24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

KOMBORA LA MAKONDA LAPIGA POLISI 12

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

OPERESHENI Maalumu ya kupambana na dawa za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, imeonekana kuigusa moja kwa moja Wizara ya Mambo ya Ndani.

Katika hatua ambayo pengine haikutarajiwa na wengi, operesheni hiyo imemgusa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu.

Ikiwa ni siku yake ya tatu jana, operesheni hiyo imesababisha IGP Mangu atangaze kuwasimamisha kazi askari 12 ambao majina yao yamo kwenye orodha iliyotolewa na Makonda Alhamisi na Ijumaa wiki hii.

Askari waliosimamishwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Christopher Fuime na aliyekuwa Ofisa wa Operesheni Kituo cha Osterbay, Inspekta Jacob Swai.

Wengine ni Sajenti Steven Ndasha, Sajenti Mohamedi Haima, Sajenti Steven Shaga na Koplo Dotto Mwandambo.

Wamo pia Koplo Tausen Mwambalangani, Koplo Benatus Luhaza, Koplo James Salala, Koplo Noel Mwalukuta, D/C  Gloria Massawe na D/C Fadhili Mazengo.

Wakati Makonda akilitikisa Jeshi la Polisi ambalo lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Mwigulu  Nchemba, hali iko hivyo hivyo pia mkoani Arusha ambako mwanzoni mwa wiki hii, Mkuu wake wa Mkoa, Mrisho Gambo alionekana kutoa kauli nzito kumlenga Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Wakati Maghembe akiwa tayari alikwishatangaza uamuzi wa kutenga eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa pori tengefu la Loliondo, Gambo wiki hii alitangaza kutotambua uamuzi huo na badala yake kuendelea na suluhu katika mgogoro wa eneo hilo.

Tangu wakuu hao wawili wa mikoa vijana wachukue hatua hizo kwa nyakati tofauti, mawaziri ambao maeneo yao ya kazi yameguswa, wameendelea kukaa kimya pasipo kuzungumza lolote.

Hadi kufikia jana, ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambaye alikuwa angalau ametoa kauli juu ya kile kinachoendelea kutekelezwa na Makonda katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuigusa moja kwa moja wizara hiyo.

Hata hivyo, hatua ya IGP Mangu kutangaza kuwasimamisha kazi askari 12 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowahusisha na mtandao wa dawa za kulevya, ni kielelezo cha wazi kwamba suala hilo sasa limechukua sura ya kitaifa.

Aidha kwamba Makonda na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro waliitwa Ikulu juzi, ni kielelezo kingine kwamba taarifa ya operesheni ya kupambana na dawa za kulevya aliyoianzisha mkuu huyo wa mkoa imegusa mamlaka za juu za dola.

Hilo pia linathibitishwa na kauli iliyotolewa na IGP Mangu jana katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kutangaza kuwasimamisha kazi askari hao. Alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na dawa za kulevya kwa aina yoyote.

Mangu ambaye alisema tuhuma hizo wamezichukulia kwa uzito wa kipekee, alisisitiza kuwa jeshi hilo litaendelea kuwafanyia uchunguzi askari hao kulingana na taratibu za kijeshi na baadae watafikishwa mahakamani.

“Kama Jeshi la Polisi ndiyo kiongozi na askari wake wanatuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, ni jambo tunalolichukulia kwa uzito wa pekee na kamwe hatulichukulii la kawaida.

“Kufuatia taarifa za mkuu wa mkoa, zipo hatua mbalimbali tunazochukua na tunaendelea kuchukua maana huu ni uhalifu,” alisema IGP Mangu.

Alisema ili kupambana na matukio mbalimbali ikiwamo dawa za kulevya, wananchi wanapaswa kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya uhalifu ili hatua zichukuliwe mapema.

“Hata kama ni askari wetu watabainika kujishughulisha na uhalifu, hatuwezi kumvumilia hata kidogo kwenye hili,” alisema IGP Mangu.

Alisema katika vita ya kupambana na uhalifu, askari polisi inabidi wawe wasafi kama alivyo kiongozi wa dini anayewahubiria waumini waache dhambi.

IGP Mangu alisema pamoja na tuhuma hizo za dawa za kulevya kuwakumba baadhi ya viongozi waliokuwa katika ngazi za juu za polisi, haimaniishi kuwa jeshi hilo limechafuka.

 “Jeshi la Polisi haliwezi kuchafuka kwa sababu ya kashfa ya watu wachache, watu tisa wachafue watu 47,000 kwa vigezo gani?” alihoji.

Akizungumzia wasanii, IGP Mangu alisema bado wanaendelea kuwakamata na kuwahoji, wakiwamo watu mbalimbali wanaotajwa katika mtandao huo, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

“Kama tutakavyofanya kwa askari, hivyo hivyo kwa wasanii tutafanya, tunatafuta vithibitisho tukijiridhisha na wao tunawapeleka mahakamani,” alisema IGP Mangu.

Mbali na hilo, aliwataka wananchi kutoa taarifa rasmi kwa polisi zinazowahusu wafanyabiashara wakuu wa dawa za kulevya maarufu kama ‘mapapa’ na si kuwaongelea mitandaoni.

 “Wananchi walete majina, kila jina tunalotajiwa tunalishughulikia, hao mapapa nao ni watu, wapo ambao ni wafanyabiashara wakubwa tumewahi kuwakamata na wamepelekwa mahakamani, mkisema mapapa maana mnawaweka watu walio katika mabano kwa nini hamtupi majina? Sisi kazi yetu sio ya siri, tunakamata na tutawapeleka mahakamani,” alisema IGP Mangu.

Katika operesheni aliyoianzisha wiki hii ya kupambana na dawa za kulevya, Makonda aliwakamata na kuwaweka ndani baadhi, huku akiwataja kwa majina askari polisi 12 kati ya 17, wasanii na watu mbalimbali 18.

Baadhi ya majina ya wasanii wakubwa waliotajwa katika orodha hiyo ni pamoja na Wema Sepetu, Khalid Mohamed (TID), Vanessa Mdee, Mr Blue na Chidi Benz.

Ingawa taarifa hizi hazijathibitishwa, katika msako wake, Makonda inaelezwa aliwakamata baadhi wakiwa na kete za dawa za kulevya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Masauni, alipotafutwa kuzungumzia operesheni hiyo, alikaririwa na gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi jana, akisema kuwa hawaaniki mikakati yao kwenye magazeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles