25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

KUFUTA ADHA YA MAJI KUTAWAEPUSHA WANANCHI NA KIPINDUPINDU

Na FERDNANDA MBAMILA


SERIKALI inaendelea kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwapatia huduma bora iwe za kiuchumi au kijamii kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Yote hayo yanafanikiwa kutokana uwapo wa taasisi imara za umma kama Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) ambalo wajibu wake ni kuhudumia wananchi kwa kutoa huduma bora huku likitambua umuhimu wa upatikanaji wa uhakika wa huduma ya maji.

Ili kufanikiwa katika azma ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda, huduma ya uhakika ya maji ni nyenzo muhimu kwani itasaidia uwapo wa uhakika wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile uzalishaji wa umeme, viwandani na kwa matumizi ya kawaida ya binadamu.

Kutokana na ukweli huo, Serikali ina malengo ya kuwapatia maji ya uhakika wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa jirani, Pwani, maeneo ambayo pia yana shughuli nyingi za kiuchumi kama vile viwanda na biashara nyingi na kubwa kubwa.

Ili kuwa na uzalishaji wa uhakika viwandani huduma ya maji ni muhimu sana, jambo ambalo linaifanya serikali ya awamu ya tano kuipa umuhimu wa kipekee sekta hiyo.

“Viwanda vingi, watu wengi wanahitaji uwepo wa huduma ya maji ya uhakika, hivyo juhudi za serikali ya awamu ya tano za kuhakikisha maji yanapatikana kwa muda wote zitasaidia kujenga uchumi wetu,” anasema Juma Ali, Mchumi na mkazi wa Gongo la Mboto.

Anasema wakazi wa jijini na maeneo mengine ya nchi yetu wanahitaji huduma ya uhakika ya maji ya bomba kwani huduma hiyo ni rahisi na pia salama kwa afya ya watumiaji.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Mhandisi Cyprian Luhemeja anasema amejipanga kikamilifu kuwatumikia wananchi lengo likiwa ni kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda na uchumi wa kati.

Anasema uamuzi huo unalenga kuwawezesha wananchi ambao tayari walipoteza matumaini ya kupata maji kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipia gharama ya kuunganishiwa.

“DAWASCO tumedhamilimia kuwajibika kikamilifu na kutimiza kauli mbiu ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ya “Mama Tua Ndoo ya Maji Kichwani.

“Tuko hapa kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania wote na kuhakikisha kwamba wanapata maji ya uhakika na salama kwa muda wote,” anasema Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja anatoa wito kwa wananchi ambao hawajaunganishiwa huduma hiyo kwenda katika ofisi za DAWASCO zilizoko karibu yao ili kupatiwa huduma hiyo.

“Natoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam na jirani zetu wajitokeze kwa wingi waweze kuunganishiwa huduma hiyo ili kila mtu afaidi matunda ya serikali yake bila kubughudhiwa,” anasema.

Anasema yeye na timu yake wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu ili kuhakisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati na uhakika.

Anasema kwa kuchapa kazi mabadiliko yametokea kwani upatikanaji wa huduma hiyo umekuwa ni wa uhakika.
“Dar es Salaam ilikuwa na uhaba wa maji, lakini baada serikali kubuni na kuanzisha miradi mikubwa ya maji, hali hiyo inaweza kuwa historia katika kipindi kijacho cha mwaka mmoja kuanzia sasa,” anasema.

Anafafanua kuwa maji si tatizo isipokuwa watumiaji ndio tatizo -si maji bali watu. “Naweza kusema kuna baadhi ya watu kushindwa wenyewe kuomba kuunganishiwa huduma hiyo,” anasema.
Anasema shirika lake limeimarisha kutoa huduma ya maji na kwamba kila siku lina uwezo wa kuzalisha lita milioni 483 jambo ambalo halikuwapo siku za nyuma.

Mhandisi Luhemeja anasema awali Dar es Salaam ilikuwa ikitegemea vyanzo vikuu vya maji kutoka mitambo ya Ruvu Juu ambao kwa siku unazalisha lita milioni 82, Ruvu Chini unazalisha lita milioni 270.

Mtoni unazalisha lita milioni 9 na visima virefu 106 ambavyo vinazalisha jumla ya lita milioni 106 kwa siku.
Anasema vyanzo vyote hivyo huzalisha wastani wa lita milioni 371 kwa siku ambazo zilikuwa zikitosheleza asilimia 75 ya mahitaji ya wananchi ambapo sasa imeongezeka hadi zaidi ya asilimia 80.

Kuhusu huduma ya maji taka, Luhemeja anasema imepiga hatua ya kuridhisha tofauti na awali kwani shirika lake limekuwa likikarabati miundombinu ya majitaka, hivyo kuweza kudhibiti kuvuja kwa baadhi ya mabomba.
“Hali hii tumeidhibiti na kuepusha milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na matumbo ya kuhara,” anasema Luhemeja.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa, maji yanayozalishwa bado hayatoshelezi wakazi wa mji huu lakini, Serikali inajitahidi kwa hali na mali, kuwasaidia wananchi wake kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama.
Katika kutekeleza kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” ya Rais Dk Magufuli aliagiza kuwa, ifikapo Juni mwaka huu wateja 400,000 wa Dar es Salaam wawe wamepatiwa huduma ya maji safi na salama.

Ili kutekeleza agizo hilo, DAWASCO imeamua kugharamia uunganishaji wa huduma hiyo kwa wakazi wake ambapo gharama hiyo ilikuwa ikilipwa na mteja mwenyewe.
Akielezea utaratibu huo wa kugharamia uunganishaji wa huduma ya maji kwa wateja, anasema utakuwapo kwa kipindi maalumu cha miezi miwili.

Anasema baada ya hapo mteja atawajibika kurudisha gharama za uunganishaji kidogo kidogo kila mwezi kwa muda wa miezi 12.
Fursa hiyo imesaidia hata kwa wananchi wenye kipato cha chini kuweza kuunganishiwa huduma ya maji na hivyo kuepuka kunywa maji yasiyo na viwango ambayo ndio chanzo cha magonjwa ya mlipuko kama kipindipindu.
Malipo ya kuunganishiwa maji hayana riba bali mteja anahitajika kulipia gharama za uvutaji wa bomba kama zilivyoainishwa na utaratibu wa malipo unaunganishwa na bili ya kawaida ya maji inayopelekwa kwa mteja kila mwezi.

Uondoaji wa kero ya maji umesaidia nguvu nyingine na muda uliokuwa unatumika kwa ajili ya kutafuta maji, kutumika kwa shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Sehemu nyingi za makazi ya watu katika jiji la Dar es Salaam, walikuwa wakipata huduma ya maji kwa kununua kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo kwenye visima, ambayo si salama kwa kunywa.
Pia maji ya visima katika baadhi ya maeneo yana chumvi kiasi cha kufanya nguo zifubae na unywaji maji au matumizi katika mapishi kuwa magumu.

Mbali na hilo, gharama ya kununua maji ilikuwa kubwa kuliko gharama ya chakula na wananchi wengi walikuwa wakitumia muda wao mwingi kuhangaika kutafuta maji jambo ambalo lilikuwa likikwamisha kutekeleza majukumu mengine ya kujenga nchi.

Katika kero hiyo ya uhaba wa maji, waathirika wakuu walikuwa kina mama. Hivyo basi, mkakati wa DAWASCO wa kusambaza huduma ya maji safi kwa wananchi utasaidia kupunguza kero hiyo kwa kiasi kikubwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles