Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WASOMAJI wa haki hainunuliwi katika safu yetu tanaendelea kukumbushana haki za watoto kama Sheria ya Haki za Mtoto ya mwaka 2009 inavyosema.
Katika sheria hiyo kuna majukumu ya mzazi, wajibu na jukumu la mzazi ni kwamba mtoto atakuwa na haki ya kuishi, kwa hadhi, heshima, uhuru, afya, kupumzika na kupatiwa elimu na malazi kutoka kwa wazazi.
Haki ya kupumzika na uhuru kwa mtoto vitategemea maelekezo na uwezo wa wazazi, walezi au ndugu.
Kila mzazi ana wajibu na majukumu kwa mtoto. Wajibu na majukumu hayo yatatekelezwa, yawe yamewekwa na sheria au vinginevyo.
Majukumu yanahusisha wajibu wa kumlinda mtoto dhidi ya kutelekezwa, kutengwa, kufanyiwa vurugu, kunyanyaswa, kutumiwa vibaya, na kuwa katika mazingira mabaya kimwili na kimaadili.
Kutoa maelekezo, uangalizi, msaada, na hifadhi kwa ajili ya mtoto na uhakika wa maisha na maendeleo ya mtoto, kuhakikisha kuwa wazazi wanapokuwa mbali na mtoto, mtoto atapata uangalizi kutoka kwa mtu mwenye uwezo wa kutimiza majukumu hayo.
Wajibu na majukumu haya yanasitishwa wakati wazazi wanapotoa wajibu na majukumu hayo kwa mtu mwingine.
Kutoa majukumu kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtu mwingine kunafanywa kulingana na sheria iliyoandikwa au kwa mpango wa mila na desturi.
Iwapo wazazi waliomzaa mtoto wamefariki, wajibu wa wazazi utahamia kwa ndugu wa mzazi wa kiume au wa kike au mlezi.
Watapewa wajibu na majukumu hayo kwa amri ya mahakama, au mpango wowote utakaowekwa kimila.
Mtu haruhusiwi kumnyima mtoto kumiliki na kutumia mali ya urithi kutoka kwa mzazi.
Sheria ya mtoto inaweka bayana kwamba mtoto atakuwa na haki ya kutoa maoni. Hakuna mtu anayeruhusiwa kumnyima mtoto mwenye uwezo wa kutoa maoni haki ya kueleza maoni, kusikilizwa na kushiriki katika kufanya maamuzi yatakayoathiri ustawi.
Mtu yeyote haruhusiwi kumuajiri mtoto katika shughuli yoyote inayoweza kuwa na madhara katika maendeleo ya afya, elimu, akili, mwili na maadili yake.
Kwa mfano, kazi katika viwanda vya kemikali inaleta athari kwa afya ya mtoto. Kazi ya mashambani au machimboni inayozuia mtoto kwenda shule inaathiri elimu, akili na mwili wake.
Kazi ya ukahaba inaathiri maadili ya mtoto, mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, au adhabu ya kikatili, ya kinyama au afanyiwe matendo yenye kumshushia hadhi.
Hii ni pamoja na desturi zozote za mila zenye kudhalilisha utu wa mtoto au zinazosababisha athari za maumivu ya mwili au akili ya mtoto.
Kwa mfano, kukeketa wasichana ni kudhuru vibaya mwili, akili na hisia za mtoto wa kike, pia ni kitendo kinachomdhalilisha.
Hakuna adhabu kwa mtoto inayokubalika ambayo imekithiri kimatendo au kwa kiwango kulingana na umri, hali ya mwili na akili yake.
Hakuna adhabu inayokubalika kwa ajili ya umri mdogo wa mtoto au vinginevyo kwa sababu mtoto hawezi kuelewa nia ya adhabu hiyo.
Tendo lenye kudhalilisha, kama maneno hayo yalivyotumika katika fungu hili una maana ya tendo lililofanywa kwa mtoto kwa nia ya kudhalilisha au kumshushia hadhi yake.
Kwa mfano, kuchapa mtoto mbele ya wenzake au mbele ya umma wa watu ni tendo lenye nia ya kumdhalilisha mtoto
Mtu anayevunja sheria kama ilivyoainishwa katika sehemu hii, anatenda kosa.
Mtendaji wa makosa hayo baada ya kutiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo, atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa muda usiozidi miezi sita au vyote kwa pamoja.