Na ANDREW MSECHU
WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea (Ubungo) na Antony Komu (Moshi Vijijini), wamekiri kushiriki katika mazungumzo yanayodaiwa yalikuwa ya kupanga hujuma dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Kutokana na kukiri kwao huko, kamati kuu ya chama hicho iliyokutana juzi ilitoa adhabu kwa wabunge hao ikiwa ni pamoja na kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12.
Adhabu nyingine waliyopewa ni kuvuliwa nafasi zote za uongozi walizokuwa nazo ndani ya chama, kuandika barua za kujieleza na kuomba radhi hadharani kwa watu wote waliowataja katika sauti hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya jamii.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Mkuu ya Chadema Dar es Salaam jana, Kubenea na Komu walikiri kuwa sauti hizo zilikuwa za kwao lakini mazungumzo hayo yalikuwa binafsi ambayo hayakupaswa kuingia katika mitandao ya jamii.
Komu alisema walikuwa kwenye mazungumzo ya faragha lakini teknolojia iliwashinda hadi ilipotokea ujumbe huo ukasambaa katika mitandao ya jamii suala ambalo hawakulitarajia.
Alisema katika kikao cha juzi cha Kamati Kuu, walitoa maelezo marefu ya kina kuhusu tukio hilo na kwamba katika hali ya kawaida hawakuwa wametarajia hilo kujitokeza.
“Kilichosababisha kuonekana kuwa tulitaka kuzuru au kuhujumu viongozi wa chama ni kwa sababu kipande hicho cha sauti kilitolewa kwa ufupi baada ya kujirekodi kwa bahati mbaya katika simu yangu na kuingia katika kundi moja la Whatsapp ,” alisema Komu.
Alisema hatua hiyo ndiyo inayoonekana kutoa nafasi ya watu kutafsiri kila mmoja kwa upeo wake.
“Tunaueleza umma kwamba suala hili halihusishi kwa namna yoyote agenda ya siri, yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida tu ambayo hayakuwa na nia au dhamira yoyote mbaya.
“Tulikuwa kwenye mjadala tukiwa ndani ya gari, ilikiwa ni mazungumzo yetu kutokana na taarifa tuliyokuwa tumeipata kwa jamaa mmoja tuliyekutana naye,” alisema.
Alisema kile kinachosikika kwenye mazungumzo hayo ni kipande kidogo tu katika sehemu ya mazungumzo yao na kwamba yangesikika mazungumzo yao yote, watu wangepata picha halisi.
Aliushukuru uongozi wa chama hicho kwa jinsi ulivyoshughulikia suala hilo na kulipa uzito na kwamba tayari yeye na Kubenea wameshawasilisha barua za kujieleza kama walivyoagizwa .
Kauli ya Kubenea
Naye Kubenea alisema anatumia nafasi hiyo kuomba radhi kama alivyoelekezwa na kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika kwa zaidi ya saa 14 juzi.
“Nichukue nafasi hii kusema kuwa nimeumizwa na mambo yaliyotokea katika kipande hiki ninaomba radhi kwa waliotajwa, wanachama na Watanzania,” alisema.
Alisema kimsingi hata tatizo na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na kwamba yeye kwa nafasi yake ya ubunge amekuwa akiingia katika vikao vya halmashauri kama diwani na amekuwa akitoa ushirikiano wa karibu kwa meya huyo
“Siku zote tumekuwa tukishirikiana na Meya Jackob na hatuna mgogoro naye. Tena napenda kuwaambia kwamba katika maisha ya kawaida kila mtu ana marafiki zake wa karibu na miongoni mwa marafiki zangu wa karibu ni Boniface Jacob,” alisema.
Akizungumzia suala la taarifa zinazoendelea kuwa yeye ni miongoni mwa wabunge wanaotarajia kuhamia CCM kutoka Chadema, alisema yeye si legelege na ni mtu imara ndiyo maana amethubutu hata kuitika wito wa Kamati Kuu ya Chadema tofauti na wengine ambao wanapopata wito wa aina hiyo huondoka moja kwa moja.
Alisema ana imani na uongozi wa Chadema kwa kuwa ni sehemu ambayo inaruhusu uhuru wa maoni, unaotambua kuwa katika jamii yoyote suala la kuwa na maoni tofauti siyo kosa na kuwa ni jambo linaloleta uhai.
“Ndiyo maana kwenye Kamati Kuu yetu iliyosheheni watu wakubwa kama mawaziri wakuu wawili wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, watu kama kina Profesa Mwesiga Baregu, akina Profesa Abdalla Safari mambo yalienda vizuri” alisema.
Melekezo ya Mnyika
Awali, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, alisema uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu ya chama kilichofanyika juzi umefikiwa baada ya kuwahoji kwa muda mrefu watuhumiwa ambao walipewa nafasi ya kujieleza na kusikilizwa na wajumbe wote.
Alisema kikao hicho cha Kamati Kuu kiliitishwa kwa dharura baada ya kipande hicho cha sauti kilichodaiwa kuwa kilikuwa cha majadiliano baina ya Kubenea na Komu kusambaa kuanzia Oktoba 13.
“Kufuatia kusambaa kwa ujumbe huo wenye maudhui ya kuashiria utovu wa nidhamu, Kamati Kuu ya chama iliitisha kikao hicho na Katibu aliwasilisha tuhuma za utovu wa nidhamu dhidi ya wahusika.
“Hii ni kwa mujibu wa kanuni kifungu cha 6.52 b, ambako wahusika waliitwa mbele ya kamati hiyo,” alisema.
Alisema wahusika wote walikiri kuwa sauti hizo ni za kwao na Kamati Kuu iliwakuta na hatia ya kukiuka kanuni na maadili ya chama hicho, hivyo ilifikia uamuzi wa kuwapa onyo kali na kuwaagiza waandike barua za maelezo.
Alisema Kamati Kuu pia iliwaagiza kuomba radhi kwa chama na wahusika waliotajwa na watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 na kuwavua nafasi zote za uongozi ndani ya chama na kubaki na nafasi ya uwakilishi wa wananchi, yaani ubunge.
Kabla ya hatua hiyo, Kubenea alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, nafasi ambayo aliwahi kuomba kujiuzulu lakini hakuwa amejibiwa hadi hatua hiyo ya juzi inachukuliwa na Komu alikuwa ni mjumbe wa kamati ya utendaji katika kanda ya Moshi.
Mnyika alisema katika kikao hicho kila kitu kilifanyika kwa ustaarabu na utaratibu mzuri kwa kuzingatia misingi ya haki za watu kujieleza na kusikilizwa, kwa kuhakikisha kuwa wahusika wanapewa haki yao kwa kiwango cha juu.
Mikakati ya kazi
Mnyika alisema kwa sasa chama hicho kinaelekeza nguvu zake za kujenga chama katika maeneo yote ya nchi na kwamba tayari Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Mashinji wamekwisha kuanza ziara mikoani.
Alisema kwa sasa viongozi wengine wanakamilisha taratibu za kawaida na wote watakwenda katika mikoa tofauti kwa ajili ya mikutano ya ndani ya ujenzi wa chama hasa baada ya mikutano ya hadhara kupigwa marufuku.
“Kwa kuwa tulishatangaza kuwa hatutashiriki uchaguzi wa marudio, nguvu yetu sasa tunaielekeza katika kujenga chama maeneo yote ya nchi.
“Kwa sasa viongozi wote watakwenda kujichimbia mikoani kwa ajili ya mikutano ya ndani, kwa ajili ya kujenga chama baada ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara,” alisema.