Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Martine Mbwana, ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Jukwaa la Biashara na Huduma litakuwa chachu muhimu kwa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo.
Mbwana alisema jukwaa hilo linalenga kuwaunganisha wafanyabiashara kwa njia mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa masoko, kuanzisha viwanda, na kuchochea uwekezaji wa ndani.
Akizungumza Oktoba 10, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo, Mbwana alisema kuwa ukosefu wa taarifa na ujuzi umekuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara.
“Biashara ni nguzo muhimu katika kuendesha uchumi wa taifa, na tutaweza kutumia jukwaa hili kutatua changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikikabili biashara zetu,” alisema.
Mbwana alieleza kwamba jukwaa hilo litawapa wafanyabiashara fursa za kupata taarifa kuhusu masoko ya ndani na ya kimataifa, pamoja na fursa za mitaji. Alisema serikali imekuwa ikichukua hatua kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kupunguza urasimu ambao umekuwa ukikwamisha sekta hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Jukwaa hilo, Freddy Leopard, aliwahimiza wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kutangaza bidhaa zinazotengenezwa nchini, akisema kuwa utangazaji huo utaongeza soko la ndani na nje.
“Lengo ni taasisi za serikali kushirikiana na wafanyabiashara kwa ukaribu, na pia kutoa mafunzo kwa wadau ili kufikia malengo ya kukuza uchumi wa nchi,” alieleza Leopard.
Mfanyabiashara wa mashuka na mapazia katika soko la Kariakoo, Ida Mwaibula, alionyesha matumaini makubwa juu ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo, akisema litatengeneza fursa mpya za ushirikiano na taasisi za serikali.
“Jukwaa hili litatuunganisha na wadau mbalimbali wa serikali, na tunatumaini kuwa biashara zetu zitakua kupitia jukwaa hili,” alisema Mwaibula.
Kwa kuanzisha Jukwaa la Biashara na Huduma, Kariakoo inajipanga kukuza uchumi wake kwa kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kuongeza ujuzi, kupata taarifa muhimu, na kujiimarisha katika soko la ndani na nje ya nchi.