22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

KUBENEA AKABIDHI JENERETA ZAHANATI YA MAVURUNZA

MBUNGE wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema)
MBUNGE wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema)

Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema), ametoa msaada wa jenereta lenye thamani ya Sh milioni tano katika Zahanati ya Mavurunza iliyopo Kimara  ambapo wananchi walikuwa wakipata huduma kwa kutumia tochi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, baada ya kukabidhi jenereta hilo, Kubenea alisema ametoa msaada huo baada ya kupata taarifa kuwa zahanati hiyo bado haijaunganishwa na huduma ya umeme.

Alisema kitendo cha wauguzi kutumia tochi wakati wa kutoa huduma si kizuri kwa kuwa wanahatarisha maisha ya wagonjwa.

“Viongozi waliopita hawakuona  umuhimu wa kuokoa maisha ya watu na  zahanati hii inasaidia  karibia mitaa mitano katika kata hii, naamini jenereta hili litawasaidia katika kuendesha shughuli zenu za kila siku,” alisema Kubenea.

Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo, Doroth Mushi, alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo na kusema pamoja na kutatua changamoto ya umeme, bado wanakabiliwa na changamoto nyingine ya ubovu wa jengo la wazazi.

“Jengo la wazazi  kwa sasa halitumiki  kwa sababu limekuwa na mazingira hatarishi, sehemu ya ukuta ina ufa hivyo unahitaji kukarabatiwa, tuendelee kutoa huduma ya uzazi kama ilivyokuwa  zamani,” alisema Mushi.

Alisema zahanati hiyo pia haina maji ya  Dawasco na badala yake wanatumia maji ya chumvi ambayo si salama.

Aliongeza  na kusisitiza kuwa zahanati hiyo pia ina tatizo la dawa kwa kuwa dawa zinazotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) ni chache na pia zinafika kwa kuchelewa.

Baada ya malalamiko hayo, Kubenea aliahidi kuzichukua changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi na nyingine kuzifikisha kwa wahusika serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles