali ya Wilaya ya Ilala iliyopo Kivule, kukamilisha ujenzi wa soko la Kisutu na machinjio ya Vingunguti.
Kumbilamoto pia alimwomba Mkurugenzi wa Ilala Jumanne Shauri kusimamia kwa karibu ujenzi wa barabara ya kwa Mnyamani kwa kuwa mkandarasi tayari alipewa fedha, na pia ujenzi wa ofisi ya kata ya Zingiziwa.
Amewataka wakuu wa idara ndani ya Manispaa hiyo kuwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ofisi zao ili vipaumbele vyao viendane na vilivyomo ndani ya Ilani hiyo.