Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto anatarajiwa kuzindua upimaji afya bure utakaokwenda sambamba na uzinduzi wa zahanati ya Isimilla iliyopo wilayani Ilala.
Upimaji huo wa afya utafanyika Julai 15 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni katika zahanati hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisa Utawala wa Zahanati ya Isimilla, Lordriguez Peter, amesema kutakuwa na huduma za upimaji kisukari, wingi wa damu, presha pamoja na kutoa ushauri nasaha.
Amesema zahanati hiyo ni ya kisasa kwani ina madaktari bingwa wa mama na mtoto na wataalam wengine katika kada ya afya na kuwataka wananchi wa Wiĺaya ya Ilala na Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku hiyo kupata huduma bora.
“Zanahati yetu ya Isimilla ina madaktari wa kisasa wakiwemo wa watoto na wanawake, inatoa huhuma kwa magonjwa yote na pia tuna huduma ya bima ya afya ya NHIF,” amesema Peter.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya bure kwani itasaidia kugundua iwapo wana matatizo ya kiafya na kupata tiba mapema.