24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kujifunza kwa mtoto kunapaswa kuendane na umri wake

Watoto wakicheza
Watoto wakicheza

Na JOACHIM MABULA,

KUJIFUNZA kwa mtoto kunaanza pindi anapozaliwa. Kujifunza kuko kunatofautiana kulingana na umri na uwezo wa kuelewa, kufahamu na kupambana na kupambanua mazingira yanayomzunguka. Kujifunza kwake kunategemea pia ukomavu katika makuzi yake kimwili, kiakili, kijamii, kihisia na kimaadili. Ili mtoto aweze kujifunza mzazi au mlezi hana budi kuzingatia mambo anayoweza kutenda mtoto kulingana na umri na uwezo wake.

Ukiwa mzazi unayefuatilia ukuaji wa mtoto ni vyema kutambua hatua mbalimbali za kujifunza anazopitia mtoto katika umri tofauti tofauti tangu azaliwe. Ikiwa utagundua kuchelewa kwa kujifunza kwa mtoto kulingana na umri wake kutasaidia kuweza kumsaidia kwa kumpeleka kwa madaktari bingwa wa watoto na kupata msaada zaidi.

Hatua anazopitia mtoto anapojifunza katika umri tofauti:-

Miezi 0 – 6

Mtoto anatofautisha sura ya mama na watu wengine, anajizoesha kutumia viungo vyake, anajizoesha kujigeuza, kushika, kukaa, anaonyesha hisia tofauti, anatofautisha sauti, ladha ya vitu na harufu. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mwonyeshe tabasamu na kuongea naye, mpatie vitu vya kusaidia kufanya mazoezi ya kukaa bila kuanguka, mpatie vifaa vya kuchezea vyenye rangi na milio mbalimbali na weka mazingira katika hali ya usafi.

Miezi 7 – 12

Mtoto anainuka na kukaa, anatambaa, anajizoesha kusimama bila kuegemea, anajizoesha kutembea, anasema neno moja au mawili na anaiga matendo rahisi. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpatie mtoto vifaa vikubwa atakavyoweza kushika kwa urahisi, tenga muda wa kucheza na kuzungumza naye, tamka majina ya watu na vitu mbalimbali na mpe vifaa vya michezo.

Mwaka 1 – 2

Mtoto anapanga na kujenga vibao, anachora michoro mbalimbali na anaendelea kuiga matendo rahisi. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake tumia mbinu za miezi 7-12 pamoja na kumuuliza maswali rahisi na kumshirikisha katika shughuli ndogondogo.

Miaka 3 – 4

Mtoto anajifunza sehemu mbalimbali za mwili, anaosha mikono, anakula mwenyewe, anaimba, anataja namba na anashirikiana na wenzake. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake ongea naye, jibu maswali anayouliza kwa usahihi na busara, mpe vifaa vya kuhesabu na kulinganisha maumbo, msimulie hadithi, mfundishe michezo na nyimbo, mwimbie, mzoeshe kuvaa, kula chakula, kujisaidia chooni na kufunga vifungo au kamba za viatu.

Miaka 5 – 6

Mtoto anadadisi, anauliza maswali, anajifunza stadi mbalimbali kwa mfano kucheza mpira, kuchora, kuandika, kuhesabu na kusikiliza kwa makini. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake zungumza naye na kujibu maswali anayouliza na kumzoesha mtoto kupanga muda wa shughuli zake.

Miaka 7 – 8

Mtoto anakuwa mdadisi, anashiriki michezo mingi na anashiriki katika vikundi na makundi rika. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mzoeshe mtoto kupunguza muda wa michezo na kuweka mkazo katika masuala ya shule, mwelekeze na kumtia moyo wa kujifunza na kudadisi vitu mbalimbali anavyopendelea, msaidie mtoto kujifunza zaidi katika masomo yake na fuatilia maendeleo yake shuleni na katika vikundi.

Mambo yanayochochea mabadiliko katika tabia na utendaji wa mtoto wakati wa kujifunza:-

Umri

Umri wa mtoto unavyoongezeka ndivyo akili yake na viungo vingine vinavyokomaa. Hivyo, uwezo wa kupambana na mazingira yanayomzunguka unaongezeka.

Hali ya lishe kwa mtoto

Mtoto anayepata chakula chenye virutubisho vyote na cha kutosheleza mahitaji ya mwili anakuwa na hali nzuri ya lishe. Hali hii inamwezesha kukua kwa mtiririko unaolingana na umri wake, kumwezesha ukomavu wa viungo na kukuza uwezo wa utendaji wa mambo mbalimbali.

Hali ya afya ya mtoto

Hali njema ya afya humjengea mtoto uwezo wa kupambana vema na mazingira yanayomzunguka. Hali hii hujengeka kwa kumpatia mtoto mahitaji muhimu ikiwamo chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, chakula chenye virutubisho vyote na cha kutosheleza mahitaji ya mwili, uangalizi wa kutosha, tiba anapoumwa, kumpatia vifaa vya michezo na muda wa kutosha wa kucheza na kupumzika.

Mazingira safi na salama

Mazingira safi na salama yanajumuisha maeneo ya kuchezea yenye nafasi na vifaa vya michezo, familia na jamii yenye upendo, amani na utilivu, kuwapa watoto wa jinsi zote fursa sawa ya kucheza na kutenda mambo mbalimbali, uangalizi wa kutosha, wazazi, walezi na jamii kuwa na lugha adilifu, maeneo yenye usalama kwa mfano yaliyo mbali na barabara, yasiyokuwa na mashimo ya takataka, mashimo yasiyofunikwa, maji machafu na yaliyotuwama.

Mazingira ya aina hii yanaongeza uwezo wa mtoto kudadisi, kuvumbua, kulinganisha na kutatua vikwazo anavyokumbana navyo na yanamwepusha na ajali. Watoto wanaokua katika mazingira yasiyo rafiki wanakuwa hawajachangamka, wazito kudadisi, waoga na wasiojiamini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles