Na BENJAMIN MASESE
KAMANDA mstaafu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema tatizo la watanzania wengi kufariki dunia inapotokea ajali majini ni kutokuwapo watu jasiri walioandaliwa katika uokoaji wa majanga ya namna hiyo.
Aliyasema hayo jana wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya uokoaji kwa kamati ya maafa ya mkoa na wilaya, wavuvi, wanafunzi na wamiliki wa boti na mitumbwi jijini Mwanza.
Kova ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya SUKOS KOVA inayojihusisha na masuala ya maafa, utoaji wa misaada ya vifaa na mafunzo ya ukoaji.
Alisema licha ya kuwapo vikosi maalumu vya uokoaji katika majanga lakini suluhisho la kupunguza au kumaliza vifo vya majini ajali inapotokea ni kutoa vifaa na mafunzo kwa wananchi wanaoishi au kuzunguka Ziwa Victoria wajue kuvitumia waweze kujiokoa wenyewe badala ya kusubiri kuokolewa.
Alisema miongoni mwa watu wanaopaswa kuandaliwa kama jasiri wa kuokoa ni wavuvi na baadhi ya watu wengine ambao maisha yao yanategemea maji na kupewa vifaa vya aina zote za majanga.
“Baada ya kustaafu niliona niendelee kuihudumia jamii ambako nilianzisha taasisi ya SUKOS KOVA.
“Kazi yetu ni kuwatumikia wananchi wa chini kwa kuwaongezea uelewa namna ya kujiokoa wakati wa ajali za majini, pia kuwapatia vifaa na kutoa mafunzo ya majanga ya moto.
“Binafsi, ajali ya MV Nyerere inihuzunisha sana hasa nilipoelezwa kwamba watu wengi walikufa wanawake wakiwa 168.
“Kuna msemo unasema ajali haiepukiki lakini nasema tunaweza kuepuka madhara kwa kuandaa watu jasiri wa uokoaji na kuwapa vifaa vyote, tatizo hatuna na hatujaandaa jasiri ambao muda wote shughuli zao majini.
Kova alisema ikiwa wavuvi watapewa mafunzo na vifaa na kutanguliza uzalendo, vifo vitokanavyo na ajali za majini vitaisha kwa sababu wao ni wazoefu wa shughuli za majini.
Aliziomba kamati za maafa za mkoa na wilaya kuandaa timu za uokoaji ambazo zitahusisha makundi mbalimbali ya watu wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk.Philis Nyimbi alisema kama Serikali imefarijika kuzinduliwa programu hiyo kwa mkoa huo na kuahidi kushirikiana kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika katika maeneo husika.
Dk.Nyimbi alisema muda wote wa mafunzo kwa makundi mbalimbali Serikali itakuwa bega kwa bega kusimamia hatua hiyo.
Vifaa mbalimbali vilivyotolewa vikiwamo boya, redio za mawasiliano, nguo za uzamiaji na vifaa vya kuzimia moto vilikuwa na thamani ya Sh milioni 120 ambavyo vitagawia katika shule, wavuvi, kamati za mafia za mkoa na wilaya.