RAMADHAN HASSAN-DODOMA
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema bado kuna changamoto ya wanafunzi kupewa mimba, lakini familia zimekuwa zikiyamaliza kindugu.
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kilele cha Siku ya Idadi ya Watu Duniani ambapo pia ripoti ya hali ya idadi ya watu duniani imezinduliwa.
Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga, alisema ni wajibu wa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kumaliza tatizo la mimba za utotoni.
“Hapa tuna shida kidogo na hili tunatakiwa kulitolea elimu, mwanafunzi anapewa mimba na anayempa mimba anajulikana kabisa, lakini unakuta mambo haya wanayamaliza kama ndugu, hapa kunakuwa shida kwa sababu nani ataweza kutoa ushahidi mahakamani?
“Mimba ni nyingi, lakini zinaishia hewani tu, tupeleke uelewa katika mashule, wakati mwingine wanaowapa mimba ni ndugu kabisa,” alisema Waitara.
Katika hatua nyingine, Waitara alisema Serikali itaendelea kuwajali watu wenye ulemavu ambapo kwa sasa imetoa maelekezo majengo mapya yanayojengwa lazima kuwe na miundombinu kwa watu wenye ulemavu.
“Tumeagiza pia kuwe na chumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike kujihifadhi pindi wanapokuwa katika siku zao, lakini pia sasa hivi lazima kuwe na walimu wa kike ambao watakuwa wakiwaambia shida zao,” alisema Waitara.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, alisema ripoti ya hali ya idadi ya watu duniani imeonesha kwamba bado kuna changamoto katika suala la mimba za utotoni, ukosefu wa ajira, vifo vya wajawazito na ukatili wa kijinsia.
Katambi alisema ni lazima nguvu ziwekwe kutatua changamoto hizo huku akilitaka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) kusaidiana na Serikali kutatua matatizo hayo.